1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yazishambulia ngome za IS Libya

Caro Robi2 Agosti 2016

Ndege za kijeshi za Marekani zimezishambulia ngome za wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la Dola Kiislamu IS katika mji wa Sirte nchini Libya kufuatia ombi la serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/1Ja19
Picha: Reuters/G. Tomasevic

Mashambulizi hayo ya angani yaliyofanywa hapo jana yametajwa na maafisa wa Marekani kuwa mwanzo wa kampeni kabambe dhidi ya wanamgambo hao wa IS mjini Sirte.

Akihutubia kupitia kituo cha televisheni cha serikali, Waziri mkuu wa Libya Fayez Serraj amesema mashambulizi ya kwanza yalilenga maeneo maalum yanayodhibitiwa na IS na kusababisha hasara kubwa kwa majihadi hao.

IS inaudhibiti Sirte tangu mwaka jana

Tangu mwezi Mei, majeshi tiifu kwa serikali ya muungano ya Libya yamekuwa yakipambana dhidi ya IS mjini Sirte, mji alikozaliwa aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi.

Waziri mkuu wa Libya Fayez Serraj
Waziri mkuu wa Libya Fayez SerrajPicha: Getty Images/AFP/Str

Wanamgambo hao waliiudhibiti mji huo wa pwani mwaka jana na kuifanya ngome yao kubwa zaidi nje ya Syria na Iraq, lakini sasa wanazingirwa katika maeneo muhimu mjini humo.

Waziri Mkuu Serraj amesema wameamua kushiriki katika muungano wa kimataifa unaopambana dhidi ya IS na kuiomba Marekani kuisaidia kwa kufanya mashambulizi ya angani dhidi ya maeneo maalum yanayodhibitiwa na IS.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Peter Cook amesema mashambulizi hayo ya Jumatatu yaliyoidhinishwa na Rais wa Marekani Barack Obama yaliharibu kifaru na magari mawili ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu.

Cook amesema katika siku za usoni kila shambulizi litakuwa ni kwa ushirikiano na serikali ya muungano wa kitaifa ya Libya na itahitaji idhini ya kamanda wa jeshi la Marekani anayesimamia vikosi vilivyoko Afrika.

Hili ni shambulizi la tatu la angani lililofanywa na Marekani dhidi ya wanamgambo walioko Libya lakini maafisa wa Marekani wamesema shambulizi la jana linaashiria mwanzo wa kampeni kali ya mashambulizi ya angani.

Marekani yanuia kurejesha usalama Libya

Ikulu ya rais wa Marekani imesema msaada kwa Libya utakuwa tu ni mashambulizi ya angani na kutoa taarifa za kijasusi kama sehemu ya mipango ya kurejesha uthabiti na usalama Libya.

Mpiganaji mtiifu kwa serikali ya Libya akiyatoroka mapigano Sirte
Mpiganaji mtiifu kwa serikali ya Libya akiyatoroka mapigano SirtePicha: Reuters/G. Tomasevic

Kukombolewa kwa mji wa Sirte ulioko kilomita 450 mashariki ya mji mkuu Tripoli, kutakuwa ni pigo kubwa kwa IS ambao wanakabiliwa pia na changamoto kubwa za kuendelea kuyadhibiti maeneo makubwa Syria na Iraq. Juhudi za kuukomboa mji huo zimesababisha vifo vya takriban wanajeshi 280 wa Libya na kuwajeruhi zaidi ya 1,500.

Kulingana na ripoti iliyowasilishwa na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita, kuna kati ya wapiganaji 2,000 na 5,000 wa IS katika miji ya Sirte, Tripoli na Derna wanaotokea Libya, Tunisia, Algeria, Misri, Mali, Morocco na Mauritania.

Marekani ilishiriki katika mashambulizi ya mwaka 2011 yaliyopelekea kuondolewa madarakani na hatimaye kuuawa kwa Gaddafi na tangu wakati huo nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imekumbwa na msukosuko mkubwa na kuingiliwa na makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Gakuba Daniel