1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yahaha kukwamua mazungumzo Mashariki ya Kati

6 Oktoba 2010

Huku mkutano wa nchi za Kiarabu ukifanyika Ijumaa hii kujadili mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati, utawala wa Marekani unachacharika kuyarudishia uhai mazungumzo hayo

https://p.dw.com/p/PXRX
Rais Barack Obama wa Marekani na Mahmoud Abbas wa Palestina
Rais Barack Obama wa Marekani na Mahmoud Abbas wa PalestinaPicha: AP

Wasiwasi ni mkubwa. Ikiwa mazungumzo haya yatafeli, wachunguzi wa mambo wanasema, kuna hatari ya harakati za Intifadha kuibuka upya, katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Mashariki ya Jerusalem, ambako tayari hali ya usalama iko mashakani, kutokana na kubomolewa kwa makaazi ya Wapalestina ili kupisha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi.

Mapema wiki hii, kundi la walowezi wenye siasa kali liliuchoma moto msikiti kwenye eneo hili la Ukingo wa Magharibi. Matokeo ya kura ya maoni yaliyochapishwa baada ya hapo, yalionesha kwamba, Wapalestina wengi wanaunga mkono mashambulizi yaliyofanywa na kundi la Hamas hivi karibuni dhidi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi, ambayo yaliwaua Waisrael wanne.

Hii huenda ikawa ndio sababu inayomfanya mjumbe maalum wa Marekani katika mazungumzo ya Mashariki ya Kati, Seneta George Mitchell, kutumia ushawishi wake kwa viongozi wa nchi za Kiarabu ili nao wamshinikize Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, kurudi kwenye meza ya mazungumzo na mwenzake, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Wenyewe viongozi wa nchi za Kiarabu, wamekuwa wakijiepusha kuzungumzia chochote kabla ya Mkutano wao, unaotarajiwa kufanyika nchini Libya hapo keshokutwa, lakini viongozi wa Kipalestina wameshaweka wazi msimamo wao: Hakuna mazungumzo na Israel, bila ya kwanza Israel kusitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi.

Serikali ya Obama imeiahidi Israel mambo mengi ya manufaa kwake, lakini tu nayo Israel ikubaliane na matakwa haya ya kuzuia ujenzi huu. Makubaliano ambayo bado hayajawekwa wazi kati ya Msaidizi Maalum wa Rais Barack Obama katika Mambo ya Mashariki ya Kati, Dennis Rose, na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Ehud Barak, yanaonesha kwamba, Marekani imejikubalisha kuipatia Israel vifaa vya kijeshi, zikiwemo ndege, makombora na satalaiti; na pia kutumia nafasi yake kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kulipigia kura ya veto azimio lolote ambalo litakuwa dhidi ya Israel.

Licha ya kwamba hapo awali Netanyahu alikataa kuzipokea ahadi hizi za Marekani, hivi sasa wasaidizi wake wa karibu wanasema ameanza kufikiria uwezekano wa kuongeza muda wa kusitisha ujenzi huu, na hivyo kukubaliana na 'zawadi' za Marekani na kuyakidhi matakwa ya Wapalestina.

Inasemekana kwamba, kwa kiasi kikubwa kubadilika kwa mawazo ya Netanyahu kumetokana pia shinikizo la makundi yanayouiunga mkono Israel nchini Marekani, kama lile la Israel Lobby, ambayo yanamtaka Netanyahu akubaliane na zawadi ya Rais Obama.

Wachunguzi wa mambo wanasema, ikiwa Netanyahu atashindwa kukubaliana na 'zawadiä hii, basi atakuwa anailazimisha Marekani ikubaliane na hoja ya Rais Abbas, kwamba ramani ya mwaka 1967 ya Mashariki ya Kati iliyofanyiwa marekebisho kidogo tu, ndiyo iwe kiini cha mazungumzo. Na hilo ndilo jambo linalotakiwa na nchi za Kiarabu kwa miaka mingi sasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/IPS

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman