1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yahaha kufufua mazungumzo Mashariki ya Kati

17 Novemba 2010

Marekani imeahidi kuipa Israel ndege za kivita zenye thamani ya Dola bilioni tatu ili isitishe ujenzi wa makaazi.

https://p.dw.com/p/QAZ4
Baraza la Mawaziri la Israel linatarajiwa kulipigia kura pendekezo la Marekani, Jumatano wiki hii.Picha: fotolia/Westa Zikas

Leo kulikuwa mgawanyiko katika serikali ya muungano ya Israel yenye siasa za mrengo wa kulia, ikiwa ni kabla ya baraza la mawaziri kupiga kura. Kura hiyo itaamua ikiwa Israel itakubali mapendekezo ya Marekani ili isitishe ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ukingo wa magharibi wa Mto Jordan na hatimaye mazungumzo ya amani yarejewe.

Benny Begin, ambaye ni waziri anayeheshimika wa mrengo wa kulia nchini Israel, na mwanawe hayati Menachem Begin aliyeongoza jitihada za amani kati ya Israel na Misri mwishoni mwa miaka ya sabini, amekiri kwamba wanakumbwa na mgawanyiko mkubwa.

Alisema ahadi ya Marekani ya kuipa Israel ndege za kivita zenye thamani ya Dola bilioni tatu za Kimarekani, ndio ilikuwa chambo cha kidiplomasia kwa Israel ili ikubali pendekezo la kusitisha ujenzi wa makaazi kwa walowezi wa Kiyahudi katika maeneo inayodhibiti.

Naibu waziri mkuu wa Israel, Dan Meridor, amethibitisha kwamba waziri mkuu Benjamin Netanyahu anangojea kupata barua rasmi ya ahadi hiyo kutoka Marekani kabla ya baraza la mawaziri kulipigia kura wazo hilo hapo kesho.

Bw Meridor amesema ikiwa barua hiyo itaashiria yale yaliyozungumzwa na kukubaliwa kati ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani na waziri mkuu wa Israel wiki iliyopita, basi baraza la mawaziri litaipitisha.

Rais Barack Obama wa Marekani alijitahidi kuwashawishi Wapalestina warejee mazungumzo ya amani, lakini kama walivyoelezea wasiwasi wao juu ya vizingiti vya Israel, walisusia mazungumzo hayo baada ya Israel kukataa kuongeza muda wa marufuku ya ujenzi wa makaazi.

Barack Obama mit Benjamin Netanyahu und Mahmoud Abbas NO FLASH
Rais Obama akizungumza awali na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na kiongozi wa mamlaka ya ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas.Picha: AP

Wapalestina wanashuku kwamba watapendekezewa mipango ya mipaka itakayokuwa na makaazi ya Wayahudi na wakose kuifanya Jerusalem mashariki uwe mji mkuu wa taifa lao.

Kwa upande wao, Wapalestina wanadai kwamba ahadi ya Marekani ya kuipa Israel ndege za kivita ni sawa na rais Obama kuihonga Israel na anaonekana kurudi nyuma kutokana na msimamo wake kwamba ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi mashariki mwa Jerusalem na katika ukingo wa magharibi, ni haramu na lazima usitishwe.

Waziri wa ulinzi wa Israel, Ehud Barak, amesema ahadi ya Marekani inaashiria hatari ambayo Israel itachukua ikiwa itakubali kuundwe taifa la Palestina.

Mwandishi: Peter Moss /Reuters

Mhariri: Othman Miraji.