1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matayarisho kwa msimu mpya yapamba moto

Admin.WagnerD18 Julai 2016

Maandalizi ya ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga yamepamba moto, Borussia Dortmund yaelekea barani Asia kwa michezo ya kirafiki dhidi ya Manchester United na Manchester City .

https://p.dw.com/p/1JR0l
Bundesliga Dortmund gegen Wolfsburg
Wachezaji wa Borussia Dortmund wakishangiria baoPicha: Getty Images/AFP/S. Schurmann

Matayarisho kwa ajili ya msimu wa 2016 2017 katika Bundesliga yameshika kasi, ambapo timu zote zimeingia kambini na zinacheza michezo ya majaribio karibu kila siku.

Mabingwa watetezi Bayern Munich baada ya kupata huduma ya kocha nyota , aliyepachikwa jina la Mr. Champions league, Carlo Anceloti, imeanza mazowezi wiki moja iliyopita, lakini tayari imepata mshituko baada ya mchezaji wake mahiri Arjen Robben kuumia katika mchezo wa majaribio na timu ya daraja la chini ya Lippstadt.

FC Bayern München Vorstellung Trainer Carlo Ancelotti
Kocha wa Bayern Munich Carlo AncelotiPicha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 ambaye amecheza mara 15 tu katika msimu uliopita , alipachika wavuni bao moja katika mchezo wa majaribio ambapo Bayern ilishinda kwa mabao 4-3, wakati kocha Carlo Anceloti akiwa kwa mara ya kwanza anaiongoza timu hiyo.

Borussia Dortmund makamu bingwa katika Bundesliga msimu uliopita, inaondoka kesho Jumanne kwenda nchini China ambako itakuwa na ziara ya siku 9, na kucheza michezo miwili kuwania kombe la kimataifa dhidi ya Manchester United siku ya Ijumaa na kisha itapambana na kikosi cha kocha mpya wa Manchester City Pep Guardiola siku mbili baadaye.

Arjen Robben
Arjen Robben wa BayernPicha: picture-alliance/dpa/S. Simon

Borussia Dortmund ambayo imepungukiwa na nguvu zake muhimu kikosini kwa kuwakosa mchezaji wa kati mtaalamu Ilkay Gundogan ambaye amejiunga na Manchester City msimu ujao, Henrick Mkhtarian aliyehamia Manchester United na mlinzi Mats Hummels aliyetimkia Bayern Munich , inaundwa na kikosi cha wachezaji wa zamani na vijana wapya ambao wanaonekana kuwa na uwezo mkubwa , wachanga , lakini pia wakitokea katika ligi mbali mbali za Ulaya.

Je ziara ya China ilikuwa ni muhimu kwa Borussia Dortmund wakati huu ambapo kikosi chake kina majina mapya zaidi na kinahitaji mazowezi ya pamoja zaidi?. Hili ni swali ambalo wadadisi wengi wa masuala ya soka wanalijadili, wakidokeza kwamba Dortmund ilipaswa kuingia kambini na kuwapa wachezaji wao wapya nafasi ya kufahamu mbinu za kocha Thomas Tuchel badala ya kucheza michezo hiyo mikubwa na safari hiyo ndefu.

Deutschland Mkhitaryan mit Hummels und Gündogan
Wachezaji wa Borussia DortmundPicha: Getty Images/AFP/T. Kienzle

Wachezaji wapya wa Dortmund wanahitaji muda kuweza kutambua mbinu za kocha wao na uchezaji wa jumla wa kikosi hicho. Katika Wakati Bundesliga itakapoanza tarehe 26 mwezi ujao, hakutakuwa na wakati wa kurekebisha makosa yaliyopo, na hii inaweza kusababisha msimu ukawa mbaya kwa Borussia na kuwakatisha tamaa wachezaji hao vijana waliongia kwa madhumuni ya kuonesha vipaji vyao.

Tayari hali ya mambo haiko salama kutokana na michezo ya Euro 2016 iliyomalizika mwezi huu nchini Ufaransa. Wengi wa wachezaji wa timu za taifa waliomo katika kikosi cha Borussia hawatarejea mapema kujiunga na wachezaji wenzao kufanya mazowezi. Kwa hiyo watakapofika watakuwa na muda mfupi kabla ya kujichanganya kikosini.

