1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio yaendelea nchini Afghanistan

Kabogo Grace Patricia12 Agosti 2009

Mashambulio hayo mapya yamesababisha vifo vya mkuu wa polisi wa wilaya ya Dasht Archi, mlinzi wake pamoja na polisi watano.

https://p.dw.com/p/J8Kq
Rais wa Afghanistan, Hamid KarzaiPicha: AP

Mkuu wa polisi wa wilaya ya Dasht Archi na mlinzi wake wameuawa baada ya wapiganaji wa Taliban nchini Afghanistan kuvamia katikati ya wilaya hiyo iliyopo katika jimbo la Kunduz kaskazini mwa nchi hiyo, huku kwenye eneo la karibu na mji wa Kabul, polisi wengine watano wameuawa katika shambulio la bomu la pembezoni mwa barabara.

Shaikh Sahdi, mkuu wa wilaya ya Dasht Archi, amesema kuwa mkuu huyo wa polisi, Noor Khan na kaka wa Mohammad Omar, gavana wa jimbo la Kunduz, aliuawa katika shambulio lililofanywa jana usiku na kundi la Taliban. Awali, Sahdi alisema walinzi watatu waliuawa katika shambulio hilo, lakini taarifa ya Ikulu imeeleza kuwa ni mlinzi mmoja tu ndiye ameuawa.

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan amesema Khan amepoteza uhai wake wakati akiwalinda watu wake pamoja na mali zao.

Aidha, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeeleza kuwa gari la polisi liliripuliwa jana Jumanne usiku katika shambulio la bomu la kutegwa pembeni mwa barabara kwenye wilaya ya Paghman iliyopo Kabul na kusababisha mauaji ya polisi watano na wengine wanne kujeruhiwa. Haji Qader, Gavana wa wilaya hiyo, amethibitisha kutokea kwa mashambulio hayo.

Msemaji wa Taliban, Zabiullah Mujahid, amedai kuwa wapiganaji wa kundi hilo walizingira wilaya nzima kwa saa chache kabla ya kuondoka kwenda kwenye ngome zao katika jimbo la Kunduz. Msemaji huyo wa Taliban ameongeza kuwa polisi 10 akiwemo Khan, waliuawa katika shambulio hilo.

Mamia ya wapiganaji wa Taliban walirejea kwenye ngome zao za awali baada ya kuondolewa na majeshi ya Afghanistan na Ujerumani kutoka kwenye wilaya mbili za jimbo hilo. Operesheni hiyo ya siku 10 iliwahusisha wanajeshi 300 wa Ujerumani na karibu wanajeshi 1,000 wa Afghanistan na kuisafisha wilaya ya Chardarah na kuwaua wapiganaji 17 wa kundi hilo. Lakini wapiganaji hao walirejea kwenye wilaya hiyo baada ya jeshi la muungano kumaliza operesheni zake mwezi uliopita, hivyo kusababisha hali ya hatari kuelekea kwenye uchaguzi wa urais wa Agosti 20, mwaka huu.

Wakati hayo yakijiri, watu wenye silaha wamewateka watu watatu waliokuwa wakifanya kampeni kwa ajili ya mgombea mmoja wa uchaguzi wa urais, siku nane kabla ya uchaguzi huo. Watu hao walikuwa wakifanya kampeni kaskazini-magharibi mwa jimbo la Badghis kwa ajili ya waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje, Dokta Abdullah Abdullah, anayeshika nafasi ya pili baada ya mpinzani wake Rais Karzai.

Abdul Ghafar, afisa habari wa ofisi ya kampeni ya Dokta Abdullah, ameilaumu serikali kwa kutowapa ulinzi wafanya kampeni wa mgombea huyo. Mwezi uliopita serikali ya Afghanistan ilisema imeacha mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa Taliban katika baadhi ya wilaya za Badghis ili kuruhusu wananchi kupiga kura.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/RTRE)

Mhariri: M. Abdul-Rahman