1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yalaani shambulio la bomu mjini Beirut

25 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CxkZ
Ubalozi wa Marekani mjini Beirut umelilaani vikali shambulio la bomu la lililokuwa limetegwa ndani ya gari ambalo limewaua watu wasiopungua 10 mapema leo katika kitongoji cha Wakristo mjini humo. Taarifa ya ubalozi huo imesema shambulio hilo ni juhudi nyengine mpya kutaka kuivuruga Lebanon. Miongoni mwa waliouwawa ni Wisam Eid, kiongozi wa kikosi cha ujasusi aliyeaminiwa kuwa na mafungamano na kiongozi wa muungano unaoipinga Syria, Saad al Hariri. Eid alikuwa na jukumu katika uchunguzi wa kifo cha waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri unaoongozwa na Umoja wa Mataifa. Watu wengine kadhaa wamejeruhiwa katika hujuma hiyo iliyofanywa siku kumi baada ya bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari kuiharibu gari ya Marekani mjini Beirut. Elias Hanna, jenerali mstaafu wa jeshi la Lebanon anasema mgogoro wa kisiasa nchini Lebanon ndio uliosababisha shambulio la leo. Syria leo imelilaani shambulio hilo na kuwalaumu maadui wa Lebanon kwa kulenga kuvuruga usalama na uthabiti wa nchi hiyo. Lebanon imekumbwa na mashambulio ya mabomu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, mengi yakiwalenga wanasiasa wanaoipinga Syria pamoja na waandishi wa habari.