1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi mapya yaripotiwa Syria

8 Februari 2012

Vikosi vya Syria hii leo (08.02.2012) vimeyashambulia maeneo ya mkoa wa Homs kwa siku ya tano mfululizo, na kuwauwa karibu watu 47. Eneo hilo ni kitovu cha maandamano ya kuupinga utawala wa Assad.

https://p.dw.com/p/13z3V
Mazishi ya mmoja wa waliouwawa katika mji wa Homs
Mazishi ya mmoja wa waliouwawa katika mji wa HomsPicha: dapd

Vifaru viliingia katika maeneo jirani ya Inshaat na kusogea karibu na wilaya ya Bab Amro ambayo imehujumiwa kwa makombora makali ya wanajeshi walio watiifu kwa Assad. Mashambulizi hiyo yamewauwa takriban raia 100 katika siku mbili zilizopita. Walioshuhudia wamesema vifaru hivyo vilikuwa nje ya msikiti wa Qubab, na wanajeshi wakaingia katika hospitali ya Hikmeh mjini Inshaat.

Mwanaharakati Mohammad al-Hassan amesema kupitia simu ya Satellite kutoka mjini Homs kuwa vikosi hivyo vilisogea karibu na Bab Amro na milio ya risasi na makombora ilisikika katika maeneo ya Karm al-Zeitoun na al-Bayada. Ameongeza kuwa mawasiliano yamekatizwa katika sehemu nyingi za mji wa Homs, na ni vigumu kutathmini taswira ya jumla ya mambo.

Assad akubali kusitisha umwagikaji wa damu

Mashambulizi hayo katika mji wa Homs yanaendelea, licha ya Urusi kupata ahadi kutoka kwa Assad ya kukomesha umwagikaji wa damu, huku mataifa ya Magharibi na Kiarabu yakiendelea kujitenga na Assad kufuatia ukandamizaji huo ambao ni mojawapo ya mauaji mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika mapinduzi hayo yaliyodumu miezi 11.

Rais wa Syria Bashar al-Assad amkaribisha Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov
Rais wa Syria Bashar al-Assad amkaribisha Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei LavrovPicha: AP

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov, akiiwakilisha Urusi ambayo ni mshirika wa Syria, alisema jana mjini Damascus kuwa nchi zote mbili zinatathmini juhudi za Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ambazo mpango wake wa kutatua mgogoro wa Syria ulipingwa na Urusi na China kupitia kura za turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Lavrov alimwambia Assad kuwa amani ni jambo ambalo liko katika maslahi ya Urusi. Lakini hakukuwa na dalili kutokana na matamshi hayo ya Lavrov kuwa suala la Assad kuwachia madaraka, ambalo ndilo pendekezo kuu la Umoja wa Nchi za Kiarabu, lilizungumzwa katika kikao hicho.

Assad alisema atashirikiana na mpango wowote ambao utarejesha utulivu nchini Syria, lakini akaeleza bayana kuwa hilo lilijumuisha pendekezo la awali la Jumuiya ya Kiarabu ambalo lilitaka pawepo mashauriano, kuwaachilia huru wafungwa na kuwaondoa wanajeshi katika vituo vya maandamano.

Upinzani wasema Assad hafai kuendelea kuongoza

Walid al-Bunni, mwanachama mkuu wa Baraza la Kitaifa la Syria ambalo ni kundi la upinzani, amesema Lavrov hakupeleka mipango mipya, na kile kilichoitwa mageuzi ambayo Assad aliahidi hayatoshi. Alisema maovu yaliyofanywa na Assad hayampi haki yoyote kiongozi huyo kuendelea kuwa madarakani.

Maandamano dhidi ya utawala wa Bashar al-Assad
Maandamano dhidi ya utawala wa Bashar al-AssadPicha: picture-alliance/dpa

Licha ya ukandamizaji unaofanywa, wanaharakati waliripoti kuwepo maandamano dhidi ya utawala wa Assad kote nchini humo, ukiwemo mkoa wa kusini Sweida.

Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba lilisema wanachama wake wanawaita nyumbani mabalozi wake kutoka Damascus na kuwatimua mabalozi wa Syria kutoka nchini mwao kutokana na ghasia zinazoendelea kushuhudiwa.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Oummilkheir Hamidou