Hilo ni tatizo lililoikumba Borussia Dortmund mwaka 2014-15 wakati ilipokaribia kushuka daraja na hata kocha wao nyota Juergen Klopp kuachia ngazi. Msimu huu umeanza na kombe la mataifa ya Ulaya na kikosi kipya zaidi ya mwaka 2014 baada ya kombe la dunia kule Brazil.

Juventus kugharamika zaidi

Mabingwa wa Italia Juventus Turin nao wakiwa wanajitayarisha kwa ajili ya msimu ujao inatarajia kuikamua akaunti yao ya benki na kuchomoa kiasi cha euro milioni 94 ili kupata huduma ya mshambuliaji kutoka Napoli Gonzalo Higuan , zinaeleza ripoti kutoka Italia hii leo.

SSC Neapel vs. Bayern München Flash-Galerie
Gonzalo Higuan wa Napoli akishangiria katikatiPicha: dapd

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 alipachika wavuni mabao 36 msimu uliopita na kuvunja rekodi iliyowekwa na Gunnar Nordahl iliyodumu kwa muda wa miaka 66 ya mabao 35 wakati mshambuliaji huyo akivalia jezi ya AC Milan, aliyoiweka mwaka 1950.

Sasa mshambuliaji huyo kutoka Argentina anatarajiwa kuvunja mioyo ya mashabiki wa Napoli kwa kujiunga na mahasimu wao wakubwa Juventus , katika makubaliano ambayo yanaweza kushuhudia Juventus ikitoa wachezaji kadhaa mbali ya kulipa kitita hicho ili kumpata Higuan kutoka SSC Napoli.

Antonio Conte

Nae kocha mpya wa Chelsea Antonio Conte amethibitisha kwamba winga Juan Cuadrado atarejea katika klabu hiyo baada ya kuazimwa kwa mwaka mmoja na mabingwa wa Italia Juventus Turin.

UEFA EURO 2016 Italien vs Irland +++ Trainer Conte verzweifelt
Kocha wa Chelsea Antonio ContePicha: Reuters/G. Fuentes

Mshambuliaji huyo kutoka Colombia , ambaye alijiunga na Juve kutoka Chelsea Agosti mwaka jana, alipata mabao manne katika michezo 28 ya ligi msimu uliopita na kuisaidia klabu hiyo ya seria A kunyakua ubingwa na kombe la Italia Coppa Italia.

Wakati huo huo kocha wa Juventus Turin Massimiliano Allegri anaamini Paul Pogba atabakia katika kikosi hicho licha ya mazungumzo juu ya mchezaji huyo wa kati Mfaransa kuhamia England ama Uhispania.

Pogba ambaye mkataba wake na Juve unamalizika mwaka 2019, amehusishwa na kurejea katika klabu ya Premier League ya Manchester United ama mabingwa wa Champions League Real Madrid.

Mchezaji bora wa Ulaya

Cristiano Ronaldo na mchezaji mwenzake katika timu ya Real Madrid Gareth Bale wamo katika orodha ya wachezaji 10 waliotangazwa leo Jumatatu kwa ajili ya tuzo ya UEFA ya mchezaji bora barani Ulaya.

Frankreich Euro 2016 Finale Frankreich gegen Portugal Tor Eder
Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na UrenoPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Ronaldo alifunga penalti ya mwisho ya ushindi katika mpambano wa Champions League dhidi ya majirani zao wa Atletico Madrid na aliiongoza Ureno kunyakua taji la kwanza la ubingwa wa Ulaya katika michuano ya Euro 2016 nchini Ufaransa mwezi huu.

Mlinzi wa Ureno na Real Madrid Pepe pia yumo katika orodha hiyo pamoja na Gareth Bale wa Wales aliyeiongoza timu yake ya taifa kufikia nusu fainali ya Euro 2016.

Ronaldo anapigiwa upatu kushinda taji hilo kwa mara ya pili, baada ya kulipata katika msimu wa 2013-14 ambapo atakuwa sawa na mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi.

Antoine Griezmann wa Atletico Madrid nae yumo katika orodha hiyo baada ya mabao yake sita katika Euro 2016 kumpatia tuzo ya mchezaji bora wa mashindano hayo pamoja na kiatu cha dhahabu, licha ya Ufaransa kukwama katika fainali dhidi ya Ureno.

