1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza inasubiri matokeo ya kura ya maoni

23 Juni 2016

Hali nchini Uingereza inaonekana kuwa ya utulivu wakati ambapo wananchi wanayasubiri kwa hamu matokeo ya kura ya maoni waliyopiga leo iwapo nchi hiyo ibakie au ijiondoe kwenye Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1JC2w
Picha: DW/S. Shackle

Wananchi wa Uingereza bado wanaendelea kujitokeza katika vituo vya kupigia kura ili kurusha karata yao ya mwisho kabisa katika kura hiyo ya maoni ambayo ni ya kihistoria. Hata hivyo, inaelezwa kuwa wasiwasi kutokana na hali mbaya ya hewa pamoja na radi na mafuriko kwenye mji wa London na kusini-mashariki mwa England, unaweza kuathiri zoezi zima la upigaji kura.

Vituo kadhaa vya kupigia kura katika jiji la London vimehamishiwa sehemu nyingine kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha usiku kucha. Baadhi ya vituo vimechelewa kufunguliwa kwa sababu mafuriko hayo yalisababisha matatizo ya usafiri kwa maafisa kadhaa wa uchaguzi.

Wapiga kura wakisubiri kwenye foleni
Wapiga kura wakisubiri kwenye foleniPicha: Reuters/N. Hall

Akizungumza baada ya kupiga kura yake, kiongozi wa chama cha United Kingdom Independence-UKIP, Nigel Farage, anayepinga Uingereza kubakia katika Umoja wa Ulaya amesema anaamini watashinda lakini yote hayo yatatokana na idadi ya watu watakaojitokeza.

''Niliitaka sana kura hii katika maisha yangu yote ya utu uzima, kwa sababu nilikuwa na umri wa miaka 11 tu wakati tulipiga kura ya maoni kuhusu suala hili. Kwa hiyo, nina hamu sana ya kusikia matokeo ya kura hii,'' amesema Farage.

Farage ana matumaini watashinda

Farage amesema kuna dalili nzuri kwamba Waingereza watapiga kura ya kutaka Uingereza ijiondoe kwenye Umoja wa Ulaya. Matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutangazwa mapema kesho asubuhi, huku ikielezwa kuwa matokeo rasmi yatatangazwa mida ya saa moja kamili jioni.

Wakati huo huo, masoko ya fedha duniani na wanasiasa duniani kote wameendelea kuifatilia kwa karibu kura hiyo ya maoni ya Uingereza, ambapo Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema ana matumaini Waingereza watachagua kubakia kwenye Umoja wa Ulaya.

Kiongozi wa UKIP, Nigel Farage
Kiongozi wa UKIP, Nigel FaragePicha: DW/L. Scholtyssyk

Merkel amesema angetamani ufanyike mkutano wa nchi zote wanachama wa umoja huo kujadili mustakabali wake, badala ya mkutano wa nchi sita tu ambazo ni waanzilishi, au wanachama wa kanda inayotumia sarafu ya Euro.

Amesema mkutano kuhusu mustakabali wa Umoja wa Ulaya unapaswa kufanyika katika hali ya utulivu na uishirikishe Uingereza, hata kama wapiga kura wake wataamua kujiondoa katika umoja huo.

Aidha, Merkel anatarajia kukutana na Rais wa Ufaransa, Francois Hollande kabla ya mkutano huo wa kilele, uliopangwa kufanyika siku ya Jumanne. Mkutano wa viongozi hao wawili kuhusu kura ya maoni ya Uingereza, utafanyika siku ya Jumatatu mjini Berlin.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTR,DPA,AP
Mhariri: Yusuf Saumu