1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi zaidi yafanywa Libya

Kabogo, Grace Patricia22 Machi 2011

Mashambulizi zaidi yameutikisa mji mkuu wa Libya, Tripoli kwa usiku wa tatu mfululizo tangu kundi la mataifa kumi ya Magharibi, ikiwemo Marekani, Ufaransa na Uingereza yalipoanzisha mashambulizi ya anga.

https://p.dw.com/p/10et3
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: ap

Mashambulizi hayo yameanzishwa katika kutekeleza marufuku ya ndege kuruka kwenye anga dhidi ya utawala wa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi. Mjini New York, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya kikao cha siri.

Wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa wamekaririwa na shirika la habari la Reuters wakisema kuwa baraza hilo limekataa ombi la waziri wa mambo ya nchi za nje wa Gaddafi la kufanyika mjadala wa dharura. Badala yake wamesema baraza hilo linaendelea na mipango yake ya kufanya kikao chake siku ya Alhamisi kutathmini matokeo ya marufuku hiyo.

Explosion Libyen Anti-Gaddafi Rebellen Bengasi
Moto ukisambaa baada ya kutokea mripuko nchini LibyaPicha: dapd

Kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kimetangaza kuwa kambi mbili za jeshi la wanamaji la Libya zilizoko karibu na Tripoli, zinaonekana kushambuliwa katika saa za hivi karibuni. Taarifa za awali kutoka magharibi mwa Libya kwenye mji wa Zintan zilieleza kuwa wanajeshi watiifu kwa Kanali Gaddafi wamefyatua makombora na kuwalazimisha wakaazi wa eneo hilo kukimbia.

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umekubaliana kuhusu vikwazo zaidi vya kiuchumi dhidi ya utawala wa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, vikiwalenga washirika 11 wa kiongozi huyo na mashirika tisa ya kiuchumi. Hiyo ni awamu ya tatu ya vikwazo vya umoja huo kwa Libya tangu serikali ianze kuwakandamiza waandamanaji wanaopigania demokrasia kwa mwezi mmoja sasa.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle ameunga mkono vikwazo kama njia ya kumshinikiza Kanali Gaddafi ajiuzulu, huku akipinga uvamizi wa kijeshi. Pia ametetea uamuzi wa Ujerumani kutopiga kura katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kupiga marufuku ndege kuruka kwenye anga yake.