Messi ni mmoja kati ya wachezaji wa Barcelona kuingia katika orodha hiyo pamoja na Luis Suarez, wakati wachezaji wawili wa Bayern Munich Manuel Neuer na Thomas Mueller , mlinda mlango wa Juventus Gianluigi Buffon na mchezaji wa kati wa Real Madrid Mjerumani Toni Kroos pia wamejumuishwa.

Wachezaji hao walichaguliwa na waandishi habari kutoka mataifa 55 wanachama wa UEFA ambao watapiga kura kwa mara ya pili Agosti 5 kuamua wachezaji watatu watakaoingia katika fainali.

Mshindi wa tuzo hiyo atatangazwa mjini Monaco Agosti 25 wakati makundi yatakayoshiriki kombe la mabingwa barani Ulaya yatapangwa.

Kombe la shirikisho barani Afrika , Yanga yahitaji miujiza

TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ililazimisha sare ya bila kufungana na Mouloudia Bejaia ya Algeria jana Jumapili na kubakia kileleni mwa kundi A katika kombe la shirikisho barani Afrika.

Mazembe mabingwa mara tisa wa vikombe barani Afrika, ina pointi 7 baada ya michezo mitatu.

Bejaia ina pointi 5, Medeama ya Ghaba ina pointi mbili na Dar Young Africans ya Tanzania ina pointi moja wakati imebakia michezo mitatu na nafasi mbili zinawaniwa katika nusu fainali.

Mazembe inaonekana kuwa na nafasi nzuri ya kunyakua moja kati ya nafasi hizo mbili.

Matumaini ya Medeama bado yako hai , baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Yanga mjini Dar es Salaam siku ya Jumamosi.

Iwapo Medeama itaishinda Yanga nyumbani Julai 26 na Bejaia ikipoteza mchezo wake na Mazembe mjini Lubumbashi , timu hizo za Ghana na Algeria zitafungana kwa pointi wakati michezo miwili ikibakia.

Katika kundi B , FUS Rabat iliishinda Kawkab Marrakesh siku ya Ijumaa kwa mabao 3-1, mabingwa Etoile Sahel ya Tunisia iliichapa Al Ahly ya Tripoli kwa mabao 3-0.

Riadha Rio

Kwa upande wa riadha, ripoti inayotarajiwa kutolewa leo kuhusiana na madai ya matumizi makubwa ya madawa yanayoongeza nguvu za misuli kwa wachezaji , doping , nchini Urusi tayari imezusha mtikisiko na inaweza kuzusha sababu za msingi za kuipiga marufuku Urusi kushiriki katika michezo ya Olimpiki ya mjini Rio.

Richard H. McLaren
Richard McLaren mwanasheria wa CanadaPicha: picture-alliance/dpa/S.Hoppe

Wakati michezo hiyo inatarajiwa kuanza rasmi Agosti 5 , chini ya wiki tatu kuanzia sasa, matarajio ya ripoti hiyo itakayotolewa na mwanasheria wa Canada Richard McLaren inaiweka jamii ya wanamichezo wa olimpiki katika wasi wasi mkubwa. Baadhi ya viongozi wa michezo duniani wamekosoa kile wanachoona kuwa ni adhabu jumla kwa wengine kutaka Urusi ipigwe marufuku kabla ya kutolewa taarifa hiyo leo.

McLaren amepewa jukumu na shirika la kupambana na madawa hayo duniani WADA kufanya uchunguzi wa madai yaliyotolewa na mkurugenzi wa zamani wa maabara ya kupambana na madawa hayo nchini Urusi Grigory Rodchenkov baada ya kuandika katika gazeti la New York Times mwezi Mei .

kocha wa timu ya wanamasumbwi wa Urusi Aleksandr Lebzyak alipouwa akizungumza na wanamichezo hao baada ya mashindano ya kutea wachezaji watakaokwenda Rio ameonesha matumaini ya timu ya taifa ya Urusi kushiriki mashindano hayo.

"Unafahamu kwamba,hali ni ya utata hivi sasa , lakini tuko pamoja kwa hiyo ninaamini kwamba kila kitu kitakuwa sawa , tutakwenda katika michezo ya Olimpiki na tutashinda medali zote. Kila la kheri kwenu nyote na ahsanteni saan"

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga