1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yashambulia Afghanistan

Sekione Kitojo
14 Aprili 2017

Jeshi la Marekani jana (13.04.2017)lilishambulia mfumo wa njia za ardhini za kundi la IS nchini Afghanistan, kwa kile ilichokiita "mama wa mabomu yote" bomu kubwa kabisa duniani licha ya kwamba sio silaha za kinyuklia

https://p.dw.com/p/2bEJA
GBU-43/B Massive Ordnance Air Blast bomb
Bomu kubwa kabisa duniani lenye tani 11 lilidondoshwa nchini Afghanistan Picha: picture-alliance/DoD/Newscom

Bomu  hilo  halijawahi  kutumika  kabisa  katika mapambano ya  jeshi  la  Marekani , wamesema  maafisa  wa wizara  ya   ulinzi , Pentagon. Wapiganaji 36 wa  kundi  la  Dola  la Kiislamu  waliuwawa  katika  shambulio.

Bomu  hilo , linalofahamika  kama  GBU-43B , ama  silaha  kubwa kabisa  ya  kushambulia  toka  angani, lina nguvu za  tani  11  za miripuko . Lilipotengenezwa  katika  miaka  ya  mwanzo  ya  2000, wizara  ya  ulinzi  Pentagon ,  lilifanya  mapitio  ya  uhalali  wake rasmi  wa  kutumika  katika  mapambano.

USA Bombe GBU-43/B in Florida
Bomu la MOAB ambalo lina tani 11 za miripukoPicha: picture-alliance/AP Photo/Northwest Florida Daily News/M. Kulaw

Wizara  ya  ulinzi  ilisema  haina  makadirio  ya  vifo  ama  uharibifu unaoweza  kusababishwa  na  shambulio  la  bomu  hilo, ambalo  rais wa  Marekani  Donald Trump  ameliita lililofanikiwa  kabisa. Lakini imesema  katika  shambulio  hilo, wapiganaji  36  wa  kundi  la  Dola la  Kiislamu  waliuwawa  , lakini  hakuna  raia  wa  kawaida aliyeuwawa, na  kuongeza  kwamba  mahandaki  kadhaa  ya  IS pamoja  na  silaha  vimeharibiwa.

Makao  makuu  ya  jeshi  la  Marekani  mjini  Kabul  yamesema katika  taarifa  kwamba  bomu  hilo  lilidondoshwa  majira  ya  saa  za mchana  saa  za  Afghanistan jana  katika  mfumo  wa  njia  za  chini ya  ardhi zilizochimbwa  na  wapiganaji   katika  wilaya  ya  Achin katika  jimbo  la  Nangarhar, ambako  kundi  linalohusiana  na  Dola la  Kiislamu  wamekuwa  wakifanya  shughuli  zao.

 Shambulio  hilo  lililenga  eneo  karibu  na  mpaka  na Pakistan.Mshauri  mwandamizi wa  taasisi  ya  mikakati na  mitaala ya  kimataifa  katika  mpango  wa  usalama  wa  kimataifa, Mark F. Cancian   kuhusu shambulio  hilo  amesema.

"Tuliona baadhi  ya  taarifa  za  habari  kwamba  kulikuwa  na  mfuko wa  njia  za  chini  ya  ardhi  nchini  Afghanistan  na  Marekani ilishambulia  kwa  silaha  maalum , kile  kinachojulikana  kama  MOAB , bomu  kubwa  linaloweza kuvunja  kutoka  angani."

USA Statement Donald Trump zum Luftangriff auf Syrien
Rais wa Marekani Donald Trump Picha: Reuters/C. Barria

Marekani  inakadiria  kwamba  wapiganaji 600  hadi  800  wa  kundi la  IS  wapo  nchini  Afghanistan , hususan  katika  jimbo  la Nangarhar. Marekani  imekuwa  ikielekeza  nguvu  zake  nyingi katika  kupambana  nao  wakati  huo  huo  kuyasaidia  majeshi  ya Afghanistan  kupambana  na  kundi  la  Taliban.

USA Bombe GBU-43/B in Florida
Bomu la MOAB likidondoshwa katika eneo lililolengwaPicha: picture-alliance/ZUMA Wire/US Air Force

 Ni  wiki  iliyopita  tu  mwanajeshi  wa  kikosi  maalum  cha  jeshi  la Marekani , staff sajini  Mark R. De Alencar , mwenye  umri  wa miaka  37  akitokea  Edgewood , maryland , aliuwawa  katika mapambano  katika  jimbo  la  Nangarhar.

Bomu  hilo  la MOAB  ni  silaha  iliyotengenezwa  maalum kwa  ajili ya  jeshi  la  anga  ambayo  ilikuwa  imehifadhiwa  tu  katika hazina ya  silaha  kwa   zaidi  ya  muongo  mmoja  lakini  haikutumika  katika mapambano, licha  ya  kuwa  ilikuwapo  wakati  wote  wa  vita vya Iraq.

Mark F. Cancian  anaelezea  kwa  nini  silaha  hiyo  imetumika   hivi sasa.

Afghanistan Überflutungen in der Nähe von Herat
Maeneo ya milima ya Afghanistan Picha: DW/S. Tanha

"Nafikiri  kuna  mambo  yanaendelea  katika  maeneo  mawili. Kwanza  huu  ulikuwa  uamuzi  wa  mbinu  ya  kijeshi. Unakuwa  na lengo  kama  hili muhimu, njia  za  chini  ya  ardhi  zilizoko  katika kina  kirefu  na  kisha  una  hii  silaha  ambayo  imeundwa  kwa  ajili ya  kushambulia maeneo  maalum kama  hayo, kwa  hiyo  nadhani kwa  jeshi  lilikuwa  suala  la  eneo  ambalo  si  la  kawaida kushambulia kwa  silaha  maalum.

Katika mapitio  yake  ya  mwaka  2003 kuhusiana  na  uhalali  wa matumizi  ya  MOAB , wizara  ya  ulinzi  ya  Marekani  Pentagon ilitoa  hitimisho kwamba  haiwezi  kuitwa  silaha  ya  maandangamizi chini  ya  sheria  ya  mapambano  ya  silaha.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / APE

Mhariri: Caro Robi