1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa sita yakutana kuijadili Iran

2 Septemba 2009

Mataifa matano ya kudumu ya Baraza la Usalama la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani yanakutana kuijadili Iran kuhusiana na mpango wake wa nuklia.

https://p.dw.com/p/JNVV
Umoja wa Mataifa na IranPicha: AP/dpa/DW-Montage

Lakini wakati  mataifa hayo yakikutana leo mjini Frankfurt kujadiliana juu vikwazo vipya dhidi ya Iran,nchi hiyo imetangaza kuwa iko tayari kurejea tena kwenye mazungumzo na mataifa hayo.

Iran inalaumiwa kwa kushindwa kutimiza matakwa ya jumuiya ya kimataifa kuhusiana na mpango wake wa nuklia ambao nchi za magharibi zinahofu kuwa ni dhamira ya kutaka kutengeneza silaha za nuklia.

Mkutano huo ambao unafanyika katika sehemu isiyotajwa lakini kakribu na Frankfurt, unawashirikisha wakurugenzi wa siasa  kutoka  Marekani, Uingereza,Ufaransa, China, Urusi na Ujerumani kujadiliana vikwazo vipya na vikali zaidi dhidi ya Iran kutokana na nchi hiyo kukaidi azimio la Umoja wa Mataifa linaloitaka kusitisha uzalishaji wa uranium, zikihofu kuwa ni kuelekea katika utengenezaji wa bomu la nuklia.

Lakini akizungumza  na waandishi wa habari, mjumbe wa juu wa Iran katika mzozo wa nuklia, Saeed Jalili amesema Iran imepitia upya na kubadilisha mapendekezo ya kurejea tena katika meza ya mazungumzo kwa kutilia maanani hali halisiduniani hivi sasa ikiwa ni pamoja na msukosuko  wa kiuchumi duniani na mzozo wa Georgia.

Hivyo amesema ikitumia  uwezo wake, kitaifa na kieneo, iko tayari kushirikiana ili kuiondolea jumuiya ya kimataifa wasi wasi ambao imekuwa nao.

Said Dschalili / Atomstreit / Iran
Saeed Jalili,Picha: AP

´´Jamuhuri ya Kiislam ya Iran imeandaa mapendekezo mapya na iko tayari kuyawasilisha.Tunatumaini kuwa duru mpya ya mazungumzo itafanyika, tunafikiri tunaweza kuanzisha mazungumzo mapya na ushirikiano mpya kwa amani, haki na maendeleo duniani´´ alisema Jalili

Pamoja na kwamba Saeed Jalili hakusema wazi mapendekezo hayo yatawasilishwa wapi, lakini ni dhahiri kuwa yatawasilishwa kwa nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa mataifa pamoja na Ujerumani, ambazo zimekuwa zikitoa mbinyo mkali dhidi ya Iran.

MAREKANI KUYAJADILI KWA KINA

Marekani ambayo ndiyo kinara wa harakati hizo dhidi ya Iran imeipa nchi hiyo hadi mwisho wa mwezi huu kukubali nafasi iliyotoa ya kuvuta kiti na kurejea katika meza ya mazungumzo, vinginevyo ikabiliwe na vikwazo vikali zaidi.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Robert Gibbs akizungumzia juu ya tamko hilo la Iran, amesema kuwa hawajaarifiwa rasmi

Naye msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Ian Kelly amesema watayapokea na kuyahakiki kwa umakini mapendekezo hayo ya Iran

´´Tutayapatia mapendekezo yoyote watakayotuletea kwa umakini mkubwa kabisa, na katika hali ya kuheshimiana.Tutayapokea majibu yoyote yanayotekelezeka ya serikali ya Iran kwa kamati ya nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama pamoja Ujerumani ambayo April mwaka huu ilitoa mwaliko kwa Iran wa kukutana ana kwa ana´´

Kauli hiyo ya Iran imekuja siku moja tu baada ya Rais Nicolasu Sarkozy wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kuionya kuwa itakabiliwa na vikwazo vikali zaidi iwapo itashindwa kurejea tena katika meza ya majadiliano.

IRAN YAPUNGUZA KITISHO

Nalo Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomik IAEA katika utafiti wake limebaini kuwa Iran imeanza kupunguza uzalishaji wa uranium na kukubali kuwepo kwa ufuatiliaji wa karibu wa mtambo wake wa nuklia.

El Baradei scheidet aus dem Amt
Mohammed el BaradeiPicha: picture-alliance / dpa

Katika mahojiano yaliyochapishwa hapo jana Mkuu wa shirika hilo la IAEA Mohamed El Baradei amesema kitisho kutoka Iran ni suala ambalo limetiwa chumvi mno na kwamba hakuna ushahidi kuwa nchi hiyo itakuwa na silaha za nuklia hivi karibuni.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP

Mhariri:Abdul-Rahman