1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yataka washukiwa wa mashambulio ya Septemba 11 wahukumiwe kifo

12 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D6Q6

Jeshi la Marekani limesema litaitaka mahakama iwahukumu kifo wafungwa sita wa jela ya Guantanamo Bay kwa tuhuma za kuhusika katika mashambulio ya tarehe 11 mwezi Septemba mwaka wa 2001 katika miji ya New York na Washington nchini Marekani.

Mtaalamu wa sheria wa wizara ya ulinzi ya Marekani anayeshughulikia mahakama za kijeshi, Thomas Hartmann, amesema wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, inawashutumu washukiwa hao kwa mauaji, kuwashambulia raia na kufanya njama.

Mashtaka hayo ambayo ni ya kwanza kwa wafungwa wa jela ya Guantanamo yanayohusiana moja kwa moja na mashambulio ya Septemba 11, yanatarajiwa kusikilizwa na mahakama ya kijeshi, jambo ambalo limezusha utata.

Miongoni mwa washukiwa hao ni Khalid Sheikh Mohammed, ambaye inasemekana alipanga mashambulio hayo.

Raia huyo wa Pakistan aliyezaliwa nchini Kuwait, amekiri kwamba alipanga kila hatua ya mashambulio ya mwaka wa 2001.

Hata hivyo, kukiri kwake huenda kukaleta matatizo kwa kuwa shirika la ujasusi la Marekani, CIA, limekubali kuwa lilitumia mbinu ya kuwamwagia maji washukiwa wakati walipokuwa wakihojiwa.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameikosoa njia hiyo ya kuwahoji washukiwa yakisema ni mateso dhidi ya wafungwa.