1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marina Silva kuamua hatima ya urais wa Brazil

5 Oktoba 2010

Matokeo ya uchaguzi mkuu wa wa Jumamosi nchini Brazil yanampa nafasi mgombea aliyeshika nafasi ya tatu, Marina Silva, kuamua nani awe rais baada ya uchaguzi wa mrudio wa Oktoba 31

https://p.dw.com/p/PVXS
Mgombea aliyeshika nafasi ya kwanza, Dilma Rousseff (kulia) na Marina Silva, aliyeshika nafasi ya tatu katika uchaguzi mkuu wa Brazil
Mgombea aliyeshika nafasi ya kwanza, Dilma Rousseff (kulia) na Marina Silva, aliyeshika nafasi ya tatu katika uchaguzi mkuu wa BrazilPicha: DW/AP/Picture-alliance

Mgombea wa Chama cha Mazingira, Marina Silva, anaonekana kuwa ndiye mtu aliyekamata funguo za Ikulu kwa Rais ajaye wa Brazil, baada ya uchaguzi wa marudio mwishoni mwa mwezi huu. Mwanamke huyu aliwashangaza wengi baada ya kuchukua nafasi ya tatu kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika juzi, akijizolea asilimia 19 ya kura badala ya asilimia 14 aliyokuwa amekisiwa na kura za maoni.

Bi Silva aliwahi kuwa waziri wa mazingira katika serikali ya Rais anayemaliza muda wake, Luiz Inacio Lula da Silva kuanzia mwaka 2003, lakini mwaka 2008 alijiuzulu wadhifa huo, alipotafautiana na kile alichokiita "sera za serikali zinazoharibu mazingira katika eneo la Amazon kwa kisingizio cha kuimarisha uchumi." Bi Silva mwenyewe ni mwenyeji wa Amazon.

Rais Luiz Inacio Lula da Silva (kulia) akiwa na Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle
Rais Luiz Inacio Lula da Silva (kulia) akiwa na Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido WesterwellePicha: picture-alliance/dpa

Hata kama yeye mwenyewe hatashiriki kwenye awamu ya pili ya uchaguzi, bado inamaamisha kwamba, ni kura za wafuasi wake, ndizo zitakazoamua nani awe rais, kati ya mgombea aliyeshika nafasi ya kwanza, Dimla Rousseff, au yule aliyeshika nafasi ya pili, Jose Serra. Bi Rousseff anagombea kupitia muungano wa vyama 10 na ni chaguo la Rais Lula, na Serra anatokea chama cha upinzani cha PSDB.

Akizungumza na wafuasi wake mara baada ya matokeo kutangazwa, Bi Silva alisema kwamba ni wao walioibuka washindi, kwani wameweza kulitetea wazo lao na Brazil ikawasikia. Wachambuzi wanamuona mwanamke huyu wa miaka 52 kuwa anafanana zaidi, kihistoria na kimapambano, na Rais Lula kuliko lilivyo chaguo la Rais Lula, yaani Bi Rousseff.

Lula anatokea kwenye familia ya kimasikini kama alivyo Bi Silva, na wote wawili ni wameanzia harakati zao katika makundi yanayotetea haki maalum. Rais Lula anatokea vyama vya wafanyakazi na Bi Silva anatokea chama cha ulinzi wa mazingira. Lakini Bi Rosseff, kwa upande wake, ni mtoto wa familia ya kitajiri, ambaye amekuja kuinuliwa na uteuzi wa Rais Lula, na hajawahi hata mara moja kupigania nafasi yoyote ya kisiasa maishani mwake.

Taarifa zinasema kwamba wengi kati ya wale waliompigia kura Bi Rousseff, walifanya hivyo zaidi kwa lengo la kuonesha utiifu wao kwa Rais Lula, ambaye anamuunga mkono mgombea huyu, na sio kwa Bi Rousseff mwenyewe. Rais Lula anaheshimiwa kutokana na kuiinua nchi yake kiuchumi katika kipindi cha miaka nane ya urais wake.

Lakini shutuma za kashfa ya ufisadi kwenye chama chake, siku moja tu kabla ya uchaguzi, zinatajwa kama sababu ya wapiga kura kuondosha kura nyingi za utiifu kwake na kuzipeleka kwa Bi Silva, mwanamke ambaye ana misimamo ya kimapambano kama yake.

Hadi sasa Bi Silva hajasema wazi ikiwa atamuunga mkono nani kati ya Bi Rousseff na Serra, lakini ni wazi kuwa yeyote atakayeamua kumuunga mkono, lazima kwanza amuhakikishie nafasi ya sera zake za mazingira ndani ya serikali atakayoiunda. Hili linathibitisha kwamba katika mchezo huo wa nipa-nikupe, ni Bi Silva ndiye mwenye karata ya turufu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP

Mpitiaji: Hamidou Oummilkheir