1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaiomba radhi Pakistan.

Halima Nyanza7 Oktoba 2010

Marekani imeomba radhi kutokana na mashambulio ya umwagaji damu iliyoyafanya nchini Pakistan, hatua ambayo nchi hiyo inatumai kuwa itahamasisha Islamabad, kufungua tena vizuizi ilivyoiweke NATO kuelekea Afghanistan.

https://p.dw.com/p/PXnw
Malori ya mafuta ya NATO yaliyounguzwa na wapiganaji nchini Pakistan.Picha: AP

Katika taarifa yake aliyoitoa mjini Isl!amabad, balozi wa Marekani nchini Pakistan Anne Pattersson aliiomba radhi nchi hiyo na familia za askari waliouawa na kujeruhiwa.

Ameongeza kuwa Jeshi la Pakistan ni washirika wao katika vita, ambavyo ni kitisho kwa nchi hizo mbili.

Pakistan ilifunga njia muhimu za jumuia ya kujihami ya NATO, kuelekea Afghanistan kufuatia  kufuatia uvamizi katika ardhi yake.

Wanajeshi wawili wa Pakistan waliuawa wiki iliyopita kimakosa baada ya ndege za NATO kufanya shambulio katika eneo la mpaka na kudhani kuwa ni wapiganaji.

Lakini uhusiano huo nyeti wa nchi hizo mbili, unaweza kuwa wa mashaka zaidi kufuatia ripoti ya Ikulu ya Marekani katika bunge la nchi hiyo, ambayo imeyaonya majeshi ya Pakistan kwa kile ilichokiita '' kuepuka mzozo wa moja kwa moja'' na wapiganaji wa Taliban wa Kiafghan pamoja na al Qaeda, ambao wote wameweka makaazi kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Ripoti hiyo inasema pia kwamba majeshi ya Pakistan yanaendelea na operesheni zake dhidi ya wapihganaji kusini mwa Waziristan, lakini imeongeza kusema kuwa  wanajeshi hao wamekuwa wakikaa zaidi barabarani na hivyo operesheni hiyo kuendelea taratibu.

Marekani inamatumaini kwamba Pakistan itakubali kuomba radhi kwake  kwa helikopta zake kufanya mashambulio na kufungua tena mpaka wa Khyber , ambao ni muhimu kwa ajili ya kupelekea wanajeshi 152,000 wa Marekani na wa NATO nchini ASfghanistan kupambana na Taliban.

Takriban matanki na malori 100 ya NATO ya kubebea mafuta,yaliharibiwa  katika shambulio lililofanywa na Taliban wiki iliyopita tangu kufungwa kwa mpaka baada ya wapiganaji walipokishambulia kituo kimoja kilichoko kwenye njia hiyo ya kuingia Afghanistan, ambako wapiganaji sasa wanatimiza mwaka wao wa 10 tangu Oktoba 7 mwaka 2001, uvamizi ulipofanyika.

Hii leo tena wafanyakazi wa kupambana na moto, kaskazini magharibi mwa Pakistan, walikuwa na kazi ya kujaribu kuzima moto uliokuwa ukiunguza malori 54 yaliyokuwa yakipeleka vitu kwa ajili ya majeshi ya NATO nchini Afghanistan.

Wapiganaji wa Taliban nchini Pakistan wameapa kufanya mashambulizi zaidi kwa lengo la kulipa kisasi, mashambulio yanayofanywa na Marekani ambayo yanawalenga wapiganaji hao wa Taliban na al Qaeda, kaskazini magharibi mwa Pakistan, kwa kuwahusisha na njama za kupanga mashambulio ya kigaidi dhini ya miji mbalimbali barani Ulaya.

Kwa upande wake, Jumuia ya Kujihami ya NATO imesema mashambulio hayo yanayofanywa na wapiganaji, hayataathiri juhudi zao za kijeshi nchini Afghanistan.

Wakati huohuo, shirika la kijasusi la Pakistan linawashinikiza wanachama wa taliban wa Afghan, kujitoa katika mazungumzo ya amani yanayoungwa mkono na Marekani ambayo yanalenga kumaliza vita nchini Afghanistan. hiyo ni kwa mujibu wa jarida la Wall street.

Likiwanukuu maafisa wa Marekani na makamanda wa Taliban, gazeti hilo limesema shirika la kijasusi la Pakistan limekuwa likiwahamasisha wapiganaji wa kiafghan kusonga mbele na mashambulio, ikiwemo kushambulia pia raia na kutokubali mazungumzo hayo ya amani ama kuacha kupigana.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri: Mwadzaya,Thelma

 .