1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashariki ya Kati-Vita vya Siku Sita

P.Martin4 Juni 2007

Miaka 40 iliyopita Israel ilifanikiwa kunyakua sehemu kubwa ya ardhi katika kipindi cha juma moja.

https://p.dw.com/p/CHDC
Israel yajenga nyumba kwenye Milima ya Golan
Israel yajenga nyumba kwenye Milima ya GolanPicha: DPA

Kwa maoni yake,ilichukuwa hatua ya kujihami; kwa Waarabu hilo lilikuwa shambulizi la vita.

Vita vya tatu vya Mashariki ya Kati vilivyoanza tarehe 5 mwezi Juni mwaka 1967 na kudumu hadi tarehe 10 vimebadili sura ya kisiasa na ya kijeshi katika Mashariki ya Kati.Vita hivyo vya siku sita kimsingi,vimebadili hali ya mambo katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati.Kwani Israel ilitia mikononi mwake milima ya Golan ya Syria:ardhi ya Jordan iliyoanzia Ukingo wa Magharibi hadi Ukanda wa Gaza ambao wakati huo ulidhibitiwa na Misri.Kwa hivyo,Israel ikadhibiti eneo zima lililokuwa Palestina ya kale. Kuambatana na uamuzi ulioptishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1947,taifa moja la Kiyahudi na moja la Kiarabu yangeundwa katika eneo hilo.Ulimwengu wa Kiarabu lakini haujakubali uamuzi wa kulitenga eneo hilo.Kwa Waisraeli wengi,vita vya mwaka 1967 vile vile vilimaanisha kupigania uhai wao kwa sababu ya vitisho vilivyotokea Cairo na Damascus.

Ahmed Shukeiry aliekuwa mwenyekiti wa kwanza wa chama cha Ukombozi wa Palestina PLO,alionya kuwa chama chake kinangojea tu ”kuwatumbukiza Wayahudi baharini”.Lakini ukweli wa mambo na jinsi vita vilivyokuwa vikiendelea,ulikuwa tofauti kabisa na vitisho hivyo.Kwani vikosi vya anga vya Israel katika muda wa saa moja,viliweza kuteketeza jeshi la anga la Misri. Vikosi vya jeshi la ardhini la Misri vilitimuka. Israel haikupata shida yo yote upande huo.Hata vita dhidi ya Syria na Jordan vilikwenda hivyo hivyo katika siku zilizofuatia.

Vita hivyo vya siku sita viliondoa matumaini ya aliekuwa rais wa Misri,Gamal Abdel Nasser ya kuwa na muungano wa nchi za Kiarabu.Vita hivyo vilianzisha mtazamo mwengine kuelekea dini.Baadhi ya watu walitumaini kujipatia nguvu kwa njia hiyo kwani uzalendo wala ukomunisti haukuweza kuwasaidia na hasa si nchi za magharibi.

Mwanzoni,baadhi ya Waisraeli walitumaini kupata amani kwa kubadilishana maeneo yaliyokaliwa.Hata Syria imejadiliana na Israel suala la kuondoka Milima ya Golan lakini hadi hivi leo hakuna ishara za kupatikana amani.Hatimae matokeo ya Intifada na mapigano makali kati ya Wapalestina wenyewe na hatua kali zinazochukuliwa na Israel dhidi ya Wapalestina ni mambo ambayo kwa hivi sasa yameondosha matumaini hata kwenye Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi,kuwa uvamizi wa miaka 40 unakaribia kumalizika.