1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasaka azimio jengine Syria

Mohammed Khelef
13 Machi 2018

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linasaka azimio jengine la kusitisha mapigano ya Syria likiongozwa na Marekani, baada ya azimio lililoongozwa na Urusi kushindwa na mashambulizi kuendelea maeneo mbalimbali.

https://p.dw.com/p/2uDwH
USA UN-Sicherheitsrat US-Botschafterin für die UN Nikki Haley
Picha: picture-alliance/dpa/AA/A. Ozdil

Licha ya kupitishwa kwa Azimio 2401 la tarehe 24 Februari, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja huo kwamba hali nchini Syria haikuwahi kuwa na afadhali yoyote, na badala yake mauaji yameendelea sio tu Ghouta Mashariki, ambako azimio hilo lililenga, bali pia Afrin, sehemu kadhaa za Idlib hadi ndani ya mji mkuu, Damascus, na viunga vyake. 

"Azimio lilitaka pande zote kujiondoa kuyazingira maeneo yanayokaliwa na raia, ikiwemo Ghouta Mashariki, Yarmouk, Fu'ah, na Kefriya. Hadi sasa hakuna mzingiro ulioondolewa. Azimio lilitaka kuondolewa watu kwa ajili ya matibabu. Lakini hakuna hata mgonjwa wala majeruhi aliyehamishwa," alisema Guterres ambaye alilitolea wito Baraza hilo kuwa halipaswi kuvunjika moyo.

Kwa mujibu wa Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, azimio hilo lililosimamiwa na Urusi lilishindwa kufanya kazi kwa kuwa watekelezaji wakubwa, zikiwemo Urusi, Iran na serikali ya Syria, hawakuwa na dhamira njema.

Ndio maana sasa Marekani inatayarisha azimio jengine ambalo litakuwa halitoi nafasi ya kuvunjwa na mataifa hayo ambayo yanatumia kisingizo cha kupambana na magaidi.

Urusi, Syria zapinga

Hata hivyo, Urusi na Syria zinashutumu Marekani na washirika wake kuwa kikwazo kwa azimio hilo la awali kwa kulikopotosha kwamba lilikuwa kwa ajili ya kusitisha mapigano kote, badala ya kuandaa mazingira ya kuweka silaha chini kwa pande zote. 

Vikosi vya Uturuki vikiingia mji wa Afrin nchini Syria.
Vikosi vya Uturuki vikiingia mji wa Afrin nchini Syria.Picha: picture-alliance /AA/H. Al Homsi

Balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa, Bashar Ja'afari, aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa pendekezo hilo la Marekani ni ushahidi mwengine wa uingiliaji kati usio na manufaa unaofanywa dhidi ya nchi yake.

"Nimemsikiliza balozi wa Marekani, ambaye kwa mara nyengine anazidisha shutuma zake dhidi ya nchi yangu, akisema kuwa nchi yake itaendesha operesheni dhidi ya nchi yangu, bila kuzingatia uhalali wa kimataifa, kama vile ambavyo walifanya mwaka jana kwa kuushambulia kwa mabomu uwanja wa ndege za kijeshi wa al-Shayrat."

Uturuki yaizingira Afrin

Hayo yakiripotiwa, jeshi la Uturuki likishirikiana na makundi ya waasi linaoyaunga mkono nchini Syria, limeuzingira mji wa Afrin ulio kaskazini mwa nchi hiyo. Mji huo unadhibitiwa na wanamgambo wa Kikurdi wa kikosi cha YPG.

Taarifa ya la Uturuki iliyotoewa Jumanne (Machi 13) ilisema mzingiro huo ni sehemu ya operesheni yake iliyoanza tarehe Januari 20 inayodhamiria kuliondoa kundi la YPG kutoka mkoa wa Afrin.

Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu la Syria lenye makao yake Uingereza, linasema kuwa raia wapatao 2,000 tayari wameshaukimbia mji huo, wakikimbia mji wa Nabul unaodhibitiwa na vikosi vitiifu kwa serikali ya Bashar Assad.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman