1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matarajio ya usalama wa chakula Afrika Mashariki yanafifia

Kabogo Grace Patricia24 Septemba 2009

Hayo yameelezwa na wataalamu wa kilimo cha misitu ambapo wanapendekeza upandaji miti kama suluhisho la tatizo hilo.

https://p.dw.com/p/Jo7p
Mti wa Mfenesi nchini Uganda.Picha: DW/Helle Jeppesen

Matarajio ya usalama wa chakula katika eneo la Afrika Mashariki kwa mwaka huu yanafifia kufuatia kukosekana kwa mvua, ambapo inafifisha kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao huku wakikabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa barani Afrika. Wataalamu wa kilimo cha misitu wanasema upandaji wa miti linaweza likawa suluhisho la tatizo hilo.

Tayari watu milioni 20 wanategemea msaada wa chakula katika eneo la Afrika Mashariki na Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO), linahofia kuwa idadi hiyo inaweza ikaongezeka katika maeneo mengine ya bara hilo. Mavuno yaliyovunwa yamepungua kwa asilimia 50 chini ya kiwango katika baadhi ya maeneo ya Pembe ya Afrika. Bei ya mahindi kwa Uganda na Kenya imeongezeka mara mbili katika miezi 24 iliyopita.

Kitengo cha Utafiti wa virutubishi cha FAO nchini Somalia, kimeeleza kinahofia kuwa nchi hiyo itakabiliwa na mzozo mbaya wa kibinaadamu kwa miaka 18, huku watu milioni 3.6 wakiwa wanahitaji msaada wa chakula. Madhara yatokanayo ha uhaba wa mvua yamesababishwa na mizozo na kutawanyika kwa watu katika eneo hilo.

Mwezi Agosti, mwaka huu wanasayansi waliokutana mjini Nairobi, Kenya katika kongamano la pili la dunia la misitu, walipendekeza upandaji wa miti kama hatua ya mwisho ya kupatikana kwa suluhisho la usalama wa chakula. Dennis Garrity, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Dunia cha Misitu chenye makao yake mjini Nairobi, amesema wataalamu wa misitu wamekuwa wakishuhudia kwa miaka mingi jitihada zinazofanywa na wakulima wa Afrika wakijaribu kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia rasilimali walizonazo.

Upandaji wa miti aina ya Faidherbia na miti mingine kunaweza kuwapatia wakulima vyanzo vingine vya mapato kutokana na mbao, mkaa, matunda, mbegu za mafuta au mazao ya kilimo kama vile kakao, kahawa, chai au mpira. Stephen Carr, aliyekuwa Afisa Kilimo wa Benki ya Dunia katika eneo la Kusini mwa jangwa la Sahara, amesema wamekuwa wakifanya majaribio na miti ya Faidherbia nchini Malawi tangu mwaka 1989, lakini haikuwa na mafanikio makubwa sana. Afisa kilimo huyo anasema miti inahitaji karibu miaka 25 ili kukua vizuri na iimarike kama utapanda kwa ajili ya watoto wako. Hata hivyo, Carr ana wasi wasi kuwa kilimo cha misitu hakiwezi kuenea kwa haraka na kukidhi mahitaji ya idadi ya watu ya Afrika inayoongezeka. Akitolea mfano Malawi afisa kilimo huyo anasema hekari milioni tatu za kilimo wamefanikiwa kupanda miti katika eneo la hekari 2,100. Anasema miti hiyo inaweza kusaidia katika miaka ya baadaye, lakini wananchi wanahitajika kulishwa kwa sasa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (IPS)

Mhariri: Abdul-Rahman