1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio yaendelea kugharimu roho za wasio na hatia nchini Iraq

Saumu Mwasimba9 Julai 2007

Watu 250 wameuwawa na wengine kiasi cha 270 wamejeruhiwa kote nchini Iraq kwenye wimbi la mashambulio mwishoni mwa wiki.

https://p.dw.com/p/CB2z
Mashambulio ya mabomu Iraq
Mashambulio ya mabomu IraqPicha: AP

Mshambuliaji wa kujitoa muhanga amewauwa watu 23 waliokuwa wamejiandikisha jeshini nchini Iraq. Mshambuliaji huyo aligongesha lori lake dhidi ya gari walimokuwa wanajeshi hao wapya karibu na mji wa Baghdad.

Waziri mkuu wa Iraq Nouri al Maliki ameyataja mashambulio ya mabomu yaliyotokea jumamosi kaskazini mwa nchi katika kijiji cha Amirl kuwa kitendo kibaya cha uhalifu.

Shambulio hilo lililotokea kwenye mji wa Amirli lilisababisha kuuwawa kwa zaidi ya watu 130 na wengine 240 kujeruhiwa vibaya kabisa.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa bwana Ban Ki Moon pia amelaani mashambulio hayo akisema ni uhalifu dhidi ya raia wasio na hatia.Katibu mkuu amewatolea mwito viongozi wote nchini Iraqi kushirikiana kumaliza ghasia na kuingia kwenye mazungumzo kamili ya kisiasa yatakayoleta amani nchini humo.

Waziri mkuu al Maliki amewalaumu wapiganaji juu ya mashambulio hilo la Amirli akisema vitendo vyao vinaonyesha dalili za kukosa matumaini.

Hapo jana kiasi cha wanajeshi wapya 23 waliuwawa na wengine 27 kujeruhiwa kwenye shambulio la kujitoa muhanga lililofanywa kwenye kituo cha kuwandikisha wanajeshi mashariki mwa Fallujah.

Wanajeshi wengine wapya waliuwawa katika shambulio jingine lililofanywa karibu na mji wa Kharma.Mashambulio mengine mawili yalifanyika kwenye mji wa Baghdad ijapokuwa idadi ya waliojeruhiwa haikuthibitishwa.

Maafisa katika mji wa Amirli wanasema shambulio lililotokea kwenye kijiji hicho linaonyesha wazi kuwa waasi wakisuuni wamekimbilia eneo hilo baada ya kuongezeka opresheni za wanajeshi wa Marekani katika mji wa Baquba.

Kiasi cha watu 20 inasemekana bado wametoweka katika kijiji hicho cha Amirli siku moja baada ya shambulio baya kabisa kukumba eneo lenye shughuli nyingi za soko.

Wakati hayo yakiripotiwa kiongozi wa kidini wa madhehebu ya shia Moqtada al Sadr amejiingiza kwenye vita vya maneno na waziri mkuu Nuri al Maliki akimshutumu kwa kuwapigia magoti Marekani na kufuata matakwa yao. Vita hivi vya maneno vimetokea baada ya wanamgambo wa Mehdi kupambana na polisi na wanajeshi wanaongozwa na Marekani. Sadr amemuonya Maliki kwamba huenda asisalie kwa muda mrefu kuwa waziri mkuu huku kukiwa na ripoti kwamba baadhi ya wabunge wa Mahehebu ya Sunnia na shia huenda wakaungana kulazimisha kura ya imani bungeni.

Hata hivyo mbunge katika muungano wa wakurdi Mahmoud Othman anasema mivutano kama hiyo miongoni mwa wanasiasa na viongozi wa kidini ndio chanzo cha kuongezeka kwa mashambulio nchini Iraq na endapo hali hiyo haitokoma na viongozi kutafuta suluhu basi hata kuongezwa kwa vikosi vya wanajeshi wa Marekani hakutasaidia Kitu.Hapo jumamosi waziri mkuu Nuri al Maliki alisema jeshi la Mehdi la Moqtada al Sadr limejaa wahalifu na wanachama wa chama cha Baath cha aliyekuwa kiongozi wa Iraq Sadam Hussein.

Wafuasi wa Sadr wanasema matamshi hayo ya waziri mkuu yanatoa ruhsa kwa vikosi vya wanajeshi wa Marekani kulishambulia jeshi la Mehdi.

Wakati huo huo kiongozi wa kundi linalodaiwa kuwa na mafungamano na al Qaeda nchini Iraq,Abu Omar al Baghdadi ameapa kwenye ukanda wa video uliotolewa jana kwamba atawashambulia wairan hadi pale Iran itakapokomesha uungaji mkono kwa serikali ya Iraqi katika muda wa miezi miwili.

Abu Omar amesema uamuzi wa kundi lake umetokana na wairan kuunga mkono washia wenzap nchini Iraq na kuishutumu serikali hiyo ya mjini Tehran kwa kuwa nyuma ya mauaji ya viongozi wa kisunni,kuchoma shule za wasunni pamoja na misikiti.