1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yawasihi waafrika wamshinikize Gaddafi ang'atuke

10 Agosti 2011

Wanadiplomasia wa Marekani wako Afrika kuwasihi viongozi wa bara hilo wamshinikize Muammar Gaddafi aondoke madarakani katika wakati ambapo serikali ya Libya inailaumu NATO kuwauwa raia 85.

https://p.dw.com/p/12Dw2
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary ClintonPicha: dapd

Balozi wa zamani wa Marekani nchini Libya Gene Cretz na afisa mmoja wa ngazi ya juu wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Donald Yamamoto wamewasili katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa tangu jumatatu iliyopita.

"Wanadiplomasia hao wamekwenda Afrika kwa lengo la kuzungumza na wanachama wa Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa Libya na umuhimu wa kumuona Gaddafi aking'oka madarakani-" amesema hayo msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Mark Toner mjini Washington.

Wanadiplomasia hao wawili wameshazungumza na waziri mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi na walipangiwa kuonana na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Jean Ping kabla ya kuondoka Addis Ababa hapo jana.Walizungumza pia na kiongozi wa pili wa waasi wa Libya,Mahmoud Djibril ambae pia yuko ziarani nchini Ethiopia.

Libyen Machthaber Gaddafi TV Auftritt Vertreter Stämme
Kiongozi wa Libya Muammar GaddafiPicha: dapd

Marekani imeliruhusu baraza la mpito lililoundwa na waasi nchini Libya kukalia kukalia ubalozi wa Libya mjini Washington.Ubalozi huo ulifungwa na serikali bya Washington tangu March kumi iliyopita.Marekani imelitambua baraza la mpito la waasi kuwa ndio" uongozi halali unaodhibiti serikali nchini Libya".

Wakati huo huo serikali ya Libya imeituhumu jumuia ya kujihami ya NATO kuwauwa watu 85 madege yake ya kivita yalipotupa mabomu katika kijiji cha mashariki ,umbali wa kilomita kama 10 hivi kusini mwa mji unaogombaniwa wa Zliten.

Msemaji wa serikali ya Libya,Musa Ibrahim anasema:

"Raia 85,ikiwa ni pamoja nawaatoto 35,wanaume 20 na wanawake 32 wameuliwa,na bado tunaendelea kuhesabu idadi ya wahanga wa mashambulio makali ya madege ya Nato dhidi ya mji wa Majr."

Libyen Trümmer Ruinen Zliten 04.08.2011
Magofu ya jengo lililoripuliwa na NATO karibu na ZlitanPicha: dapd

Jumuia ya kujihami ya NATO imekiri madege yake yamehujumu majengo mawili ya shughuli za kilimo yanayotumiwa,inasema kwa masilahi ya kijeshi."Hatuna ushahidi bado kama raia wameuwawa."amesema msemaji wa jumuia ya NATO Roland Lavoie.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Afp

Mhariri:Abdul-Rahman