1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa sita yataka nafasi katika baraza la usalama la UM

Kalyango Siraj17 Oktoba 2008

Uganda inagombania nafasi ya kanda ya Afrika

https://p.dw.com/p/Fbu3
Moja wa vikao vya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.Uganda nayo inataka kukaa katika baraza hilo.Picha: AP

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linawachagua wanachama wapya watano ambao si wa kudumu katika baraza lake la usalama leo Ijumaa .Viti hivyo vitano vinagombaniwa na mataifa saba mkiwemo Uganda.

Uganda, taifa kutoka eneo la Afrika Mashariki linagombania kiti hicho kwa kutumia tiketi ya kanda ya Afrika. Kiti hicho kilikuwa kinashikiliwa na Afrika Kusini.

Gazeti la serikali ya Uganda la kila siku 'The New Vision', katika toleo lake jipya, limesema kuwa uwezekano wa Uganda kuchaguliwa ni mkubwa kwani haina mpinzani.Lakini ili kufanikiwa ni lazima iungwe mkono na mataifa matano ambayo yana viti vya kudumu katika baraza la usalama.Nayo ni Marekani, Urusi,Ufaransa, Uingereza,pamoja na China.

Mataifa ambayo hujiunga na baraza hilo lenye uwezo wa kuiwekea nchi yoyote vikwazo aidha vya kiuchumi au silaha na pia kutuma vikosi vya kulinda amani katika taifa linayokiuka sheria za Umoja wa Mataifa,hukaa katika baraza hilo kwa kipindi cha miaka miwili kunzia Januari mosi.

Uganda sio taifa pekee miongoni mwa yanayowania nafasi katika baraza hilo ambayo haina mpinzani,bali Mexico nayo haina mpinzani kutoka kanda ya mataifa ya Amerika yanayozungumza kilatino.Kiti kimekuwa kinakaliwa na Panama.

Mataifa mengine yanayogombania nafasi ni Austria,Iceland,Iran, Japan na Uturuki. Kati ya hayo mataifa yanayotarajiwa kupata upinzani ni Iran na Iceland.Iran ambayo inagombania nafasi ya kanda ya bara la Asia inashindana na Japan.

Iran ni miongoni mwa mataifa anzilishi ya Umoja wa Mataifa mwaka wa 1945 imewahi kukaa katika baraza hillo mara moja tu kuanzia mwaka wa 1955 hadi 1956.Na mpinzani wake Japan imeka katika kiti hicho kwa kipindi cha miaka 18 tangu mwaka wa 1956.

Lakini Iran ambayo imewekewa vikwazo na baraza hilo kutokana na mpango wake tatanishi wa Nuklia, inatarajiwa kupoteza kwa Japan ambayo ni taifa lenye uchumi imara kuliko yote katika bara hilo, na pia hutoa mchango mkubwa wa takriban asili mia 20 kwa bajeti ya Umoja wa Mataifa.Isitoshe mataifa ya magharibi yanaweza kuipendelea Japan kuliko Iran ambayo ni maadui.Kiti hicho kimekuwa kinadhibitiwa na Indonesia.Iran inasema haijawahi kukaa katika baraza hilo kwa kipindi cha miaka 52.

Viti viwili ambavyo vimetengwa kwa yanayoitwa mataifa ya magharibi na mengine, mkiwemo Australia na New Zealand ,vinagombaniwa na Austria, Iceland na Uturuki. Mataifa yanayoondoka ni Italy pamoja na Ubeligiji.Tatizo la Iceland ni kuporomoka kwa uchumi kutokana na mgogoro wa kifedha unaoendelea.

Wanadipolomasia wanasema kuwa Uturuki yaweza ikapata kiti labda kutokan na kuungwa mkono na mataifa ya kiislamu.

Muundo wa baraza la usalama la umoja wa Mataifa haujabadilika sana tangu mwaka wa 1945. Wajumbe ambao si wa kudumu katika baraza hilo kama vile Libya,Burkina Faso,Costa Rica,Croatia na Vietnam watabaki hadi mwisho wa mwaka wa 2009.

Baraza la usalama huwa linawanachama 15,watano wakiwa wa kudumu ilhali wegine 10 hubadilishwa kila baadaya kutumikia miaka miwili.