1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashauriano baina ya Moroko na Chama cha Polisario cha Sahara ya Magharibi

18 Juni 2007

Chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa wiki hii yameanza karibu na mji wa New York mashauriano baina ya Moroko na Chama cha Ukombozi cha Polisario kuhusu hali ya baadae ya Sahara ya Magharibi.

https://p.dw.com/p/CHCX
Wapiganaji wa Polisario karibu na mpaka na Moroko
Wapiganaji wa Polisario karibu na mpaka na MorokoPicha: AP

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika azimio lake nambari 1754, limezitaka pande hizo mbili zianze kufanya mazungumzo baina yao bila ya masharti ili kupata suluhisho la kisiasa litalokubalika na pande zote mbili za mzozo huo ambao umedumu zaidi ya miaka 30 sasa. Sahara ya Magharibi ambayo ni ardhi yenye utajiri wa mali asili na yenye ukubwa wa eneo sawa na Ujerumani ilitwaaliwa na Moroko mwaka 1975. Chama cha Polisario kiliikataa hatua ya Moroko ya kulitwaa eneo hilo, na, ikisaidiwa na Algeria, ikataka uhuru wa Sahara Magharibi.

Mzozo huu wa Sahara Magharibi ni moja kati ya mizozo iliosahauliwa hapa duniani, kwani sio wenye utumiaji nguvu, na mtu huhisi kwamba mzozo huo unaweza ukaendelea maisha bila ya kupatiwa ufumbuzi. Hajo Lanz bingwa wa Wakfu wa Kijerumani wa Friedrich-Ebert mjini Rabat, ana haya ya kusema juu ya mzozo huu:

+Jamii ya kimataifa inaishi na hali hiyo hivi sasa na hakuna tena vita. Kuna amri ya kusitisha mapigano na watu wote wanaweza kuishi na hali kama ilivyo sasa.+

Hata hivyo, mzozo huu, ambao ni matokeo ya mabaki ya ukoloni, shinikizo la watu wa Sahara Magharibi kutaka kuwa na haki yao ya kujiamulia wenyewe mustakbali wao na ushindani wa kimkoa baina ya Moroko na Algeria, haujawa maisha usiomwaga damu. Tangu ilipopata uhuru mwaka 1956, Moroko imekuwa ikiidai Sahara Magharibi, wakati huo bado koloni ya Mhispania, kuwa ni milki yake. Mwaka 1973, vijana wachache wa kizalendo wa Ki-Saharawi waliunda Chama cha Ukombozi cha Polisario kwa lengo la kuunda dola huru. Mwaka mmoja baadae, Moroko ilikwenda katika Mahakama ya Kimataifa mjini The Hague, Uholanzi, ambayo katika hukumu yake ilitaka makabila fulani ya Saharawi yaingizwe katika ufalme wa Moroko, lakini sio kwamba Moroko iwe na mamlaka ya Sahara Magharibi.

Oktoba mwaka 1975 ulikuwa wakati wa mabadiliko katika historia ya mzozo huo. Wakati mtawala wa kidikteta wa Spain, Jenerali Franco, akiwa mahututi kitandani. Mfalme Hassan wa Moroko alitayarisha maandamano ya amani yaliopewa jina la Maandamano ya Kijani. Raia laki tatu na nusu walishiriki kwenda kutwaa kile kilichoitwa rasmi katika Msamaiti wa Moroko mikoa ya Kusini. Spain iliondoka Sahara Magharibi bila ya kupigana. Hapo tena kukaanza vita juuya Sahara Magharibi. Chama cha Polisario kiliwahamisha maelfu ya Wa-Saharawi na kuwapeleka Tindouf, nchini Algeria, na kuanzisha vita vya chini kwa chini dhidi ya Moroko, vita vilivosababisha maelefu ya watu kufa katika pande zote mbili.

Juhudi zote za kimataifa kuupatia mzozo huu suluhisho la mwisho zimeshindikana. Mafanikio pekee ambayo jamii ya kimataifa yameyapata ni ile amri ya kusitisha mapigano baina ya pande mbili amapo ilitokana na upatanishi wa Umoja wa Mataifa hapo mwaka 1991 na ambapo pia ilikubaliwa kwamba kufanywe kura ya maoni katika Sahara Magharibi kuwauliza watu wa eneo hilo wanataka mustakbali wao uwe vipi. Kura hiyo ya maoni haijawahi kufanyika Pande hizo mbili hazijaweza kuafikiana kama angalau uchaguzi huo ufanyike, kama vile Bachir Eddalchil, mwanachama muasi wa Chama cha Polisario alivosema. Yeye amesharudi Moroko:

+Umoja wa Mataifa haujaweza kutafsiri ni nani watakuwa wapigaji kura. Wameanza, lakini hawajaweza Wa-Saharawi gani watakaokuwa na haki ya kushiriki katika kura hiyo ya maoni.+

Wakati huo huo, Moroko inakataa kuendeshwa kura hiyo ya maoni na imependekeza kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba Sahara Magharibi iwe na utawala mkubwa wa mambo yake ya ndani chini ya mamlaka ya Moroko. Jambo hilo linakataliwa na Polisario, kama vile Ahmed Sidaty, waziri wake wa mambo ya kigeni, alivohakikisha.

