1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

131211 USA Irak Truppenabzug

Klaus Kastan/ZPR/Mohammed Khelef13 Desemba 2011

Wiki chache kabla ya kuondoka majeshi ya Marekani nchini Iraq, Rais Barack Obama amethibitisha kuendelea kwa msaada wa nchi yake kwa serikali ya Iraq licha ya kumalizika kwa operesheni ya kijeshi.

https://p.dw.com/p/13Raf
Rais Barack Obama na mgeni wake, Waziri Mkuu Nouri al-Maliki wa Iraq.
Rais Barack Obama na mgeni wake, Waziri Mkuu Nouri al-Maliki wa Iraq.Picha: dapd

Ujumbe Rais Obama kwa mgeni wake haukuwa na shaka, nao ni kwamba "hadi kufikia mwaka ujao, vita vitakuwa vimeshamalizika nchini Iraq."

Lakini kauli ya Obama haitoki tu kwa kiongozi wa nchi, bali pia mgombea wa urais, ambaye lazima asimame mbele ya wapiga kura kwa uchaguzi wa mwakani. Na baada ya ahadi nyingi za kisiasa ambazo amezitoa ndani ya Ikulu ya Marekani na kushindwa kuzitimiza, jana Obama alisimama kwa majigambo ya kutangaza mafanikio yake, yaani mwisho wa vita vya Iraq.

"Huu ni wakati wa kurudi nyumbani. Familia nyingi za Wamarekani zinataka kuwa tena pamoja." Amesema Obama.

Obama pia ameanza kujenga ushawishi mpya wa Marekani kwa Iraq. Baina ya mataifa mawili haya huru na baada ya kuondoka kwa majeshi ya Marekani, sasa panaanza aina mpya ya uhusiano, na ambao msingi wake ni maslahi na heshima ya kila mmoja kwa mwenzake.

Obama amesema kwamba ni lazima sasa Iraq isimame kwa miguu yake yenyewe, akiyaeleza matarajio ya watu wa eneo zima la Ghuba na Mashariki ya Kati ni kuiona Iraq ikibeba hatima yake mikononi mwake na ikitatua tafauti za ndani kwa amani na kidemokrasia, licha ya tafauti za kidini na au kimadhehebu.

Majeshi ya Marekani yakijitayarisha kuondoka Iraq.
Majeshi ya Marekani yakijitayarisha kuondoka Iraq.Picha: AP

Wakati Obama alipokuwa akiyasema haya, waziri mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki, alitikisa kichwa kwa ishara ya kukubali na pia kuongeza maneno yake mwenyewe: "Hata mtu atakapolalamika kwa mengine, bado kuondoka kwa vikosi vya Marekani ni alama ya mafanikio."

Al-Maliki amesema sasa ukurasa wa kwanza wa kufanya kazi pamoja baina ya serikali hizo mbili ndani ya ardhi ya Iraq umefungwa na ukurasa mwengine umefunguliwa. Al-Maliki amesema ukurasa huo ni mwanzo wa mahusiano mapya na ya kimkakati baina ya Washington na Baghdad, ambapo ndani yake Iraq itahitaji msaada mkubwa katika kujenga taasisi zake, kiuchumi, kama vile kupatiwa mafunzo na uwezeshaji. Kuhusu hilo, Rais Obama alirudia uthibitisho wa nchi yake kwa raia wa Iraq, kwamba "Marekani itaendelea kuwa mshirika madhubuti na wa kuendelea."

Hata hivyo, Rais Obama aliyaonya mataifa mengine kutokuingilia mambo ya ndani. Bila ya kuitaja jina, hapana shaka alikusudia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo serikali ya Marekani inahofia kwamba kuondoka kwa vikosi vyake nchini Iraq, kutaliwezesha taifa hilo la Ghuba ya Uajemi kuongeza nguvu zake kwenye eneo hilo.

Mwandishi: Klaus Kastan/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji