1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yatoa msaada

MjahidA23 Januari 2013

Maafisa kutoka Marekani wamesema hatua ya nchi hiyo kusafirisha vikosi vya Ufaransa mjini Bamako inaweza kuendelea kwa wiki nyengine mbili zijazo.

https://p.dw.com/p/17Q54
Ndege ya Kijeshi ya Marekani
Ndege ya Kijeshi ya MarekaniPicha: picture-alliance/dpa

Jeshi la Marekani limeweka kati ya watu 8 hadi 10 katika uwanja wa ndege wa Mali, kusaidia katika ndege zinazoingia na kutoka mjini Bamako hadi pale wanajeshi wote watakaposafirishwa mjini humo.

Tayari ndege tano za Marekani zimewasili Bamako na kuwapeleka takriban wanajeshi 80 wa Ufaransa mjini humo pamoja na tani 124 za vifaa vya kijeshi. Hata hivyo Marekani haitoi msaada wa moja kwa moja kwa wanajeshi wa Mali kwa sababu serikali iliyoteuliwa kidemkorasia nchini humo ilipinduliwa mwezi Machi mwaka jana na wanajeshi walioasi.

Ufaransa ilio na wanajeshi 2,500, iliingia Mali Januari 11 mwaka huu kupambana na waasi kaskazini mwa nchi hiyo. Vikosi hivyo vikishirikiana na vile vya serikali ya Mali kwa sasa vimefanikiwa kuikomboa miji ya Diabaly, Konna na Doutenza iliyokuwa inadhibitiwa na waasi.

Wanajeshi wa Ufaransa
Wanajeshi wa UfaransaPicha: Reuters

Vikosi vya nchi hizo mbili Mali na Ufaransa vinaendelea kusonga mbele kuingia katika miji zaidi inayodhibitiwa na waasi ili kuiokomboa na kuirudisha mikononi mwa serikali ya Mali.

Japan kufunga ubalozi wake, Mali

Huku hayo yakiarifiwa, Japan imesema huenda ikaufunga ubalozi wake nchini Mali kwa hofu ya kutokea ghasia zaidi. Kulingana na taarifa iliyotoka katika wizara ya mambo ya nchi za nje ya Japan, wafanyakazi wote wa ubalozi huo wataendelea kufanya kazi katika ubalozi wake nchini Ufaransa.

Taarifa hiyo imesema wafanyakazi wote wataondoka mjini Bamako ifikapo Januari 27 pindi maandalizi ya kuondoka yatakapokamilika. Habari hii imekuja siku moja baada ya nchi hiyo kutangaza kuwa raia wake 7 walikufa katika nchi jirani na Mali, Algeria, kufuatia mzozo wa mateka katika kiwanda cha gesi nchini humo.

Waasi nchini Mali
Waasi nchini MaliPicha: dapd

Wakati huo huo, wachambuzi wa siasa nchini Chad wanasema rais wa nchi hiyo, Idriss Deby, anaonekana kuwa tayari kabisa kutuma kikosi kikubwa cha wanajeshi nchini Mali kusaidia kupambana na waasi.

Hata hivyo taarifa kutoka kwa maafisa wa Chad, zinasema kikosi hicho kilicho na mafunzo ya hali ya juu ya kijeshi, kilicho na vifaa vya kutosha pamoja na uzoefu mkubwa wa vita vya jangwani, hakitajiunga rasmi na mpango wa kimataifa wa kuisaidia Mali ambao utakuwa na wanajeshi zaidi ya 4,000 walioombwa na mataifa ya magharibi.

Rais wa Chad Idriss Deby
Rais wa Chad Idriss DebyPicha: AP

Lakini kitakuwa ardhini kikifanya kazi na kikosi ambacho kitakuwa kikioongozwa na Nigeria. Watafanya kazi pia na vikosi vya Ufaransa ambavyo viliingilia kati katika kuwafurusha waasi kaskazini mwa Mali.

Mwandishi Amina Abubakar/AP/AFP

Mhariri Josephat Charo