1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yakabidhi mkoa kwa Iraqi

Kalyango Siraj23 Oktoba 2008

Huku waziri mmoja anusurika shambulio la bomu

https://p.dw.com/p/FfUp
Askari wa Usalama wa IraqPicha: AP

Vikosi vya Marekani vilivyoko Iraq vimekabidhi usimamizi wa mkoa wa Washia wa Babil kwa utawala wa Iraq katika kile kinachoonekana kama alama ya kuwa usalama umeimarishwa.Lakini hatua hiyo imekuja huku kwingineko nchini humo mambo yakiwa si mazuri, kwani watu 11 wameuawa na wengine 22 kujeruhiwa baada ya msafara wa waziri mmoja wa Iraq kushambuliwa.Waziri amenusurika bila majeruhi.

Mtu ambae amejitolea mhanga amelibamiza gari lake lililokuwa limejaa milipuko,katika moja wa magari yaliyokuwa yanafuatana na waziri wa Leba Mahmud Jawad al-Radi ambae ni mshia.Shambulio hilo limetokea mjini Baghdad.

Msemaji wa wizara hiyo amesema kuwa waziri hakujeruhiwa ila mafisa wa usalama wanasema takriban watu 11 wamefariki na wengine 22 kujeruhiwa kutokana na mlipuko huo.Taarifa ya wizara imeongeza kuwa miongoni mwa waliofariki ni walinzi watatu wa waziri huyo.

Huku waziri huyo akiponea chupuchupu kwingineko inasemakena kuwa usalama umeirishwa. Miongoni mwa maeneo ambayo zamani yalikuwa hatari kwa usalama ni mkoa wa Kishia wa Babil.

Mkoa huo umekuwa unakabiliwa na mashambulio kadhaa ya kila mara hasahasa kwa mahujaji wa Kishia tangu uvamizi wa Marekani mwaka wa 2003.Mkoa huo umekuwa katika mikono ya majeshi ya Marekani, lakini leo umekabidhiwa kwa utawala wa Iraq.Huu ni mkoa wa 12 kati ya mikoa yote 18 ya nchi hiyo kutoka mikononi mwa majeshi ya Marekani na kukabidhiwa utawala wa Baghdad.

Maafisa wa sehemu hiyo wamepongeza mchango wa waasi wa zamani wa Kisunni ambao baadae waliungana na majeshi ya Marekani kupambana dhidi ya kundi la Al-Qaida,jambo ambalo limeboresha hali ya usalama katika mkoa huo ambao sehemu yake ya kaskazini ilijipatia jina la kupanga la 'medani ya kifo' kutokana na visa vingi vya umwagikaji damu.

Katika sherehe ya kukabidhi uongozi wa mkoa huo iliofanyika katika mji wake mkuu wa Hilla,naibu mkuu wa majeshi ya Marekani nchini Iraq,Luteni Generali Lloyd Austin, amesema kuwa mwaka mmoja uliopita,mkoa huo ulikuwa unashudia mashambulizi zaidi ya 20 kila wiki lakini sasa mashambulio yamepungua kwa asili mia 80.

Hata hivyo ameonya dhidi ya wale aliowaita,'maadui wa Iraq',na kusema kuwa baado hawajashindwa na hivyo kutoa ahadi kuwa Marekani iko tayari kuviisaidia vikosi vya wazalendo vya hapo katika kudumisha usalama.

Mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Iraq,Mowaffaq al-Rubaie amesema kuwa vikosi vya usalama vya nchi yake mda usio mrefu vitachukua usimamizi wa mkoa jirani wa Wasit kutoka mikononi mwa wanajeshi wa Marekani.

Hatua ya leo imekuja siku mbili baada ya mapigano makali katika mkoa huo kati ya wapiganaji dhidi ya wanakijiji wa kisunni yaliyopelekea watu 15 kufariki na wengine kadhaa kujeruhiwa. Hata hivyo Gavana wa mkoa huo amesema kuwa sasa ni hali ni tulivu.

Kati ya mikoa 18 ya Iraq iliosalia mikononi mwa majeshi ya Marekani ni sita;Wasit, Kirkuk, Nineveh, Salaheddin,Diyala pamoja na Baghdad.