1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yalaani shambulizi Sudan Kusini

11 Novemba 2011

Marekani imelaani vikali shambulizi lililotokea katika kambi moja ya wakimbizi ya Yida Sudan Kusini na kusema tukio hilo ni la kikatili na kuyumbisha amani nchini humo.

https://p.dw.com/p/138vq
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: picture alliance/dpa

Marekani kupitia msemaji wa Ikulu mjini washinton, imesema shambulizi hilo dhidi ya kambi ya wakimbizi nchini Sudan Kusini ni ya kikatili  mno na kuwa inapima uwezo wa usalama wa ndani wa nchi hiyo na kusababisha vurugu baina ya nchi hizo mbili.

Kulingana na  taarifa iliotolewa na ikulu hiyo, shambulio lililokumba raia na wafanyikazi wa kutoa misaada katika kambi ya Yida ni la kinyama na wale waliohusika  na kufanya kitendo hicho wanapaswa kuadhibiwa vikali. Kambi ya Yida ni makaazi ya wakimbizi zaidi ya elfu 20.

Hata hivo sasa Merekani kupitia msemaji wake wa ikulu, imeitaka Sudan ambayo imeishutumiwa kwa kutekeleza mashambulizi hayo kuyakomesha mara moja. " Tunaomba serikali ya Sudan Kusini kutojibu mashambulizi hayo ili kutoyumbisha amani nchini humo" alisema msemaji huyo.

UN Generalsekretär Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture-alliance/ dpa

Naye katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amezitaka pande zote mbili za Sudan na Sudan kusini kurudilia mazungumzo ya amani ili kukomesha ghasia nchini humo. Ban Ki Moon amesema shambulizi hili linarudisha nyuma mazungumzo hayo ya kutafuta amani ya kudumu katika nchi hizo.

Serikali ya Khartoum imekanusha kuhusika na shambulio hilo la angani lililofanyika jana na kusababisha vifo vya watu 12 na kuwajeruhi wengine 20. Wengi wa wakimbizi katika kambi hiyo wanatokea Kusini mwa Kordofan na jimbo la Blue Nile ambapo waasi wamekuwa wakishambuliana na jeshi la Sudan tangu mwezi Juni mwaka huu.

Taban Deng gavana katika serikali ya Suda Kusini, ameishutumu Sudan kwa kutekeleza shambulio hilo, na kusema lazima Khartoum iwajibike katika hatua zake na kufuata sheria za kimataifa. Amesema wakimbizi wanapaswa kulindwa kwa kuwa wametoroka makaazi yao kutokana na ghasia, kwa hivyo hawapaswi kufuatwa kwa mashambuli katika kambi zao.

Omar el Bashir und Salva Kiir Mayardit
Rais wa Sudan Kusini Salva Kirr na mwenzake wa Sudan Omar el BashirPicha: picture-alliance/dpa

Wiki iliopita Khartoum ilitoa malamiko yake kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa kuwa Sudan Kusini inatoa silaha za kivita kwa waasi wa kusini mwa Kordofan na jimbo la Blue Nile, Jambo hilo lilikanushwa vikali na rais wa Sudan Kusini, Salva Kirr, akisema hii ni mojawapo ya njama ya Sudan kuingia katika vita vya chini kwa chini na taifa lake.

Sudan Kusini ilijitenga na kuwa taifa huru mwezi wa July mwaka huu baada ya uchaguzi uliofanyika wa kujitenga, na kuwa taifa huru kufuatia mkataba wa mani uliotiwa saini mwaka wa 2005. Mkataba huo ulivimaliza vita vya miaka mingi vya wenyewe kwa wenyewe kati ya kaskazini na kusini.

Mwandishi Amina Abubakar/ AFPE/ RTRE

Mhariri Othman Miraji