1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

''Jihadi John'' alengwa kwenye mashambulizi ya Marekani

13 Novemba 2015

Marekani imefanya mashambulizi ya anga nchini Syria yanayomlenga ''Jihadi John'', raia wa Uingereza anayetuhumiwa kuonekana kwenye video kadhaa za kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu-IS, zinazoonyesha watu wakichinjwa.

https://p.dw.com/p/1H53I
Picha ya ''Jihadi John''
Picha ya ''Jihadi John''Picha: SITE Intel Group/Handout via Reuters

Mkurugenzi wa habari wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Peter Cook amesema mashambulizi hayo ya vikosi vya Marekani, yamefanyika usiku wa jana kwenye ngome muhimu ya IS ya Raqqa, kaskazini mwa Syria.

Amesema mashambulizi hayo yalikuwa yakimlenga Mohammed Emwazi, anayejulikana pia kama ''Jihadi John'', ambaye amekuwa akionekana kwenye mikanda ya video inayomuonyesha akiwachinja waandishi wa habari wa Marekani, Steven Sotloff na James Foley, akiwa kajifunika uso wake.

Raia huyo wa Uingereza pia ameonekana kwenye video za mauaji ya mfanyakazi wa shirika la misaada la Marekani, Abdul-Rahman Kassig, wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya Uingereza, David Haines na Alan Henning, mwandishi wa habari wa Japan, Kenji Goto pamoja na watu wengine kadhaa waliokuwa wakishikiliwa mateka.

Nalo shirika la kufuatilia haki za binaadamu nchini Syria, lenye makao yake Uingereza, limesema leo kuwa kiongozi wa IS ambaye ni raia wa Uingereza na wanamgambo watatu wa kigeni, wameuawa katika mashambulizi hayo ya Marekani. Hata hivyo shirika hilo, halijaeleza iwapo raia huyo wa Uingereza ni ''Jihadi John'' au la. Mapema leo Marekani ilisema huenda Emwazi ameuawa katika mashambulizi hayo.

Picha ikionyesha ndege za Marekani zinazoishambulia IS
Picha ikionyesha ndege za Marekani zinazoishambulia ISPicha: picture-alliance/Us Air Force/M. Bruch

Cook amesema wanaitathmini operesheni hiyo na watatoa taarifa zaidi kwa wakati utakaofaa. Vyombo vya habari vya Marekani na Uingereza, vilimpachika Emwazi jina la ''Jihadi John'', baada ya kundi la watu walioshikiliwa mateka kusema kwamba alikuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wanaojiita ''The Beatles.''

Mzaliwa wa Kuwait

Emwazi, alizaliwa Kuwait katika familia isiyo na uraia ambayo ina asili ya Iraq. Wazazi wake walihamia Uingereza mwaka 1993, baada ya juhudi zao za kupata uraia wa Kuwait, kushindikana.

Mashambulizi hayo ya anga ya Marekani dhidi ya ''Jihadi John'' yamefanyika wakati ambapo vikosi vya Kikurdi vya Peshmerga leo vimeingia katika mji wa Sinjar, ili kuendesha operesheni ya kuusafisha mji huo wa kaskazini mwa Iraq, uliokuwa unadhibitiwa na IS.

Vikosi vya Peshmerga vinavyoungwa mkono na mashambulizi ya anga ya Marekani, jana vilianzisha operesheni waliyoipa jina ''Operesheni ya kuisafisha Sinjar,'' vilifanikiwa kuifunga barabara kati ya mashariki na magharibi, wakati vikipambana na wanamgambo wa IS. Kamanda wa Peshmerga Dyar Namo, anafafanua zaidi.

Wapiganaji wa Peshmerga wakipambana na IS Sinjar
Wapiganaji wa Peshmerga wakipambana na IS SinjarPicha: Reuters/A. Jalal

''Jana baada ya mashambulizi ya anga tukisaidiwa na vikosi vya muungano, hapakuwa tena na operesheni zao wala mizunguko miongoni mwao. Mji ulikuwa umetulia,'' alisema Namo.

Taarifa iliyotolewa na baraza la usalama la eneo la Kurdistan katika mtandao wa mawasiliano ya kijamii wa Twitter, imeeleza kuwa milio mikubwa ya risasi imesikika ndani ya mji huo, wakati ambapo wapiganaji hao walijikusanya chini ya mlima wakiuangalia mji huo kutoka upande wa kaskazini. Watu walioshuhudia wamesema baadhi yao walikuwa wamebeba mabegani mikanda yenye mabomu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,DPAE,APE
Mhariri: Gakuba Daniel