1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yazidi Somalia

20 Aprili 2007

Mshambuliaji mmoja wa kujitoa mhanga alivamia na kulipua kituo cha wanajeshi wa Ethiopia na mizinga kulipuliwa katika soko moja ambapo watu 21 waliuwawa. Zaidi ya raia mia moja walijeruhiwa vibaya katika matukio hayo lililofanyika Mogadishu.

https://p.dw.com/p/CB4Z
Majeruhi wafikishwa katika hospitali ya Medina,Mogadishu.
Majeruhi wafikishwa katika hospitali ya Medina,Mogadishu.Picha: AP

Mlipuaji huyo wa kujitoa mhanga aliendesha gari na kulipitisha katika lango la kituo hicho cha kijeshi cha Ethiopia kabla kujilipua. Japo Naibu waziri wa usalama Salad Ali Jelle alikanusha madai ya wanajeshi kuwawa huku akisema ni wale waliokuwa ndani ya gari waliofariki Walioshuhudia kisa hicho walisema wanajeshi kumi wa Ethiopia waliuwawa au kujeruhiwa wakati walipofaytuliana risasi nwa washambulizi hao.

Katika tukio lengine gari la wanajeshi wa Ethiopia lilipuliwa na bomu la kutega kusini Mogadishu. Milipuko pia ilisikika katika soko moja usiku kucha na watu sabini kupelekewa kwa matibabu katika hospitali ya Medina.

Waasi kutoka kwa jamii ya Hawiye na wanamgambo wa mahakama za kiislamu waliotolewa uongozini mwaka uliopita na wanajeshi wa Ethiopia, ndiyo wanaodaiwa kuipiga vita serikali ya mpito ya Somalia,majeshi ya Ethiopia na yale kutoka umoja wa Africa.

Kisa hiki cha mlipuaji wa kujitoa mhanga kimezuwa wasiwasi kuwa vita hivi Somalia vimechukua mtindo wa ki Al Qaeda na kudhihirisha mahakama za kiislamu wana mahusiano na kundi hilo la kigaidi.

Tayari Kiongozi mkuu wa mahakama za kiislamu Sheik Shariff Sheik Ahmed,Naibu waziri mkuu wa Somalia Hussein Aided na aliyekuwa spika wa bunge Hassan Sheik Aden wamesema ikiwa wanajeshi wa Ethiopia hawataondoka kwa amani,wasomali watawaondoa kwa nguvu. Viongozi hawa walisema haya baada ya kukutana na rais wa Eritrea Isaias Afwerki ambaye ameshtumiwa na Marekani kwa kuunga mkono makundi ya waasi, kwa dhana yake kuwa wasomali wajitatulie shida zao wenyewe bila ya mataifa mengine kujiingiza katika mizozo yao.

Umoja wa mataifa umesema tangu mwezi Machi ambapo watu elfu moja waliuwawa katika mashambulizi ya siku nne,wameshindwa kusafirisha misaada kwa raia. Tayari watu mia nne wamefariki kutokana na kipindupindu, yamkini msimu wa mvua umewadia na huenda hali ikazorota zaidi.

Serikali ya mpito ya Somalia ilishindwa kuanzisha mkutano wa mapatanisho baada ya hali ya usalama kuzorota mjini Mogadishu.

Wakati huohuo raia wa Marekani amekiri mashtaka ya kupewa mafunzo ya kigaidi nchini Somalia. Daniel Jospeh anayejulikana pia kama Daniel Aljughaifi baada ya kuslimu, alikiri kwamba alisafriki kutoka Marekani hadi somalia mwezi desemba ambapo alipewa mafunzo hayo kwa madhumuni ya kusaidia makahama za kiislamu kuipindua serikali ya mpito. Jospeh alikamatwa na maafisa wa polisi nchini Kenya alipokuwa akijaribu kutoroka Somalia. Hatia hii Marekani huandamana na kifungu cha miaka 10 na faini ya Dolla laki mbili unusu. Mahakama kuu ya Marekani imesema hukumu yake itakuwa funzo kwa wamarekani wengine wanaotaka kujiunga na makundi ya kigaidi

Isabella Mwagodi