+Haiwezekani kabisa kwamba mpango wa utawala wa ndani uliopendekezwa na Moroko uweze kuwa msingi wa mashauriano, ikiwa tunataka kuwa wakweli na moyo wa azimio la baraza la usalama la umoja wa Mataifa. Azimio hilo linataka kuweko mashauriano ya moja kwa moja ili kupata suluhisho la kisiasa litakaloruhusu Wa-saharawi wajiamuliwe wenyewe mustakbali wao.

Nilimuuliza mwandishi wa habari wa Kimoroko anayesihi hapa Ujerumani, Abdul samad Jatiwi, kwanini Wamoroko wamekubali kwenda mara hii katika meza ya mashauriano, na pia Wa-saharawi:

+Hii inaonesha nia safi kwanini Moroko imekwenda katika meza ya mashauriano. Inakwenda na mswaada wa kutaka kuweko serekali ya madaraka ya ndani, kukiweko nia ya kulipatia eneo hilo la Sahara Magharibi mustakbali na kuondosha mivutano kutoka upande wowote, na kuhakikisha amani na neema kwa watu wa Sahara Magharibi.+

+ Kwa uchache, tunaweza kulibadilisha suali na kuuliza vipi Algeria imegeuza msimamo wake. Algeria imeelezea utayarifu wake kushauriana na Moroko kwa vile, kimsingi, inahisi kuna hatari maalum. Tunapozungumza juu ya mashauriano Moroko inashauriana, japokuwa sio moja kwa mnoja, na Algeria, haishauriani na Polisario, kwani inayoihifadhi Polisario ni Algeria ambayo inaipa Polisario silaha na misaada, na mwishowe msimamo wa kisiasa utakaochukuliwa na Polisario utakuwa unaelemea kwa Algeria, na jambo hili ni wazi kabisa.+

Raia, hasa wale walio wakimbizi wa Kisaharawi huko Tindouf, Algeria, wanalipia bei ilio ghali kutokana na mzozo huu usiokwisha. Zaidi ya watu 160,000 wanaishi katika hali ngumu kwenye makambi ya wakimbizi yalioko katika jangwa la huko Algeria. Wote wakitegemea kabisa misaada ya kiutu ya kimataifa. Lakini jamii ya kimataifa inapendelea kuupuuza mzozo huu, lakini pia umezigawa nchi, kati ya zile zinazouunga mkono msimamo wa Polisario, nyuma yake ikiweko Algeria, na wale wanaoiunga mkono Moroko. Hata Umoja wa Ulaya hauna msimamo mmoja kuhusu suala hili:

+Naamini hakuna hasa lengo maalum la Umoja wa Ulaya, licha ya tu kuunga mkono, bila ya shaka, harakati za Umoja wa Mataifa zitakazopelekea suluhisho la kisiasa litakalokubalika.+

Mataifa makuu, yakitilia maanani kuweka wizani katika maslahi yao ya kijeshi, yanaurefusha muda wa kuweko mzozo huu. Hali hiyo inazidi kuendelea kama ilivyo na inazuwia maendeleo katika eneo la Maghreb, yaani Afrika Kaskazini.

Kama mashauriano ya sasa ya New York yatafua dafu, mweandishi wa habari wa Kimoroko, Abdul samad jatiwi aliniambia hivi:

+Naamini kwamba mashauriano haya yatapelekea huenda mambo mengi mazuri sana kwa Wamoroko wote, kwa vile Saharawi ni ya Moroko, kihistoria, na mashauriano juu ya kupata suluhisho la kweli ndio njia ilio bora, na ni njia iliokubaliwa na pande mbili. Kunabaki tu masuala ya kiufundi ambayo yanaweza kutanzuliwa kwa urahisi, huenda yasihitaji kuweko ugumu wowote ila tu ikiwa pande nyingine zitajiingiza kuyafanya mambo yawe magumu.+

Vyovyote itakavyokuwa, huenda mashauriano haya yakafungua mwangaza mpya, licha ya kwamba misimamo ya pande mbili hizo inaonekana kuwa haikaribiani.