1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaipatia misaada ya kijeshi serikali ya Libnan

Oummilkheir25 Mei 2007

Mapigano yamepungua kidogo katika eneo la kaskazini la Libnan inakokutikana kambi ya wakimbizi ya Nahr al Bared

https://p.dw.com/p/CHDl
Wapalastina wanayapa kisogo mapigano
Wapalastina wanayapa kisogo mapiganoPicha: AP

Misaada ya kijeshi ya Marekani imeanza kufika Libnan ambako jeshi limekua likipambana na wanamgambo wa Fatah al-Islam waliojificha katika kambi ya wakimbizi wa kipalastina ya Nahr al-Bared tangu jumapili iliyopita.

“Ndege nne za mizigo za jeshi la wanaanga la Marekani US AIR FORCE zimeanza kutuwa Libnan zikisheheni vifaa na zana nyenginezo za kijeshi kwaajili ya jeshi la Libnan.”Duru za kibalozi za nchi za magharibi zimesema hayo bila ya kutaja lakini lini hasa ndege hizo zimeanza kutuwa Libnan.

“Zana hizo ziliagiziwa na jeshi la Libnan ,lakini zinaharakishwa kuletwa hivi sasa kutokana na hali namna ilivyo” duru hizo zimeongeza kusema.

Kwa mujibu wa gazeti la Al Nahar la Libnan,ndege ya mwanzo ilifika jana usiku ikitokea Kuweit.Ndege nyengine mbili zinatazamiwa kuwasili hii leo zikitokea Misri na ndege zilizosalia zitafika Libnan kutoka nchi nyengine za Ghuba kunakokutikana ghala za silaha za Marekani.

Serikali ya mjini Washington imedhamiria kumpatia waziri mkuu wa Libnan Fouad Siniora msaada wa dharura wa kijeshi wenye thamani ya dala milioni 30 ili kukabiliana na wimbi la matumizi ya nguvu nchini humo.

“Tunazingatia maombi ya msaada kwa serikali ya Libnan” amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje Sean McCormack mbele ya waandishi habari.

Hakufafanua lakini kiwango cha msaada huo,lakini msemaji wa wizara ya ulinzi alizungumzia juu ya kitita cha dala milioni 30 na laki nne zitakazotumiwa kununulia zana za kijeshi,magari ya kijeshi na vipuri kwaajili ya helikopta na magari.

Nchini Libnan kwenyewe mapigano katika kambi ya wakimbizi wa kipalastina ya Nahr al Bared yamegharimu jumla ya watu 78 tangu yaliporipuka jumapili iliyopita.Jeshi la Libnan linasema limewapoteza wanajeshi wake 33 kufuatia mapigano hayo na Fatah el Islam wamepotelewa na wanamgambo 25.Wpalastina 19 na raia mmoja wa Libnan ni miongoni mwa wahanga wa mapigano hayo.

Hali inasemekana ni shuwari hii leo baada ya milio ya risasi kusikika hapa na pale jana usiku.Risasi hizo zilizofyetuliwa karibu na kambi ya Nahr el Bared ziliwafanya watu waingiwe na hofu ,makubaliano ya kuweza chini silaha yaliyofikiwa jumanne iliyopita yasije yakavunjika.

Wakati huo huo misaada ya dharura kutoka shirika la kimataifa la Msalaba mwekundu na shirika la Umoja wa mataifa la UNRWA inaendelea kupelekwa Tripoli na katika kambi ya karibu ya Baddaoui walikokimbilia maelfu ya wapalastina walioihama kambi ya Nahr al Bared.