1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio ya mabomu yatikisa Baghdad

Omar Babu19 Aprili 2007

Hali ya huzuni ingali imetanda nchini Iraq kutokana na mashambulio ya jana ya mabomu yaliyosababisha kiasi watu mia mbili kuuawa. Mashambulio hayo ya mabomu yaliyotegwa kwenye magari, yamesababisha kutiliwa shaka mkakati wa majeshi ya Marekani wa kudhibiti usalama mjini Baghdad.

https://p.dw.com/p/CB4c
Wakazi wazingira eneo lililokumbwa na mripuko wa bomu, Baghdad.
Wakazi wazingira eneo lililokumbwa na mripuko wa bomu, Baghdad.Picha: AP

Mashambulio ya jana katika maeneo yanayokaliwa na wafuasi wa madhehebu ya Shia mjini Baghdad, yalisababisha maafa makubwa zaidi tangu mashambulio ya tarehe 23 Novemba mwaka jana ambapo kiasi watu 202 waliuawa katika mtaa wa madongoporomoka wa Sadr.

Watu kama 140 waliuawa jana wakati bomu lililotegwa kwenye magari liliporipuka kwenye soko.

Tukio hilo ndilo baya zaidi kuwahi kutokea mjini Baghdad tangu miaka minne iliyopita wakati majeshi ya Marekani yalipoivamia Iraq.

Mkesha wa kuamkia leo, serikali ilitangaza hali ya kutotoka nje na kulipokucha na hali kuwa shwari, watu wakafurika katika Hospitali ya Imam Ali kwenye Mtaa wa Sadr kutafuta maiti za jamaa zao.

Maiti zilizoteketea kiasi cha kutotambulikana zlikuwa zimerundikana, hadi ya hali kuwa ngumu kwa watu kutambua jamaa.

Baadhi ya wakazi hawakubahatika kupata maiti kamili bali waliambulia viungo au hata nguo zilizochanikachanika.

Kwa jinsi hali ilivyokuwa, wakazi wengine hawakuwa na hakika iwapo maiti walizopata ni za jamaa zao.

Mashambulio ya jana yameutia walakini mkakati wa miezi miwili wa majeshi ya Marekani wa kuhakikisha kurejeshwa usalama nchini Iraq.

Waziri Mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki, aliwashutumu waliohusika na akawataka wanasiasa wa madhehebu yote kuwalaani wahusika wa mashambulio hayo.

Waziri Mkuu huyo aliagiza msimamizi wa majeshi wa eneo hilo atiwe nguvuni na achunguzwe kwa kutochukua hatua mwafaka kuwalinda raia.

Tarehe tatu mwezi Februari, bomu lililokuwa limetegwa kwenye lori liliripuka na kuwaua watu kiasi 130.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates, aliahidi kwamba Marekani ingeendelea na mkakati wake wa usalama hata baada ya shambulio hilo la Februari.

Wanasiasa wa Iraq waliyashutumu majeshi ya Iraq yanayoungwa mkono na Marekani wakisema majeshi hayo hayakuwa na uwezo wa kukabiliana na ghasia.

Mbunge mmoja wa Kisunni, Naseer al-Ani wa chama cha kiislamu cha Iraq ameukosoa mkakati huo wa Marekani akisema usalama ulihitajika kudhibitiwa tangu hapo visa vya mabomu vilipoongezeka.

Wafuasi wa kiongozi wa Kishia, Moqtada Sadri, wanayalaumu majeshi ya Iraq yanayoungwa mkono na Marekani.

Tangu hapo kiongozi huyo pamoja na wafuasi wake wamekuwa wakiipiga vita Marekani wakitaka iondoke nchini mwao.

Wamarekani nao wanachukulia kundi hilo kuwa hatari kwa usalama wa Iraq.