1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasaini mkataba wa silaha

Admin.WagnerD26 Septemba 2013

Marekani imeutia saini mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kudhibiti biashara ya kimataifa ya silaha, huku utawala wa rais Barack Obama ukituliza hofu kuwa mkataba huo utakiuka haki za kikatiba za Wamrekani.

https://p.dw.com/p/19p3a
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry akisaini mkataba wa kimataifa wa kudhibiti biashara ya silaha duniani.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry akisaini mkataba wa kimataifa wa kudhibiti biashara ya silaha duniani.Picha: picture alliance/AP Photo

Marekani imeutia saini mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kudhibiti biashara ya kimataifa ya silaha, huku utawala wa rais Barack Obama ukituliza hofu kuwa mkataba huo utakiuka haki za kikatiba za Wamrekani.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry ambaye alisaini Mktaba huo siku ya Jumatano, alisema hiyo ilikuwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha usalama wa dunia, na kuwazuia magaidi na makundi mengine kupata silaha. Hatua hii ya utawala wa rais Obama inaonekana kuwa ya muhimu katika kufanikisha mkataba huo. Marekani ilikuwa nchi ya 91 kusaini, lakini mkataba huo hautaanza kufanya kazi hadi uridhiwe na mataifa 50. Mataifa sita tu ndiyo yalikuwa yameuridhia kufikia siku ya Jumatano.

Mataifa mengi yanayoongoza duniani kwa uuzaji wa silaha bado hayajasaini, na upinzani katika bunge la seneti la Marekani, likiungwa mkono na chama cha wamiliki wa silaha nchini humo NRA, unamaanisha kuwa uridhiaji wa mkataba huo nchini Marekani utakuwa mgumu sana. Theluthi mbili ya wabunge wa baraza hilo, linalodhibitiwa kwa wingi mdogo na chama cha rais Obama cha Democrats zinahitajika ili kuridhia mktaba huo.

Akijibu hoja za wakosoaji kuwa mkataba huo utakiuka haki za Wamerakani kumiliki silaha, waziri John Kerry alisema hoja hizo hazina ukweli wowote, kwa sababu mkataba huo haudhibiti uuzaji wa silaha ndani ya Marekani, na kufafanua kwamba hautaondoa uhuru wa mtu yeyote, na kwamba unaheshimu uhuru wa watu binafsi na mataifa kupata, kumiliki na kutumia silaha kwa malengo yaliyo halali.

Makamo wa rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa chama cha wamiliki wa silaha nchini Marekani NRA, Wayne LaPierre. NRA inapinga Marekani kujiunga na mkataba wa kudhibiti silaha duniani.
Makamo wa rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa chama cha wamiliki wa silaha nchini Marekani NRA, Wayne LaPierre. NRA inapinga Marekani kujiunga na mkataba wa kudhibiti silaha duniani.Picha: AP

Moja wa maseneta wahafidhina katika kamati ya mahusiano ya nje, Bob Corker alielezea wasiwasi juu ya mkataba huo, aliosema unaacha maswali mengi ya kikatiba na kisheria bila majibu, na aliuuonya utawala katika barua aliyomuandikia rais Barack Obama siku ya Jumanne, dhidi ya kuchukua hatua zozote kutekeleza mkataba huo hadi uridhiwe na baraza la Seneti.

Italia yawa ya kwanza kuuridhia barani Ulaya

Nchini Italia, bunge lilipiga kura na kuuridhia mkataba huo, hatua ambayo ilisifiwa na mbunge wa chama cha mrengo wa kushoto cha Democratik, Silvana Amati. Amati alisema Italia, ambayo ndiyo nchi ya kwanza katika umoja huo kuridhia mkataba huo, inaweza kuyatia msukumo mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya kuuridhia pia. Italia ndiyo nchi ya nane kwa uuzaji wa silaha duniani kwa mujibu wa Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa amani ya mjini Stockholm, ambayo inatunza data kuhusiana na biahsra hiyo.

Silaha za nchi hiyo, mizinga na helikopta za mashambulizi vinasifiwa hasa, na huko nyuma imewahi kuuza silaha kwa kiongozi wa Libya alieondolewa Muammar Ghadafi, na rais wa Syria Bashar al-Assad. Baraza la Umoja wa Mataifa lenye mataifa wanachama 193 liliidhinisha mkataba huo April 2 kwa kura 154 dhidi ya 3, ambapo Urusi, China, India na nchi nyingine 20 zilijizuwia kupiga kura.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre,ape,afpe.

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman