1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya kura ya maoni ya Ulaya na mkutano mkuu wa CDU

Oumilkheir Hamidou
6 Desemba 2016

Kishindo cha matokeo ya uchaguzi nchini Italy na Austria kwa nchi za Umoja wa Ulaya,na mkutano mkuu wa chama cha Christian Democratic Union-CDU mjini Essen ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa magazetini

https://p.dw.com/p/2To88
Italien Referendum
Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Borgia

Tuanzie lakini kwa kuchambua matokeo ya uchaguzi nchini Austria na Italy na kishindo chake kwa nchi za Umoja wa ulaya."Kwa bahati nzuri ushindi wa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia  si jaala ya Mungu" linaandika gazeti la mjini Cottbus "Lausitzer Rundschau " na kuendelea: "Ingawa nchini Italy kura ya maoni ya mageuzi ya katiba imemalizika vibaya kama ilivyokuwa ikitarajiwa. Hata hivyo katika nchi jirani ya Austria,wapiga kura wamezusha maajabu ya furaha walipojitambulisha moja kwa moja na Umoja wa Ulaya. Matokeo hayo hayakuwa yakitegemewa watu wakizingatia kilichotokea Uingereza na kura ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya Brexit pamoja na kuchaguliwa Donald Trump kuwa rais wa Marekani. Hata  hivyo litakuwa kosa kisiasa watu wakitulia tu na kuangalia. Kwasababu hata Austria takriban kila mpiga kura wa pili amependelea kuizungushia kuta nchi hiyo. Ushindi mkubwa wa demokrasia ya kiliberali hauwi hivi. Ndio maana mnamo wiki na miezi inayokuja, Angela Merkel atakuwa anaangazia kwa hisia za mchanganyiko yanayotokea.

Imani ya wananchi kwa Umoja wa Ulaya yapunguwa

Gazeti la mjini Dresden "Säshsischer Zeitung" linachambua matokeo ya kura ya maoni ya Italy na kuandika: "Kilichotokea Italy ni onyo kwa Umoja wa Ulaya. Ingawa hakuna sababu ya kutokea mzozo mwengine wa kanda ya Euro  au kujitoa Italy na umoja wa sarafu.Yote mawili ingekuwa sawa na kutia chunvi. Hata hivyo kushindwa kura ya maoni ni sawa na wito wa kutaka ibadilishwe mbinu ya kukabiliana na mizozo ndani ya kanda ya Euro. Mbinu za kale hazitoshi kuipatia ufumbuzi mizozo ya kiuchumi na kijamii,si Italy,si Ufaransa na wala si Ugiriki. Kura ya maoni dhidi ya Renzi ni ishara pia ya kupotea haraka imani ya wananchi kuelekea Umoja wa ulaya,ambao hauna jibu la kukabiliana na mizigo ya madeni isipokuwa kutoa wito wa kufunga mkaja,kuhifadhi benki badala ya nafasi za kazi za wananchi na kuziacha pekee yao nchi wanaachama kukabiliana na matatizo mfano wa ile ya wakimbizi.

Angela Merkel hatopata mteremko safari hii katika mkutano mkuu wa chama chake cha CDU

Chama cha Christian Democratic Union-CDU kinakutana kwa mkutano wake mkuu mjini Essen. Mwenyekiti wa chama hicho,kansela Angela Merkel hatokuwa na kazi rahisi,linaandika gazeti la "Osnabrücker Zeitung". "Wana Christian Democrats wamechoshwa kusema hewala kila wakati. Mikutano iliyoitishwa mikoani  miezi ya hivi karibuni imedhihirisha jinsi watu walivyochoshwa na uamuzi wa mtu mmoja: "Merkel anabidi ang'atuke", kauli hiyo ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD, limedakwa na baadhi ya wanachama wa CDU.Yaonyesha zimekwisha zile zama ambazo, katika zoezi la kumchagua mwenyekiti wa chama hicho,kansela Merkel hujikingia asili mia 96.7. Lakini kwakua wana CDU ni watu wa anri,mwenyekiti anaweza kutegemea matokeo ya kuridhisha. CDU kinasalia na kitaendelea kuwa kongamano la kansela na anaefaidika na hali hiyo ni Angela Merkel.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef