1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maridhiano nchini Madagascar yakabiliwa na kikwazo kipya

8 Oktoba 2009

Ravalomanana asema Rajoelina asiwe mgombea urais 2010.

https://p.dw.com/p/K24K
Mpatanishi wa mgogoro huo kwa niaba ya Umoja mataifa Joachim Chissano.Picha: AP

Nchini Madagascar licha ya pande za kisiasa zinazohasimiana kukubaliana kuundwa serikali ya mseto itakayokiongoza kisiwa hicho katika kipindi cha mpito hadi uchaguzi mwakani, kumetokeza dalili kwamba mustakbali wa kisiasa kisiwani humo ni tete. Makubaliano hayo yaliofikiwa Jumanne iliopita juu ya kugawana madaraka yanakabiliwa na kikwazo .

Ishara za matatizo mapya:

Tayari kuna ishara za kuzuka matatizo mengine.Kambi ya Marc Ravalomanana Kiongozi aliyeangushwa na Andry Rajoelina, kufuatia vuguvugu la wapinzani lililoungwa mkono na jeshi, inasema wanakubaliana na yaliofikiwa ili mradi tu Rajoelina hatokuwa mgombea Urais katika uchaguzi wa rais mwishoni mwa mwaka ujao 2010 ili kutoipa uhalali serikali ilioingia madarakani kinyume cha katiba ambayo chanzo chake ni yeye binafsi. Ikaonya kwamba kama si hivyo makubaliano hayo yatakuwa ni batili.

Marc Ravalomanana Präsident Madagaskar
Rais aliyeangushwa Marc Ravalomanana .Picha: AP

Rai ya mjumbe wa umoja wa Afrika:

Mjumbe wa Umoja wa Afrika katika mazungumzo ya upatanishi Ablasse Ouedraogo hata hivyo anasema muhimu kuhusiana na makubaliano ya Maputo ni kuwepo kwa rais wa mpito bila kujali nafasi yake katika uchaguzi ujao. Wadadisi wanasema msimamo usio wazi kuhusiana na hali ya baadae ni kikwazo katika kuleta suluhisho la kudumu la mgogoro wa kisiasa nchini Madagascar.

Makubaliano hayo kimsingi yanamaanisha kuwa vizingiti vilivyokuweko kwa miezi miwili iliopita sasa vimekiukwa. Ili kuyapa msukumo makubaliano hayo yaliofikiwa chini ya upatanishi wa rais wa zamani wa Msumbiji Joachim Chissano katika mji mkuu wa Msumbiji Maputo,ikatangazwa kwamba viongozi wa pande zinazohusika, rais wa sasa Andry Rajoelina, mtangulizi wake aliyeangushwa kwa msaada wa jeshi na kuwa chanzo cha mgogoro huu Marc Ravalomanana na marais wawili wa zamani Didier Ratsiraka na Albert Zafy huenda wakakutana mjini Geneva au Paris.

Kambi ya Ratsiraka yatoa Waziri mkuu:

Eugene Mangalaza, msomi na mbunge wa zamani ambaye jina lake liliwasilishwa na kambi ya Ratsiraka amepata uungaji mkono mkubwa wa kuwa Waziri mkuu wa mpito akichukuwa nafasi ya Monja Roindefo ambaye kutokana na uaminifu wake kwa kambi ya Rajoelina hakuweza kukubaliwa na pande nyengine.

Madagaskar Unterstützer von Oppositionsführer Andry Rajoelina feiern
Andry Rajoelina anayeungwa mkono na jeshi anabakia kuwa rais.Picha: AP

Chini ya makubaliano hayo Rajoelina kiongozi mwenye umri mdogo kabisa na mcheza muziki wa zamani DJ,atabakia kuwa Rais.

Wito wa Ban Ki-moon:

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon amezitaka pande zote husika nchini Madagascar kuyaheshimu makubaliano ya kuundwa serikali ya mpito, yaliofikiwa chini ya upatanishi wa Bw. Chissano. Aliwataka viongozi wa kisiasa kuhakikisha kipindi hicho cha mpito kinaleta mafanikio na kuwa Umoja wa mataifa unasimama bega kwa bega na wananchi wa Madagascar na katika juhudi hizo za upatanishi.

Mtandao mmoja wa binafsi nchini Madagascar Sobika.Com ulikuwa na maoni yanayoungwa mkono na wengi miongoni mwa Wamalagasi kwamba historia imeonyesha kwamba makubaliano yoyote huwa ni machungu kidogo kwa upande mmoja au mwengine, lakini mwishowe lazima paweko na maridhiano.

Mwandishi:Mohamed Abdul-Rahman/AFP

Mhariri: Hamidou Oummilkheir