1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaiwekea vikwazo Crimea

20 Desemba 2014

Wakati serikali ya Ukraine na waasi wanaotaka kujitenga wakijiandaa kwa mazungumzo mapya, serikali ya Marekani Ijumaa (19.12.2014) imeweka vikwazo zaidi dhidi ya jimbo la Crimea linalodhibitiwa na Urusi.

https://p.dw.com/p/1E85Q
Rais Barack Obama katika mkutano na waandishi wa habari wa mwisho wa mwaka Ikulu Washington.(19.12.2014)
Rais Barack Obama katika mkutano na waandishi wa habari wa mwisho wa mwaka Ikulu Washington.(19.12.2014)Picha: Reuters/K. Lamarque

Wakati serikali ya Ukraine na waasi wanaotaka kujitenga wakijiandaa kwa mazungumzo mapya, serikali ya Marekani imeweka vikwazo zaidi dhidi ya jimbo la Crimea linalodhibitiwa na Urusi.

Rais Barack Obama amepiga marufuku kusafirisha bidhaa. teknolojia au kutowa huduma katika eneo hilo lililotwaliwa na Urusi.

Rais Obama amesema katika taarifa kwamba "Marekani haitokubali hatua ya Urusi kuikalia kwa mabavu na jaribio la kuinyakuwa Crimea."

Obama pia ameiagiza Wizara ya Fedha ya Marekani kuwawekea vikwazo watu binafsi na kampuni zenye kuendesha shughuli zake katika eneo hilo wakiwemo Waukraine na Warusi 24 halikadhalika kampuni kadhaa zinazodhaniwa kuwa zinachangia kuiyumbisha Ukraine.

Shinikizo la mataifa ya magharibi

Hapo Alhamisi hatua kama hizo za vikwazo zimechukuliwa na Umoja wa Ulaya.Siku moja baadae Canada pia iliongeza vikwazo vipya vyenye kuwalenga viongozi wa waasi wanaotaka kujitenga na sekta ya mafuta na gesi ya Urusi.

Jean-Claude Juncker Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya Brussels. (18.12.2014)
Jean-Claude Juncker Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya Brussels. (18.12.2014)Picha: AFP/Getty Images/T. Charlier

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ameonya kwamba vikwazo zaidi vinavyowekwa na Marekani vinaweza kuvuruga uwezekano wa ushirikiano wa kawaida baina ya nchi hizo mbili kwa kipindi cha muda mrefu.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana Brussels hapo Alhamisi wameionya Urusi kwamba wako tayari kubakia kwenye mkondo huo wa malumbano kwa muda mrefu iwapo Rais Vladimir Putin wa Urusi atagoma kujitowa kutoka Ukraine.

Machafuko ya kiuchumi

Ikiwa ni matokeo ya vikwazo hivyo na kushuka kwa bei za mafuta Urusi hivi sasa inakabiliwa na msukusuko wa kifedha unaozidi kukua.Licha ya Benki Kuu ya Urusi kuchukuwa hatua ya kupandisha kiwango kikubwa cha riba sarafu ya Urusi rubble imeendelea kushuka thamani dhidi ya sarafu ya Euro na Dola wiki hii.

Sarafu ya Urusi ruble inayoshuka thamani.
Sarafu ya Urusi ruble inayoshuka thamani.Picha: Alexander Nenenov/AFP/Getty Images

Hapo jana sarafu hiyo imepoteza zaidi ya asilimia ishirini ya thamani yake katika kipindi cha siku moja.

Tokea kunyakuliwa kwa jimbo la Crimea hapo mwezi wa Machi Ikulu ya Irusi pia imekuja kushutumiwa kwa madai ya kuwapatia silaha na wapiganaji waasi wanaotaka kujitenga katika majimbo ya mashariki mwa Ukraine ya Donetsk na Luhansk madai ambayo serikali ya Urusi imekuwa ikiendelea kuyakanusha.

Ujerumani yaonya

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter- Steinmeir awali alielezea wasi wasi wake kwamba vikwazo viliyvowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi kuhusiana na mzozo wa Ukraine kunaweza kuzidi kuidoofisha Urusi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.Picha: picture-alliance/dpa

Waziri huyo ameonya dhidi ya kuendelea kile alichokiita "kuibana zaidi skurubu."

Matamshi ya Steinmeier yaliyochapishwa katika gazeti la kila wiki la Ujerumani Der Spiegel hapo Ijumaa yamedokeza uwezekano wa kuregeza msimamo wake katika suala la vikwazo.

Steinmeier ambaye ni mwanachama wa mshirika mdogo katika serikali ya mseto ya Ujerumani chama cha SPD amesema kwamba kuporomoka kwa thamani ya sarafu ya Urusi rubble na kushuka kwa bei za nishati kumesababisha msukosuko wa kiuchumi na kifedha nchini Urusi.

Mzozo kutodhibitika

Waziri huyo ambaye chama chake tokea jadi kimekuwa kikipendelea kuiridhiana na Urusi ameonya kwamba mzozo huo usiachiliwe kuingia hatua ya kushindwa kudhibitika.

Amekaririwa akisema "Haitokuwa kwa maslahi yetu kwamba mzozo huo ufikie hatua ya kushindwa kuudhibiti " na kuongeza kwamba "Inabidi tulizingatie hilo katika sera yetu ya vikwazo".

Steinmeier ambaye alikuwa mmojawapo wa wapatanishi wakuu katika mzozo wa Ukraine hapo Ijumaa alikwenda Kiev mjii mkuu wa Ukraine kukutana na Rais Petro Poroshenko na Waziri Mkuu wa Arseny Yatsenyuk. Amezitaka bila ya mafanikio pande zinazohusika na mzozo huo kukutana katika mji mkuu wa Belarus Minsk hapo Jumapili.

Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: Reuters/M. Zmeyev

Steinmeier amesema yoyote yule anayetaka kuipigisha Urusi magoti kiuchumi atakuwa amekosea kufikiria kwamba jambo hilo litapelekea kupatikana kwa usalama zaidi barani Ulaya.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameliambia bunge la Ujerumani hapo Alhamisi kwamba Umoja wa Ulaya haitoiwachilia Urusi ikiuke kanuni za sheria,heshima na ushirikiano na kwamba kadri lengo litakapokuwa halikufikiwa vikwazo vitaendelea kubakia.

Umoja wa Mataifa unaamini kwamba mapigano ya kila leo nchini Ukraine yameuwa zaidi ya watu 4,700 na kuwapotezea makaazi wengine milioni moja.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP,dpa,Reuters

Mwandishi : Mohammed Khelef