1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yanuwia kulimaliza kundi la IS kijeshi

24 Januari 2016

Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden amesema jana Jumamosi(23.01.2016) Marekani na Uturuki zitalimaliza kundi la Dola la Kiislamu kijeshi iwapo serikali ya Syria na waasi watashindwa kufikia makubaliano ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/1Hj16
Joe Biden und Ahmet Davutoglu in Istanbul
Picha: Reuters/M. Sezer

Duru ya hivi karibuni ya mazungumzo ya amani ya Syria inapangwa kuanza kesho Jumatatu (25.01.2016) mjini Geneva, lakini mazungumzo hayo yanasemekana huenda yakacheleweshwa kwa kiasi fulani kutokana na mzozo kuhusiana na nani atakuwamo katika ujumbe wa upinzani.

Makundi ya waasi yenye silaha nchini Syria yamesema jana Jumamosi yanaitwika serikali ya Syria na Urusi jukumu kwa kushindwa kwa mazungumzo ya amani kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, hata kabla ya majadiliano hayo kuanza.

Russland Syrien Luftschläge Kampfflugzeug
Ndege za kivita za Urusi katika mapambano dhidi ya kundi la IS nchini SyriaPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Kots

Suluhisho la kisiasa

"Tunafahamu kwamba inawezekana hali kuwa nzuri iwapo tutafikia suluhisho la kisiasa lakini tuko tayari, iwapo haitawezekana, kuwa na suluhisho la kijeshi katika operesheni dhidi ya kulimaliza kundi la Daesh," Biden amesema katika mkutano na waandishi habari baada ya kukutana na Waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu.

Afisa wa Marekani baadaye alifafanua kwamba Biden alikuwa akizungumzia kuhusu suluhisho la kijeshi kwa Dola la Kiislamu, na sio kwa Syria kwa jumla.

Upinzani nchini Syria unaoungwa mkono na Saudi Arabia umeondoa uwezekano wa kufanya mazungumzo hata ambayo si ya ana kwa ana hadi pale serikali ya Syria itakapochukua hatua ikiwa ni pamoja na kuzuwia mashambulizi ya anga ya Urusi.

Biden amesema yeye pamoja na Davutoglu pia wamejadili vipi washirika hao wawili wa jumuiya ya kujihami ya NATO wanaweza kuunga mkono zaidi wapiganaji waasi kutoka makundi ya Waarabu wa madhehebu ya Sunni ili kumuondoa Rais Bashar al-Assad.

Irak Krieg Kurden Peschmerga Islamischer Staat Sindschar
Eneo la Sindshar wapiganaji wa IS wakichoma mataifa kuzuwia mashambuliziPicha: Getty Images/J. Moore

Marekani imetenga darzeni kadhaa za wanajeshi maalum kusaidia waasi wanaopambana na Dola la Kiislamu nchini Syria licha ya kwamba vikosi hivyo havikuwekwa kwa lengo la kupambana katika mstari wa mbele.

Pamoja na washirika wake, Marekani pia inafanya mashambulizi ya anga dhidi ya wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu IS ambao wanashikilia maeneo makubwa nchini Syria na Iraq na inaunga mkono wapiganaji wa upinzani wanaopambana dhidi ya kundi hilo.

Mazungumzo yatafanyika

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema jana Jumamosi kwamba ana imani mazungumzo ya amani ya Syria yatafanyika, baada ya kufanya mazungumzo na mataifa ya baraza la ushirikiano katika ghuba GCC nchini Saudi Arabia.

Kerry pia alikutana mjini Riyadh na Riad Hijab, mwenyekiti wa kamati kuu ya majadiliano ya upinzani nchini Syria pamoja na wajumbe wengine wa kamati hiyo wanaowakilisha upinzani nchini humo.

Syrien Russische Luftangriffe
Mashambulizi ya ndege za Urusi katika eneo la Maaret al-NumanPicha: Reuters/K. Ashawi

"Wamejadiliana kuhusu majadiliano yajayo yanayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa kuhusiana na kipindi cha mpito cha kisiasa nchini Syria na wote wamekubaliana kuhusu haja kubwa ya kumalizika kwa ghasia zinazowakumba watu wa Syria," msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani John Kirby amesema.

Kerry pia amesisitiza umuhimu wa kuendeleza msukumo huo wa kundi la kimataifa linalounga mkono Syria , kundi la mataifa makubwa ya dunia na mataifa ya eneo hilo yanayounga mkono hudi za amani.

Baada ya mazungumzo yake na kundi la mataifa ya GCC, Kerry amesema wote katika mkutano huo wamekubaliana kwamba kundi la kutoa msaada linapaswa kukutana tena haraka baada ya kukamilika kwa duru ya kwanza ya mazungumzo ya Syria.

Raia wauwawa katika mashambulizi

Wakati huo huo, mashambulizi yanayoshukiwa kwamba yamefanywa na Urusi yamesababisha kuuwawa kwa raia 47 katika eneo la mashariki lililoharibiwa kwa vita nchini Syria jana Jumamosi, huku kukiwa na ripoti kwamba majeshi ya Marekani yanajikusanya katika kituo cha jeshi la anga kuimarisha mapambano yake dhidi ya wapiganaji wa jihadi upande wa kaskazini.

Upande wa mashariki nchini Syria , raia hao 47 waliuwawa katika shambulio la anga linaloshukiwa kuwa limefanywa na ndege za kijeshi za Urusi dhidi ya kijiji kinachoshikiliwa na wapiganaji wa jihadi.

Syrien Russische Luftangriffe
Mashambulizi ya anga ya ndege za Urusi yanashukiwa kuwauwa raiaPicha: picture-alliance/AA/M. Khder

Shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria limesema watoto tisa na wanawake wawili ni miongoni mwa watu waliouwawa mjini Kasham, mji ambao unadhibitiwa na kundi la Dola la Kiislamu IS.

Kijiji hicho kiko katika eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta nchini Syria la jimbo la Deir Ezzor, ambako kundi la IS lilitaka kusonga mbele hivi karibuni licha ya mashambulio makubwa ya anga yanayofanywa na majeshi ya Urusi na yale ya serikali.

Mashambulizi ya wiki nzima ya kundi la IS katika mji mkuu wa jimbo hilo yamesababisha karibu watu 500 kuuawa na kuzusha hofu ya mauaji ya kuhilikisha miongoni mwa wakaazi 200,000 ambao bado wanaishi katika mji huo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /rtre

Mhariri:Caro Robi