1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani Yapanga Kuiwekea Vikwazo zaidi Urusi

28 Aprili 2014

Marekani inapanga kutangaza vikwazo zaidi dhidi ya Urusi ,hatua inayotarajiwa pia kufuatwa na Umoja wa Ulaya,lengo likiwa kuitanabahisha Moscow iache kupalilia mgogoro wa Mashariki ya Ukraine

https://p.dw.com/p/1BpPk
Jengo la meya huko Kostyantynivka lalindwa na waasi wanaoelemea upande wa UrusiPicha: Reuters

Alikuwa rais Barack Obama aliyetangaza habari hizo mjini Manilla Philippines kituo cha mwisho cha ziara yake barani Asia.

Washington ilisema hapo awali awamu hii mpya ya vikwazo vinavyowekwa kutokana na kuzidi makali mzozo wa Ukraine,vitawahusu viongozi waalio karibu zaidi na rais Vladimir Putin na kwamba vizuwizi vitawekwa pia katika shughuli za usafiri katika sekta ya za usalama na teknolojia ya kimambo leo ya kijeshi.

Rais Obama anasema hatua itakayofuata ya vikwazo itahusu kwa mfano sekta ya benki na ulinzi.

Nchini Ukraine kwenyewe mzozo wa mashariki unazidi kuenea.Waasi wameliteka jengo la ofisi ya meya katika mji wa Kostiantynivka, wenye wakaazi 80 elfu karibu na Donetsk.Bendera ya "Jamhuri ya Donetsk imepandishwa katika jengo hilo na vizuwizi kuwekwa majiani.

Hali inatisha pia umbali wa kilomita 20 kutoka hapo,katika mji wa Slaviansk,ngome ya waasi wanaoelemea upande wa Urusi,licha ya kuachiliwa huru jana usiku mmojawapo wa wanataamal 12 wa kijeshi wa shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya-OSCE.

"Majadiliano yanaendelezwa pamoja na OSCE ili waachiliwe huru wataalam 11 waliosalia wa OSCE,amesema msemaji wa waasi Stella Khorocheva na kuongeza mkutano na waandishi habari huenda ukaitishwa baadae leo mchana.

Wanne kati ya wataalam hao ni wajerumani.

Ujerumani imelaani vikali kitendo cha kuwafikisha mbele ya waandishi habari wataalam hao wa OSCE.

Ukraine Donezk Pro Russland 27.4.2014
Wafuasi wa vuguvugu linaloelemea Urusi,Mashariki ya UkrainePicha: Stepanov/AFP/Getty Images

Mmojawapo wa waasi hao, Voatcheslav Ponomarev,aliyejitangaza meya wa Slaviansk,aliwataja wataalam hao wa OSCE kuwa ni "wafungwa wa vita".

Waasi wa Slaviansk wanawashikilia pia wanajeshi wa tatu wa ngazi ya juu wa Ukraine,wanaowatuhumu kuwa ni majasusi.Televisheni ya Urusi imewaonyesha wanajeshi hao wakivalia suruali kipande,namacho yao kufumbwa kwa kitambaa cha gundi.

Hali inatisha pia katika miji mengine pia ya mashariki ya Ukraine.Kituo cha televisheni cha Donetsk kinadhibitiwa tangu jana na wanamgambo wanaoelemea upande wa Urusi.

Nchi za Magharibi zapanga kutangaza vikwazo zaidi

Nchi za magharibi zinaituhumu Urusi kupalilia kichini chini mzozo wa mashariki ya Ukraine na kubuni hali kama ile iliyopelekea kumezwa raas ya Crimea mwezi uliopita.

Russland Sanktionen G7
Mataifa saba tajiri kiviwanda-G7 yakitangaza vikwazo dhidi ya UrusiPicha: Jerry Lampen - Pool/Getty Images

Baada ya Marekani,Umoja wa Ulaya pia unatarajiwa kutangaza hatua kali dhidi ya Urusi ili kuitanabahisha nchi hiyo ibadilishe msimamo wake.

Nchi za magharibi zinahofia pia nyendo za wanajeshi wa Urusi katika mpaka wa magharibi ambako Moscow inasemekana imekusanya wanajeshi 40 elfu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp/Reuters

Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman