1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yanayoinukia kiuchumi yamebadilisha wizani wa nguvu za kiuchumi duniani

Sekione Kitojo12 Novemba 2010

Mvutano kuhusu vita vya kibiashara pamoja na sarafu viligonga vichwa vya habari katika mkutano wa G20 lakini wizani wa uwezo wa sauti unabadilika pia.

https://p.dw.com/p/Q7Tc
Rais Barack Obama akikutana na kansela wa Ujerumani Angela Merkel. mataifa makubwa tajiri yanapoteza uwezo wao wa kulazimisha mada katika medani ya kimataifa.Picha: AP

Mivutano  kuhusu   vita  vya  kibiashara  pamoja  na   sarafu vilikuwa  vikigonga   vichwa  vya  habari  katika   mkutano wa  siku  mbili  wa  kundi  la  mataifa  ya  G20, lakini  suala kuu  ni  jinsi  mambo  yanavyobadilika  na kutoa  kwa  nchi zinazoendelea  sauti  kubwa  zaidi  katika  meza  ya kimataifa   ya  majadiliano.

Mabadiliko  haya  ya  nguvu  yanakisiwa  katika  taarifa  ya pamoja  iliyotolewa   baada  ya  mkutano  huo  wa  kundi  la mataifa  ya  G20  uliomalizika  jana  Novemba  12, na kuonyesha  kuwa  wajumbe  wamekubaliana  kupanga ajenda  elekezi  pamoja  na  hatua  za   kuzuwia upunguzaji  wa  thamani  za  sarafu  ambao  unaleta  athari badala  ya  malengo  yaliyopangwa, ambayo  kwa  kawaida huweka  mbinyo  mkubwa   kwa   mataifa  yanayoendelea.

Wito  wa  Marekani  kuweka  viwango  maalum  katika ziada  za  mauzo  ya  biashara, ambao  haukupendelewa na  China  nchi ambayo   ina  ziada  ya  karibu  dola  bilioni 272  haukuidhinishwa  na  mkutano  huo  wa  G20.

Badala  yake  viongozi  wa  kundi  hilo  la  G20  wamesema katika  taarifa  yao  ya  pamoja   baada  ya  mkutano  wao kuwa  wataandaa  muongozo  wenye  viashirio   kadha ambavyo  vitasaidia   kugundua  na  mapema  uwiano mkubwa  usio kuwa  sawa  wa  kiuchumi  ambao unapaswa  kuchukuliwa   hatua  za  kuzuiwa  pamoja  na kusahihishwa.

Rais  Barack Obama  amesema kuwa  amemwambia   rais wa  China,  Hu Jintao,  kuwa  mataifa  yanayoinukia kiuchumi  yanahitaji  sarafu  zao   kuendeshwa  na  masoko na  kwamba  Marekani  itaangalia  kupanda  kwa  sarafu  ya Yuan , ambayo  maafisa  wa  China  waliruhusu  kupanda kidogo  tu  katika  miezi  michache  iliyopita.

Mataifa  mengine  yanayoinukia  kiuchumi  kutoka   Brazil hadi  Thailand, yameachia  sarafu  zao  kupanda   katika kiwango  cha  juu  cha  miaka  15  iliyopita, kasi  ambayo imesababisha   benki  kuu  kuweka  aina  mbali  mbali  za udhibiti  wa  mitaji.

Utaratibu  katika  mkutano  wa  mwaka  huu  wa  G20  uko katika  sura  ya  ambapo  mataifa  yenye  uchumi  unaokua kwa  haraka  katika  nchi  zinazoendelea , kama  China  na India , wanachukua  jukumu  la  injini  ya  kuendesha uchumi  wa  dunia  wakati  mataifa   ya  asili  yenye   nguvu , ikiwa  ni  pamoja  na  Marekani  na  Japan , yanazuiwa  na ukuaji wa  taratibu.

Mkutano  wa  Seoul  umeonyesha  vipi  maafikiano yanavyoweza  kwenda   sambamba   na  madai   ya mataifa  yanayoinukia  kiuchumi  katika  makubaliano  ya mwisho, amesema  profesa  Kenzaburo Ikeda, mkuu  wa taasisi  ya  utafiti  ya  Taijyu.

Ikeda , ambaye  pia  amekuwa  akifuatilia  mikutano  ya kundi  la  G7  kama  afisa , anasema   kuwa  matokeo  ya mkutano  huo    ni  kwamba  mataifa  tajiri   hayawezi  tena kuchukua  jukumu  la  ukarimu, zikitoa  fedha  na kupunguza  deni  la   nje, kwa  mfano  kama  vile walivyokuwa   wakifanya   kwa  mataifa  masikini yanayoendelea.

Lakini  kuna  hisia  kubwa  miongoni  mwa   nchi zinazoinukia  kiuchumi  kuwa  bado  zinahitaji  msaada  na kusababisha   hali  ambapo  madai   katika  meza  ya majadiliano  mjini  Seoul  yalikuwa  hayalingani, anafafanua mwanauchumi  Kensuke  Kubo, mtaalamu  kuhusu  uchumi wa   India  ambaye  yuko  katika  taasisi  ya  nchi  zenye uchumi  unaoinukia.

Mwandishi : Sekione  Kitojo / IPS    

Mhariri: Othman  Miraji.