1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashtaka ya Mlebanon yaahirshwa hadi Mei 18

11 Aprili 2007

Mashtaka ya watuhumiwa 4 waliopanga njama kuripua mabomu katika magari-moshi 2 nchini Ujerumani imeahirishwa leo huko Beirut hadi Mei 18.

https://p.dw.com/p/CHGY

Kesi ya walibanon 4 wanaoshtakiwa kutaka kuripua bomu katika gari-moshi mjini Cologne,Ujerumani,Julai mwaka jana iliokua ianze leo mjini Beirut,Lebanon, imeahirishwa hadi Mei 18.Hii ni kwa muujibu wa duru za mahkama zilivyoarifu hii leo.

Watuhimiwa 4 waliokuwa korokoroni nchini Lebanon tangu Septemba mwaka jana walifikishwa leo mbele ya Mahkama ya makosa ya kihalifu chini ya ulinzi mkali .

Washtakiwa hao 4 ni mtuhumiwa mkuu Jihad Hamad,Khaled al-Hajj Dib, Ayman Hawwa na Khalil Bubu.

Saddam al-Hajj Dib na nduguye Yusuf Mohammed al Hajj -Dib alietiwa nguvuni Ujerumani, August mwaka jana kwa mashtaka hayo wanashtakiwa bila kuwapo binafsi mahkamani.

Hamad ameungama alipohojiwa kuwa alipachika begi lenye miripuko katika treni nchini Ujerumani Julai mwaka uliopita.

“Azma haikuwa kuua watu ,bali kulipiza kisasi kwa dhara yoyote waliopata waislamu baada ya kuchapishwa nchini denmark kwa vikatuni vya kumdhihaki mtume Muhammad.” Hamad alinukuliwa kuiambia mahkama.

Polisi ya Ujerumani imesema kuchapishwa kwa vikatuni kuhusu mtume Muhammad katika vyombo vya habari vya nchi za magharibi na ulimwengu wa kiarabu, ni chanzo kilichowafanya watuhumiwa hao kupanga njama ya kuripua mabomu katika treni nchini Ujerumani, Julai 31, mwaka uliopita.

Njama hiyo haikufaulu pale mabomu yaliofichwa ndani ya treni 2 za kimkoa kushindwa kuripuka kutokana na hitilafu katika mtambo wao wa kuyafaytua.

Jihad Hammad na Youssef Al Hadsch-Did anaeishi Ujerumani, waligunduliwa katika kamera za kituo kikuu cha gari-moshi mjini Cologne.Wote wawili wakionekana katika kamera wakipachika miripuko hiyo ndani ya treni 2 za kimkoa.

Ni hitilafu tu ya kiufundi iliozuwia kuripuka kwa mabomu hayo.

Al Hajj-Did aliwahi kutiwa nguvuni huku huku Ujerumani wakati mwenzake Jihad Hamad alikamatwa Lebanon na yuko gerezani mjini Beirut.Mtuhumiwa mwenzake anamtuhumu kwamba amepotezwa akili kwa jazba ya kidini.Wakili wake Fawz Zakaria anasema:

“kuwa tayari kwakwe kuelezea njama hiyo ilivyopangwa ni sababu kwanini kijana huyo wa miaka 22 apewe adhabu hafifu.Natumai kifungo cha miaka 3.”

Kwa maoni ya wanasheria wengine mjini Beirut, wanaweza yeye na wenzake 3 wakapewa kifungo cha hadi miaka 15 wakikutikana na hatia.Mahakimu mjini Beirut watahitaji kiasi mwaka mzima kuhukumu kesi hii.Zakaria akasema zaidi:

“Jihad ni kijana aliepotezwa akili na wale waliokua nyuma ya njama hiyo.Hata askari kanzu wa Ujerumani waona hivyo.Hana kabisa mafungamano na Al kaida.”

Mafungamano na kundi la Al kaida hayakugunduliwa hata na wapelelezi nchini Ujerumani.Mwenzake aliekamatwa nae Youssef Al Hadsch-Did na nduguze 2 waqnaotiliwa pia shaka kuhusika ,yamkini wakawa na mafungamano kiasi Fulani na Al kaida.Waliwahi kuwasajili wapiganaji hata kupigana nchini Irak.

Watuhumiwa hao wote 4 wanatoka mjini Tripoli,Lebanon.