1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi mapya kwa IS yafanyika Kobane

Mjahida 8 Oktoba 2014

Ndege moja ya muungano wa Kimataifa unaoongozwa na Marekani unaopambana na wanamgambo wa dola la kiislamu IS, imefanya mashambulizi mapya ya angani ikiyalenga maeneo ya mji wa Syria unaopakana na Uturuki wa Kobane.

https://p.dw.com/p/1DS0O
Moshi uliotokana na Mashambulizi ya angani mjini Kobane
Moshi uliotokana na Mashambulizi ya angani mjini KobanePicha: Aris Messinis /AFP/Getty Images

Kulingana na muandishi wa shirika la habari la AFP, mashambulizi hayo yamesababisha moshi mkubwa kuonekana Mashariki mwa Kobane. Hili ni shambulizi la kwanza kuripotiwa hii leo baada ya mashambulizi kadhaa yaliofanywa hapo jana.

Aidha Shirika la uangalizi wa hakli za binaadamu nchini Syria limesema, wapiganaji hao wa jihadi wameanza kuondoka katika baadhi ya maeneo mjini Kobane usiku wa kuamkia leo baada ya mashambulizi makali kutoka kwa muungano huo unaoongozwa na Marekani dhidi ya kundi hilo.

Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Rami Abdel Rahman, amesema wapiganaji hao waliondoka eneo la mashariki la Ain al-Arab na katika maeneo ya kusini magharibi mwa mji huo. Siku ya Jumanne mapigano yalipamba moto Mashariki, Magharibi na kusini mwa mji wa Kobane ambao ni mji wa tatu kwa ukubwa nchini Syria unaokaliwa na wakurdi.

Eneo la Kobane
Eneo la KobanePicha: Aris Messinis /AFP/Getty Images

Mustafa Ebdi, mwandishi habari wa kikurdi na mwanaharakati anayeishi mjini humo amesema hali ni mbaya na watu katika eneo hilo wanahitaji kwa wingi msaada wa maji na chakula. Tangu wapiganaji wa IS walipoanza kuusogelea mji huo tarehe 16 mwezi wa Septemba, takriban watu 186,000 wameyakimbia makaazi yao na kuingia nchini Uturuki.

Nguvu za ziada zahitajika kuulinda mji wa Kobane

Kwa upande mwengine mjumbe wa Syria katika Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura amesema kunahitajika nguvu za ziada kuulinda mji wa Kikurdi wa Kobane. Mistura amesema jamii ya Kimataifa haiwezi kushuhudia wanamgambo wa dola la kiislamu wakiudhibiti mji mwengine, Akigusia umuhimu wa usaidizi wa haraka huku akisema kwamba wanamgambo hao wanaonekana kuwa na silaha kali.

Marekani na washirika wake wamezidisha mashambulizi yao karibu na maeneo ya Kobane katika siku za hivi karibuni wakati mji huo ukionekana kuwa muhimu kwa wanamgambo wa IS wanaoyadhibiti maeneo makubwa nchini Syria na Iraq na kutangaza utawala wa sheria za kiislamu huku wakiripotiwa kufanya ukatili mkubwa katika maeneo hayo.

Wakati hayo yakijiri watu 14 wameuwawa katika maandamano ya wafuasi wa kikurdi nchini Uturuki kufuatia serikali ya nchi hiyo kutochukua hatua yoyote kuulinda mji wa Syria wa Kobane.

Mjumbe wa Syria katika Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura
Mjumbe wa Syria katika Umoja wa Mataifa Staffan de MisturaPicha: Reuters

Ghasia hizo zimetokea mjini Istanbul na Ankara pamoja na miji mengine wakati polisi wakijaridhu kuwatawanya waandamanaji.Wanajeshi wa Uturuki wamepelekwa katika miji tofauti nchini humo ya Diyarbakir, Mardin na Van – ilio na idadi kubwa ya wakurdi.

Serikali ya Chama tawala cha haki na maendeleo nchini Uturuki AKP hakijaingilia kijeshi vita dhidi ya kundi la wanamgambo wa IS wanaopigana katika mji wa Kikurdi wa Kobane.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman