1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika ya hisani yana mashaka na usalama wa watoto Calais

23 Oktoba 2016

Mashirika ya hisani yamesema yana mashaka juu ya usalama wa watoto na wanyonge kabla ya kubomolewa kwa kambi ya wahamiaji nchini Ufaransa wakati hali ya vurugu ikijitokeza kwa makabiliano kati ya polisi na wahamiaji.

https://p.dw.com/p/2RaTh
Frankreich Calais Ausschreitungen Jungle Flüchtlinge Tränengas
Picha: picture-alliance/AA/C. Thomas

Mashirika ya misaada ya Ufaransa na Uingereza yamekuwa yakilalamika juu ya ukosefu wa taarifa kuhusu mpango wa kuifunga kambi hiyo ya wahamiaj inayolikana kama kambi ya porini huko Calais unaoanza kutekelezwa hapo Jumatatu.

Onyo lao linakuja wakati polisi ikiendelea kupambana na wahamiaji wanaopinga kuvunjwa kwa kambi hiyo ambapo hapo Jumapili watu kadhaa wameonekana wakiwarushia mawe polisi katika taswira zilionyeshwa na kituo cha matangazo cha BFMTV ambapo polisi ilijibu kwa kutumia gesi za kutowa machozi.Hapo Jumamosi polisi ilikabiliana na wahamiaji katika kambi hiyo ilioko katika mji wa Calais ulioko kaskazini mwa Ufaransa.

Ikiwa zimebakia saa chache tu kabla ya kambi hio kuanza kukon'golewa maafisa wamekuwa mbioni kushughulikia mchakato wa kuwahamishia Uingereza vijana wadogo wenye jamaa zao nchini humo.Vijana hao wadogo hupelekwa kwenye kontaina lenye maafisa wa Uingereza wa wizara ya mambo ya ndani ambapo huwapiga picha kwa haraka na kuwafanyia mahojiano mafupi kuamuwa hatima yao.

Watoto 194 watakiwa wawe wameondolewa

Frankreich | Das Flüchtlingslager Calais kurz vor der Schließung - erste Flüchtlinge verlassen den Jungle
Kambi ya wahamiaji ya Calais ilioko kaskazini mwa Ufaransa. Picha: REUTERS/P. Rosignol

Piere Henry wa shirika la hisani la Ufaransa la Terre D'Asile (FTDA) ambalo linahusika katika kusaidia katika mchakato huo kwa niaba ya serikali amesema kwa jumla wamefanya mahojiano 600 wiki hii ambapo vijana wadogo 194 wanatakiwa wawe wameondoka Calais kuelekea Uingereza.

Amesema lengo ni kushughulikia kesi nyingi kadri inavyowezekana kati ya watoto kama 1,300 waliotambulikana katika kambi hiyo wakiwemo 500 wenye jamaa zao nchini Uingereza na baadae kuishawishi Uingereza kukubali wengine wengi kadri inavyowezekana.

Suala hilo ni nyeti.Duru za serikali ya Ufaransa zimeyaelezea mazungumzo hayo na Uingereza kuwa "magumu sana" na kwamba wangelipendelea kuendelea kuzungumza zaidi.

Ni watoto sabini tu wamehamishiwa Uingereza kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu na mapema mwezi wa Oktoba kabla ya kuanza kutekelezwa kikamilifu kwa mpango wa kuibomowa kambi hiyo.

Uingereza imekuwa ikishutumiwa kwa kuburuza miguu katika mchakato huo lakini Ufaransa nayo pia inakoselewa kwa kuukwamisha mchakato huo kwa kushindwa kuwasilisha kesi za kutosha za kuzingatiwa.

Wasi wasi mkubwa

Frankreich | Das Flüchtlingslager Calais kurz vor der Schließung - erste Flüchtlinge verlassen den Jungle
Kambi ya wahamiaji ya Calais kaskazini mwa Ufaransa.Picha: imago/ZUMA Press

Mashirika ya hisani ya Uingereza na wabunge wamemwandikia waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Benard Cazeneuve kufafanuwa kile wanachosema "wasi wasi mkubwa kuhusiana na usalama na hali ya watoto wasioandamana na wazazi wao na watu wazima wanyonge au wasiojiweza.

Mashirika hayo yakiwemo shirika lisilo la kiserikali la Kuwaokowa Watoto la Save the Children ,Baraza la Wakimbizi na Kamati ya Kimataifa ya Uokozi ya Msalaba Mwekundu nchini Uingereza yameandika kwamba "rasilmali zinazotumika hivi sasa hazitoshi kuhakikisha ulinzi wa uhakika kwa watu walioko hatarini kabisa hususan watoto wasioandamana na familia zao."

Baruwa yao imeonya kwamba kuvunjwa kwa kambi bila ya mandalizi makini kutawaweka katika mazingira ya hatari zaidi wale ambao tayari wako hatarini.

Kambi hiyo ya Porini ambayo inawahifadhi maelfu ya wahamiaji wengi kutokea Mashariki ya Kati na Afrika imeshuhudia kuzidi kuongezeka kwa idadi ya wahamiaji katika miezi ya hivi karibuni. Wahamiaji hao huelekea katika kambi hiyo ilioko Calais kwa matarajio ya kingia Uingereza kwa kutumia kivuko au treni inayopita chini ya mkondo.

Mwandishi : Mohamed Dahman /dpa/AFP

Mhariri : Isaac Gamba