1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashariki ya Kati

20 Juni 2007

Israel imeanzisha leo mazungumzo tena na serikali ya dharura ya palestina na imechukua hatua ya kukitenga zaidi chama cha Hamas huko Gaza.

https://p.dw.com/p/CHCR

Israel leo iliwahujumu wapiganaji wa Hamas katika mwambao wa Gaza ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo tangu Hamas kuudhibiti mwambao huo.Pia Israel imeacha kuususia utawala wa Palestina kwa kuanzisha leo mazungumzo na serikali mpya huko Ukingo wa magharibi isioingiza Hamas.

Hapo kabla wanajeshi wa Israel leo waliwaua wapiganaji 4 wa kipalestina walipovuka mpaka na kuingia Gaza kuwasaka wale wanaowaita magaidi.Israel pia ilihujumu vituo vinavyofyatua makombora baada ya kombora moja leo lililofyatuliwa kutoka gaza kuangukia Israel.

Wanamgambo wengine 2 wa kipalestina-mmoja kutoka chama cha Islamic Jihad na mwengine wa chama cha Fatah waliuliwa wakati wa mapigano ya bunduki huko ukingo wa magharibi.

Waziri wa nje wa Israel Tzipi Livni alifanya leo mawasiliano ya kwanza kabisa ya hadhi ya juu na serikali ya dharura ilioundwa na rais Mahmud Abbas katika ukingo wa magharibi-moja kati ya maeneo 2 yanayodhibitiwa na wapalestina.

Livni alumuarifu waziri mkuu wa Palestina Salam Fayyad kwa njia ya simu kuwa kuanzishwa kwa serikali ya dharura iliochukua mahala pa ile iliongozwa na Hamas,kutafungua mlango wa maendeleo katika sekta mbali mbali.

Israel haikuwa na mawasiliano na serikali iliopita ya palestina kwa muda wa miezi 15 wakati chama cha Hamas kikiwa pia madarakani kufuatia uchaguzi uliopita mwaka mmoja na nusu.

Hivi majuzi katika changamoto kati ya Hamas na Fatah, rais Mahmud Abbas aliivunja serikali iliongozwa na waziri mkuu Ismail Haniyeh wa chama cha Hamas.Hamas imekataa kuitambua serikali mpya ya Palestina na kingali kikijitambua kuwa ndio kiongozi wa ile serikali ya Umoja wa Taifa ya Palestina.

Matokeo ya vuta nikuvute hii ni kuwa Hamas inatawala Gaza wakati Fatah imetamba Ukingo wa magharibi.Mwambao wa gaza umewekewa sasa vikwazo vya kiuchumi na kijeshi vya Israel na rais Bush pamoja na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert,waliahidi jana huko Washington kumuimarisha rais Abbas na kukaza vikwazo dhidi ya hamas.Ikiwa hatua ya kwanza, waziri mkuu Olmert ameahidi kuziachia kodi za wapalestina ilizozizuwia tangu pale chama cha Hamas kilipochaguliwa madarakani.

Maafisa wa hadhi ya juu wa Palestina wamearifu mapema leo kwamba, rais Mahmud Abbas na waziri mkuu Olmert huenda wakakutana wiki ijayo huko Misri,lakini msaidizi wa waziri mkuu Olmert amesema hakuna tarehe ya kikao chochote iliowekwa.