1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya Uchaguzi wa Comoro

23 Desemba 2009

Viti 19 kwa kambi ya Rais Sambi

https://p.dw.com/p/LBJ2

Kufuatia duru ya pili ya uchaguzi visiwani Comoro, taarifa kutoka mji mkuu Moroni, zinasema kwamba chama-tawala cha rais Ahmed Abdallah Sambi,kimeshinda viti 19 kati ya 24 vya Bunge la Shirikisho la visiwa hivyo.Matokeo hayo yalitangazwa jana na waziri wa maswali ya uchaguzi, Hassan Ahmed el-Barwan, siku 2 tu baada ya duru ya pili ya uchaguzi.

USHINDI MKUU KWA KAMBI YA SAMBI

Kambi ya Rais Ahmed Abdullah Sambi, imejinyakulia viti 19 vilivyo chaguliwa moja kwa moja wakati vyama vya Upinzani vimeondokea na viti 5 tu pamoja na vyote 3 vya kisiwa cha Moheli,kisiwa kidogo kabisa kati ya 3 vinavyounda Shirikisho la Comoro.Mawaziri wengi wa serikali ya sasa ya rais Sambi, wamechaguliwa tena wakati waziri wa zamani wa mambo ya nje Ibrahim Ali Mzimba na waziri mkuu wa zamani Bianrifi Tarmidi, ni miongoni mwa sura mpya za wajumbe wa Upinzani Bungeni,mjini Moroni.Shirikisho la visiwa vya Comoro, linalo jumuisha visiwa 3 tu wakati huu,linatoa haki kwa kila kisiwa kuwa na rais wake :Ngazija, Nzouani na Moheli.

BUNGE LA SHIRIKISHO:

Bunge la Shirikisho la visiwa hivyo 3, lina wabunge 33 na 24 tu kati yao , huchaguliwa moja kwa moja na wapiga kura .Viti 9 vilivyosalia , vinachaguliwa na Baraza la kila kisiwa . Mageuzi ya kikatiba ili kumwezesha rais kutawala kipindi cha miaka 5 badala ya 4, yamesha pitishwa,lakini sehemu ya Upinzani, inadai kwamba , sheria hiyo mpya haimhusu rais wa sasa Sambi .

Rais Sambi,kutoka kisiwa cha Nzouani, ana umri wa miaka 51 na alichaguliwa 2006 katika kile wachunguzi wanacho kiona ni ,"mabadiliko ya kwanza ya amani ya madaraka visiwani Comoro".Kwani, visiwa vya Comoro , katika historia yake tangu kujitangazia uhuru 1975,vimejionea mapinduzi ya kijeshi au majaribio ya mapinduzi 19 na mizengwe mingi katika uchaguzi.

KABLA UHURU 1975:

Kabla kujitangazia uhuru huo,Comoro ilikuwa ni visiwa 4-cha nne ni Mayotte, ambacho mapema mwaka huu ,kiligeuka rasmi milki ya n'gambo ya Ufaransa . Na kupitia kura ya maoni,kimegeuka pia sehemu ya Umoja wa Ulaya, ingawa kwa mlango wa nyuma,kwavile, Ufaransa ni mwanachama wa Umoja huo.

Rais Sambi, anaejiandaa kwa awamu mpya, alipata elimu yake nchini Saudi Arabia,Sudan na Iran,ambayo kwa usuhuba wake mwema na nchi hiyo, amepewa jina la "Ayatolah wa visiwa vya Comoro."

Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE

Uhariri:Mwadzaya,Thelma