1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mateka 20 wauwawa 13 waokolewa Bangladesh

2 Julai 2016

Vikosi vya Bangladesh vimeuvamia mkahawa mmoja mjini Dacca mapema Jumamosi (02.07.2016) na kuwauwa wanamgambo sita wenye silaha waliokuwa wakiwashikilia mateka watu 13 na kuwauwa wengine ishirini wakiwemo wageni.

https://p.dw.com/p/1JHz1
Picha: picture-alliance/dpa

Vikosi vya Bangladesh vimeuvamia mkahawa mmoja mjini Dhaka mapema Jumamosi (02.07.2016) na kuwauwa wanamgambo sita wenye silaha waliokuwa wakiwashikilia mateka watu 13 na kuwauwa wengine ishirini wakiwemo wageni.

Jeshi awali lilisema watu wote ishirini waliouwawa walikuwa ni wageni lakini inaaminika sasa kwamba kulikuwa pia na raia miongoni mwa waliouwawa wakati wa mzingiro wa mkahawa huo na mapambano yaliofuatia yaliyodumu kwa saa 10.

Takriban watu 35 walichukuliwa mateka Ijumaa usiku wakati watu waliokuwa na silaha walipouvamia mkahawa huo mashuhuri wa Holey Artisan Bakery katika eneo la Gulshan mjini Dacca ambayo ni kanda ya kibalozi wakati wa mwezi wa Ramadhan.Polisi wawili waliuwawa mwanzoni mwa shambulio hilo.

Vikosi vya kijeshi ambavyo vilifanya operesheni ya uokozi wakati wa asubuhi na kuwauwa washambuliaji sita viligunduwa vifaa vya miripuko na silaha za ncha kali katika eneo hilo.

Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina amelaani shambulio hilo ambalo kundi la Dola la Kiislamu limedai lina mkono wake.Amesema kutokana na juhudi za vikosi vyao magaidi hao hawakuweza kukimbia na kwamba mmoja amekamatwa.

Dini yao ni ugaidi

Katika hotuba iliyoonyeshwa na televisheni ameapa kwamba watapambana na mashambulizi ya wanamgambo nchini humo na kuwahimiza watu kujitokeza.Hasina amesema "Mtu yoyote mwenye kuamini dini hawezi kutenda hayo.Hawana dini yoyote dini yao ni ugaidi."

Polisi wakichukuwa hatua za usalama baada ya kuvamiwa kwa mkahawa na watu waliokuwa na silaha Dhaka.
Polisi wakichukuwa hatua za usalama baada ya kuvamiwa kwa mkahawa na watu waliokuwa na silaha Dhaka.Picha: picture alliance/AA/H. Chowdhury

Serikali ya Japani imesema mateka mmoja wa Kijapani ameokolewa akiwa na jeraha la risasi lakini wengine saba hawajulikani walipo.Katibu wa Baraza la Mawaziri Koichi Hagiuda amesema raia wao hao wanane walikuwa pamoja mkahawani wakati wa shambulio hilo.

Imeelezwa kwamba Wataliana tisa ambao pia walikuwepo mkahawani wakati ulipokuwa ukishambuliwa wameuwawa.

Luteni Kanali Tuhin Mohammad Masud kamanda wa kikosi cha Kuchukuwa Hatua Haraka ambacho ndicho kilichoendesha operesheni hiyo amesema Wasrilanka wawili pia waliokolewa na kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani ya nchi miongoni mwa waliokolewa kuna raia mmoja wa Argentina.

Kundi la Dola la Kiislamu limedai kuhusika na shambulio hilo kwa mujibu wa Kundi la Kijasusi SITE ambalo linafuatilia harakati za kundi hilo la jihadi mtandaoni.Shirika la habari la Amaq lenye mafungamano na kundi la Dola la Kiislamu pia limeweka picha inazodhaniwa kuonyesha miili ya mateka.Udhati wa picha hizo haukuweza kuthibitishwa.

Mateka walipembuliwa

Rezal Karim baba wa mfanyabiashara wa Bangladesh ambaye ameokolewa pamoja na familia yake amesema washambuliaji hawakumdhuru mtu yule ambaye alikuwa akiweza kukariri aya za kitabu kitukufu cha Waislamu Quran.

Wananchi wakimsadia majeruhi baada ya kuvamiwa kwa mkahawa na watu waliokuwa na silaha Dhaka.
Wananchi wakimsadia majeruhi baada ya kuvamiwa kwa mkahawa na watu waliokuwa na silaha Dhaka.Picha: picture-alliance/AP Photo

Serikali haikuzunngumzia moja kwa moja juu ya madai ya kuhusika kwa kundi la Dola la Kiislamu lakini huko nyuma imekuwa ikikanusha kwamba kundi hilo lenye makao yake nchini Iraq na Syria liko nchini Bangladesh na badala yake kulaumu upinzani kwa mashambulizi yaliokuwa yakifanyika hivi karibuni nchini humo.

Mashambulizi ya karibuni nchini humo yamekuwa yakizusha hofu kwamba wafuasi wa itikadi kali za kidini wamekuwa wakizidi kujiimarisha nchini humo licha ya nchi hiyo kwa jadi kuwa haijiegemezi katika misimamo ya kidini na ilikuwa na stahmala.

Shambulio hilo ni kupamba moto kwa ukatili wa matumizi ya nguvu ya wanamgambo ambayo yameikumba nchi hiyo ndogo yenye idadi kubwa ya Waislamu ambao kwa jadi ilikuwa ya Uislamu wa msimamo wa wastani. Mashambulizi ya huko nyuma yalihusisha wanaume wenye mapanga waliokuwa wakiwaandama wanaharakti binafsi,wageni na watu wa jamii ya wachache.

Serikali ya Hasina iliwasaka Waislamu wa itikadi kali nchini humo na kuwatia mbaroni kadhaa.Imewashutumu magaidi wa ndani ya nchi na vyama vya upinzani hususan chama cha kizalendo cha Bangladesh Nationalist na washirika wao chama cha itikadi kali cha Kiislamu Jamaat -e-Islami kwa kupalilia matumizi hayo ya nguvu ili kuiyumbisha nchi hiyo madai ambayo vyama vyote viwili vinayakanusha.

Mhariri : Mohamed Dahman /AP/Reuters

Mhariri : Sylvia Mwehozi