1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashindano ya Jumuiya ya Madola

12 Oktoba 2010

Leo ndio siku ya mwisho ya mashindano ya riadha katika michezo ya Jumuiya ya Madola inayoendelea mjini New Delhi, nchini India.

https://p.dw.com/p/PcE7
Mganda Moses Kipsiro, anyakua dhahabu katika mbio za mita 5,000 kwa wanaume.Picha: AP

Kenya inajiandaa kuongeza idadi yake ya medali katika fainali ya mbio za mita 1,500 kwa wanaume na mita 5,000 kwa wanawake. Hata hivyo mashindano hayo yaliingia doa baada ya mwanariadha wa pili kutoka Nigeria kupatikana ametumia dawa haramu za kuongeza nguvu mwilini.

Samuel Okon- mwanariadha kutoka Nigeria aliyemaliza katika katika nafasi ya sita mbio za mita 110 kuruka viunzi anakuwa mwanariadha wa pili kutoka Nigeria kugunduliwa ametumia dawa haramu za kuongeza nguvu mwilini aina ya methylexanemine.

Kulingana na mkuu wa mashindano hayo ya Jumuiya ya Madola Michael Fennell chunguzi 1,200 zilifanyiwa wanariadha tofauti na Okon akapatikana ametumia dawa hiyo ya kuongeza nguvu mwilini.

Flash-Galerie Indien Commonwealth Games Delhi 2010
Australia's inaongoza ikiwa na medali 143.Picha: AP

Hiki ni kisa cha pili baada ya mshindi wa medali ya dhahabu katika mita 100 za wanawake ambaye pia ni Mnigeria Osayemi Oludamola kupatikana pia katumia dawa hiyo haramu. Oludamola anasubiri matokeo ya uchunguzi wa pili, utakaoamua iwapo atapokonywa medali yake ya dhahabu.

Na leo Jumanne, ndio siku ya mwisho ya mashindano ya riadha katika michezo hiyo ya Jumuiya ya madola. Wakenya wanajitayarisha kuongeza idadi ya medali pale zitatakapofanyika fainali za mbio za mita 1,500 kwa upande wa wanaume na mita 5,000 kwa wanawake.

Jana ilikuwa siku njema kwa wakenya, pale Richard Meteelong alipowaongoza wakenya wenzake Ezekiel Kemboi na Brimin Kipruto kunyakua medali zote tatu- dhahabu, fedha na shaba katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi.

Indien Commonwealth Spiele Flash-Galerie
Mganda Moses Kipsiro, awapiku Wakenya kuchukua dhahabu katika mita 5000.Picha: AP

Kukosekana kwa bingwa wa dunia katika mbio za mita 800 kwa wanawake, Castor Semenya ilikuwa bahati nzuri kwa wakenya pale Nancy Jebet alipotoa tangazo hata naye ni tosha kwa kunyakua medali ya dhahabu- hii inakuwa medali ya pili kwa Jebet ambaye tayari alikuwa katia kibindoni medali ya dhahabu katika mbio za mita 1,500.

Hata hivyo furaha ya wakenya iliingia kidogo doa, pale Mganda Moses Kipsiro kwa mara nyingine tena alipowanyima Wakenya dhahabu katika mbio za mita 10,000 kwa wanaume.  Wakenya Daniel Salel na Joseph Birech waliopigiwa upatu kushinda walishangazwa na Kipsiro alipomaliza mbio hizo katika muda wa dakika 27, dakika 57 na sekunde 39.

Hii ni mara ya pili Kipsiro anakuwa kero kwa wakenya, mjini New Delhi baada ya kunyakua medali ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 wiki iliopita.

Australia bado inaongoza jedwali la medali- imeshinda medali 143, 64 zikiwa za dhahabu. India ni ya pili ikiwa na medali 76, ilhali Uingereza inafunga tatu bora. Afrika Kusini ambayo ipo katika nafasi ya tano kwa kuwa na medali 32, 12 zikiwa ni  dhahabu- ndio inaorodheshwa ya kwanza barani Afrika. Nigeria inashikilia nafasi ya sita kwa jumla lakini ni ya pili Afrika ikiwa na medali 26, nane zikiwa za dhahabu na Kenya ni ya saba kwa jumla na ya tatu Afrika, ikiwa imejipatia medali 20, 8 zikiwa dhahabu.

Mwandishi: Munira Muhammad/AFPE

Mhariri: Saumu Mwasimba