1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitetea Israel juu ya silaha za Nyuklia

Abdu Mtullya 23 Mei 2015

Marakeni imezuia kupitishwa hati ya kimataifa juu ya kuziondoa silaha za nyuklia duniani baada ya nchi hiyo na washirika wake kulikataa pendekezo juu ya kuzipiga marufuku silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/1FVIg
Waandamanaji wapinga silaha za Nyuklia
Waandamanaji wapinga silaha za NyukliaPicha: picture-alliance/Pacific Press

Mazungumzo juu ya silaha za nyuklia yaliyohudhuriwa na wajumbe kutoka nchi zaidi ya 150 yamekuwa yanafanyika kwenye Umoja wa Mataifa kwa zaidi ya mwezi mmoja. Wajumbe hao walikutana ili kuutathmini mkataba juu ya kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia, NTP. Lengo la mkataba huo ni kuzuia kuzieneza silaha hizo na tekinolojia ya kuziundia.

Hata hivyo mazungumzo juu ya kulipitisha azimio linaloufafanua mpango wa kuutekeleza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, yaligonga mwamba baada ya nchi za kiarabu kutaka mkutano uitishwe ili kulijadili suala la kuifanya Mashariki ya Kati liwe eneo pasipo na silaha hizo.

Nchi za kiarabu zilitaka mkutano huo uitishwe mapema mwaka ujao. Lakini Marekani na washirika wake wamelipinga pendekezo hilo. Israel iliyohudhuria mazungumzo hayo kwenye Umoja wa Mataifa, ingawa haijautia saini mkataba wa kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia ililipinga pendekezo la nchi za kiarabu.

Rais wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Marekani Barrack ObamaPicha: Reuters/J. Ernst

Inaaminika kwamba Israel ndiyo nchi pekee yenye silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati lakini haijakiri kuwa na silaha hizo. Naibu Waziri wa Marekani wa udhibiti wa silaha Rose Gottemoeller amesema pendekezo la kuitisha mkutano linaenda kinyume na malengo ya muda mrefu ya nchi yake.

Gottemoeller amehoji kwamba pendekezo juu ya kupiga marufuku silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati halina matumiani ya kukubaliwa na nchi zote.

Marekani imesema Misri na nchi nyingine za kiarabu zinajaribu kuuteka nyara mchakato wa mazungumzo kwa kuiwekea Israel masharti.

Wajumbe watoa mwito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.

Wajumbe waliokutana kwenye Umoja wa Mataifa kuitathmini hatua iliyofikiwa katika kuutekeleza mkataba juu ya kupiga marufuku silaha za nyuklia walitoa mwito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuitisha mkutano mapema mwaka ujao bila ya kujali iwapo Israel na jirani zake wanakubaliana na ajenda ya mkutano. Kutokana na mkutano huo Israel inaweza kulazimika kukiri kwamba inazo silaha za nyuklia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture-alliance/dpa/Karim Kadim

Kutokana utaratibu wa kupitishwa azimio kwa ridhaa ya washiriki wote, uamuzi wa Marekani kuikataa hati iliyokusudiwa kupitishwa, maana yake ni kwamba msingi wote juu ya kuondoa silaha za nyuklia dunianina kuzuia uenezaji wa silaha hizo, umetenguliwa kwa muda wa miaka mitano ijayo baada ya wiki nne za majadiliano.

Marekani iliungwa mkono na Canada na Uingereza. Mkutano mwingine juu ya kuutathmini mkataba wa kupiga marufuku silaha za nyuklia unatarajiwa kufanyika mnamo mwaka wa 2020.

Mwandishi:Mtullya Abdu/AP

Mhariri: Amina Abubakar