1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Martin Schulz kukutana na Steinmeier

Grace Kabogo
23 Novemba 2017

Kiongozi wa chama cha SPD, Martin Schulz leo anakutana na Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier kujaribu kumshawishi afikirie upya msimamo wake wa kukataa kuingia kwenye serikali mpya ya muungano na Kansela Merkel.

https://p.dw.com/p/2o7DM
Außenminister Steinmeier und Martin Schulz im Gespräch
Picha: picture alliance/dpa/S. Pilick

Steinmeier amekuwa akikutana na viongozi wa vyama vya kisiasa nchini Ujerumani, tangu mazungumzo ya kuunda serikali mpya ya muungano, kati ya muungano wa vyama vya kihafidhina - Christian Democratic, CDU, kinachoongozwa na Kansela Angela Merkel na Christian Social Union, CSU - pamoja na chama kinachowapendelea wafanyabiashara cha Free Democratic, FDP na chama kinacholinda mazingira cha Kijani, yalipovunjika siku ya Jumapili.

Kama kiongozi wa nchi, Steinmeier ana jukumu kubwa na muhimu katika kuhakikisha anatafuta njia ya kupatikana kwa serikali mpya katika taifa hili lenye uchumi mkubwa barani Ulaya.

Kabla ya mazungumzo ya leo, Schulz tayari alishaelezea msimamo wake kwamba hataki kushiriki katika mazungumzo ya kuunda serikali mpya ya muungano. Kiongozi huyo aliliambia shirika la habari la Ujerumani, DPA, kwamba chama chake cha Social Democratic, SPD kinatambua wazi kuhusu majukumu yake katika hali ngumu iliyopo sasa. Schulz amesema watapata suluhisho zuri kwa ajili ya nchi yao katika siku na wiki zijazo.

Deutschland Angela Merkel im Bundestag
Kansela Angela MerkelPicha: Reuters/A. Schmidt

Schulz amekuwa akipata shinikizo kutoka kwa viongozi wa SPD, wakimtaka abadilishe msimamo wake wa kukataa kushiriki katika mazungumzo na Kansela Merkel, kwa lengo la kuzuia uchaguzi mwingine kufanyika.

Hata hivyo, Klaus Larres, Profesa wa masuala ya historia na uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha North Carolina, anasema suala la kufanyika uchaguzi mpya sio rahisi, kwa sababu uchaguzi ulifanyika Septemba na rais wa Ujerumani amesema vyama vya siasa vina jukumu la kuhakikisha maoni ya wananchi waliyoyatoa Septemba yanakuwa ya kweli.

Uchaguzi mpya ni mchakato mrefu

''Kama unataka uchaguzi mpya, unahitaji kulivunja bunge, lakini bunge chini ya mfumo wa Ujerumani haliwezi kuvunjwa. Hivyo pana haja ya kuwa na uchaguzi wa bunge ili kumpigia kura kansela. Na kama kansela atashindwa mara tatu kupata wingi wa kura, basi raisi anaweza kulivunja bunge. Lakini huo ni mchakato mrefu na wa kuchosha ambao naamini unaweza kutupeleka hadi Februari,'' amesema Larres.

Deutschland Jamaika-Koalition Sondierungsgespräche
Wajumbe wa mazungumzo yaliyovunjika JumapiliPicha: Getty Images/AFP/O. Andersen

Viongozi kadhaa wa SPD pia wamependekeza kwamba chama hicho kinapaswa kuivumilia serikali ndogo itakayoongozwa na Merkel kama mkataba wa kuumaliza mzozo huu wa kisiasa nchini Ujerumani.

Baada ya uchaguzi wa Septemba mwaka huu, chama cha SPD kilitangaza nia yake ya kuwa kama kundi kubwa la upinzani katika bunge jipya la Ujerumani. Chama hicho kilisema kinajipanga baada ya kupata matokeo mabaya ya uchaguzi ambayo hayajawahi kuonekana tangu mwaka 1949.

Charlie Lees, mtaalamu wa masuala ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha  Bath, anasema kuna hatari kubwa ya kile kinachotokea. Anasema kwa upande mwingine, iwapo chama cha SPD kitaamua kuachana na msimamo wake na kukubali kufanya mazungumzo na chama cha Merkel, kinaweza kikashutumiwa kwa kutaka maslahi binafsi ya kisiasa na kukosa msingi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, http://bit.ly/2zvIH4A
Mhariri: Mohammed Khelef