1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yalaumiwa kuvunja haki za binaadamu

13 Mei 2011

Shirika la haki za binaadamu la Amnesty International limechapisha taarifa yake ya mwaka ambayo, pamoja na mengine, inaonesha taifa la Marekani limo kwenye orodha ya nchi zinazokandamiza haki za binaadamu.

https://p.dw.com/p/11FJZ
Ripoti ya Amnesty International ya mwaka 2011
Ripoti ya Amnesty International ya mwaka 2011Picha: picture-alliance/dpa

Rikodi ya haki za binaadamu ya Marekani inatiwa doa na sio tu uendeshaji wa gereza la Guantanamo Bay na kuwepo kwake nchini Afganistan katika kile kinachoitwa "vita dhidi ya ugaidi", bali pia na matendo yanayofanyika ndani ya taifa hilo kubwa duniani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mamlaka za Marekani ziliwanyonga watu 46 mwaka uliopita, licha ya kuwepo utata wa kisheria kwenye kesi kadhaa zilizopelekea adhabu hizo. Katika jela ya Guantanamo, ripoti hiyo inasema watu 174 walikuwa kizuizini hadi mwisho mwa mwaka jana, wakiwemo watatu ambao walitiwa hatiani katika makahama za kijeshi, ambazo uendeshaji wake wa kesi haukufuata vigezo vya kimataifa.

Jela ya Guantanamo Bay
Jela ya Guantanamo BayPicha: picture alliance/dpa

Ripoti hiyo inaitaja Marekani kwamba inawashikilia mamia ya wafungwa katika kituo chake cha kijeshí cha Bagram, nchini Afganistan, kinyume na sheria na huku ikiwatesa kwa aina mbali mbali za mateso ikiwemo kuwazuia kulala na kuwaweka kwenye joto kali sana.

Kuhusiana na wimbi la mageuzi linaloyakumba mataifa ya Kiarabu hivi sasa, ripoti hiyo imetambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari, hasa kwa njia ya mtandao, lakini wakati huo huo ikaonya kwamba kuna dalili kuwa tawala zilizobakia kwenye mataifa haya zinaweza pia kutumia mtandao kuzima mwamko wa wananchi.

Katibu Mkuu wa Amnesty International wa Ujerumani, Wolfgang Grenz, amesema kwamba kinachotokea kwenye ulimwengu wa Kiarabu bado ni mchakato usiokamilika.

"Ama ikiwa wimbi la mageuzi katika ulimwengu wa Kiarabu litakuwa na mafanikio au la, bado hatuwezi kujua, maana tawala za huko zinapambana kwa nguvu pia kama wanavyopigania wanamageuzi. Uamuzi wa kuunga mkono uhuru na haki au kuzipinga umo mikononi mwa pande zote mbili." Amesema Grenz.

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria
Rais Goodluck Jonathan wa NigeriaPicha: AP

Kuhusiana na Afrika, ripoti hiyo inayataja mataifa ya Nigeria, Msumbiji, Afrika ya Kusini na Uganda, kuwa miongoni mwa nchi ambazo uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu umerikodiwa kwa mwaka uliopita. Mtendo ya mauaji na mateso kutoka vyombo vya dola ni ya hali ya juu kwenye mataifa hayo.

Ripoti hii pia inaonesha kuwa ghasia na uvunjaji wa haki za binaadamu wakati wa uchaguzi, ukiwemo ukamatwaji ovyo wa watu na ukandamizaji wa haki ya kutoa maoni, yamekuwa matukio ya kawaida katika nchi kama vile Sudan, Ethiopia, Burundi, Guinea na Cote d'Ivoire.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf