1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Mashaka ni makubwa kuliko matumaini"

Maja Dreyer27 Novemba 2007

Kabla ya mkutano wa Annapolis kuanza, washiriki walijitahidi kutoa picha kwamba wana matumaini. Lakini nyuma ya pazia kazi ya wajumbe wa Israel na Wapalestina ya kutafuta msimamo wa pamoja juu ya mazungumzo ni mgumu.

https://p.dw.com/p/CTfC
Vita vitaisha lini Mashariki ya Kati?Picha: AP

Kwa hivyo, wahariri wa magazeti ya humu nchini wana shaka juu ya kuwepo kwa makubaliano. Huu hapa uchambuzi wa gazeti la “Frankfurter Allgemeine”:


“Habari nzuri ni kwamba Marekani imeweza kuzihusisha pande nyingi. Miongoni mwa washiriki 40 hivi kuna nchi nyingi za Kiarabu zinazoongozwa na Saudi Arabia. Hata Syria imo. Mizozo mingi ya eneo hili la Mashariki ya Kati inahusiana kwa hivyo ni hatua barabara kabisa kuzialika nchi za Umoja wa Kiarabu.”


Moja kwa moja tunaendelea na gazeti la “Westfalenpost” la mjini Hagen ambalo limeandika hivi:


“Je, kweli kunafanyika mazungumzo ya amani? Ni kama hujasikia vizuri. Baada ya mkutano huu wa Annapolis, wajumbe wa Israel na Wapalestina wanataka kuanza upya juhudi zao za kusaka amani. Licha ya kwamba mafanikio yangefurahisha sana, bado mashaka ni makubwa kuliko matumaini. Haya ni kutokana na watu wanaoshiriki katika mazungumzo. Kwa upande wa Israel ni waziri mkuu Ehud Olmert ambaye ndani ya Israel anakabiliwa na upinzani mkubwa. Upande wa Wapalestina kuna Rais Mahmoud Abbas ambaye pamoja na kuwakilisha sehemu moja tu ya Wapalestina tena hana nguvu nyingi. Na mwenyeji wa mkutano huu wa leo ni Rais George Bush ambaye hadi sasa amechangia zaidi kuhatarisha usalama Mashariki ya Kati kuliko kuuimarisha.”


Mhariri wa “Landeszeitung” la kutoka Lüneburg anaangalia pia shabaha ya rais Bush kwenye mkutano huu na ameandika:


“Rais Bush wa Marekani anabakia na miezi 14 tu kurekebisha picha juu yake kwenye vitabu vya historia. Baada ya kushindwa katika vita dhidi ya ugaidi na kuharibu usalama Mashariki ya Kati anajaribu sasa kujipatia sifa kwenye jukwaa la kidiplomasia. Lakini mkutano huu wa Annapolis kwa hakika hautatimiza matumaini yaliyopo. Kweli, Syria na Saudi Arabia zinashiriki lakini bado zina wasiwasi juu ya mapendekezo ya Marekani kuhusu kuchora ramani mpya ya Mashariki ya Kati wakati Marekani hasa inajihusisha kama mamlaka ya kulinda Israel badala ya kutetea amani kwa wote.”


Na mwisho tusikie maoni ya mhariri wa “Kieler Nachrichten” ambayo ni wazi kabisa:


“Tayari tunajua nini kitakachotokea huko Annapolis: yaani hakitatokea kitu chochote. Kwa hamu tunasubiri taarifa itakayotolewa, lakini taarifa hiyo itatumia maneno yasiyo ya maana kwa sababu bado kuna masuala mengi mno ambayo hayajatatuliwa. Kwenye mkutano huu wa Annapolis washiriki hawawezi kuharibu heshima kwa sababu maamuzi hayatachukuliwa. Lengo ni kuweka ishara tu ambayo ni kama dawa ya kutuliza.”