1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya Uchaguzi, Zimbabwe yaendelea kutolewa.

Nyanza, Halima31 Machi 2008

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu Zimbabwe yanazidi kutolewa, huku chama cha upinzani cha MDC kikichuana vikali na chama tawala.

https://p.dw.com/p/DXz6
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, tayari mawaziri wake wawili wamepoteza viti vyao katika matokeo ya awali yaliyotangazwa leo.Picha: AP

Kufuatia matokeo hayo ya awali yaliyotolewa leo, Mawaziri wawili wa serikali ya Rais Robert Mugabe, tayari wameshapoteza viti vyao, huku kukiwa na wasiwasi wa kufanyika kwa hila za wizi wa kura, kutokana na kucheleweshwa kwa matokeo hayo, katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ambao unaonesha kutoa changamoto kubwa kwa Rais Mugabe.

Mawaziri hao wa serikali ya Rais Mugabe waliopoteza viti vyao, ni Waziri wa sheria wa nchi hiyo Patrick Chinamasa na Waziri anayeshughulika na masuala ya umma Chen Chimutengwende.

Matokeo yanaonesha kuwa chama cha upinzani cha MDC na Chama tawala cha ZANU PF, vikichuana vikali kwa kuwa na viti 19 kila moja kati ya viti 210 vya bunge la nchi hiyo.

Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha MDC ambacho kinadai kupata ushindi, Tendai Biti amesema matokeo hayo yanaonesha wazi jinsi watu wa nchi hiyo walivyochoka utawala wa kidikteta.

Polisi wa kutuliza ghasia, wamekuwa wakifanya doria huku gazeti la serikali, likitoa ripoti inayolaumu chama cha upinzani cha MDC kuandaa wafuasi wake, kufanya ghasia kutokana na matokeo yasiyo rasmi ambayo wanadai kuwapa ushindi.

Serikali ya nchi hiyo, jana ilitoa onyo kufuatia taarifa zinazotolewa za ushindi zisizo rasmi na kusema kuwa Tume ya Uchaguzi nchini humo peke yake ndiyo inamajukumu ya kutangaza matokeo hayo.

Rais Robert Mugabe amelaumu vikwazo vilivyowekwa na nchi za magharibi kuhujumu uchumi wa nchi hiyo, na amepinga kuwepo kwa wizi wa kura katika zoezi hilo.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini humo George Chiweshe amesema kucheleweshwa kwa matokeo hayo kunatokana na kuwepo na uzito wa uchaguzi huo kwa mara ya kwanza ambao unajumuisha uchaguzi wa Rais, bunge na serikali za mitaa, kauli ambayo inaungwa mkono na Chriss Meroleng kutoka Taasisi ya masuala ya Usalama iliyoko mjini Pretoria Afrika kusini, ambaye anasema Tume ya Uchaguzi nchini Zimbabwe kwa mara ya kwanza imekuwa ikiendesha chaguzi nne tofauti kwa mara moja, Uchaguzi wa Rais, seneti, uchaguzi wa bunge na wa serikali za mitaa.

Anasema hali hiyo imesababisha mzigo mkubwa kwa tume hiyo ndio maana kuna kuwepo kwa kucheleweshwa kwa matokeo kutolewa.

Hata hivyo kwa upande mwingine, upinzani umekuja na hoja kwamba ucheleweshaji huo unatokana na jaribio la serikali kutaka kuiba kura ili matokeo yapendelee chama tawala cha ZANU PF.

Bwana Meroleng amesema mitazamo hiyo miwili inaweza kuwa chanzo cha kucheleweshwa kutolewa kwa matokeo hayo.

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nchi za nje wa Uingereza David Miliband amesema hakuna sababu yoyote ya kuchelewesha kutolewa kwa matokeo hayo.

Katika taarifa yake amesema Jumuia ya Kimataifa inafuatilia kwa karibu matokeo hayo.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uingereza ameongeza kusema kuwa Zimbabwe itakabiliwa na hali mbaya katika siku zijazo.

Naye Msemaji wa Kamisheni ya Ulaya ametaka kutolewa kwa matokeo hayo haraka ili kuepuka mawazo yasiyo ya lazima.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa waangalizi wa uchaguzi huo kutoka Jumuia ya SADC amesema zoezi la upigaji kura lilienda kwa amani.

Uchaguzi wa mwaka huu umempa changamoto kubwa Rais Mugabe kutokana na kugombea tena kiti hicho cha Urais huku nchi yake ikikabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi, na pia mbali na kupata ushindani kutoka kwa mpinzani wake mkubwa Morgan Tsvangirai, ameweza kupewa changamoto pia kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Fedha wa nchi hiyo Simba Makoni.


Uchaguzi huo umefanyika huku nchi hiyo ikikabiliwa na uhaba wa chakula, mafuta na ugonjwa hatari wa ukimwi ambao unachangia kudidimia kwa uchumi wake.


Rais Robert Mugabe aliyeongoza nchi hiyo toka ilipopata uhuru amekuwa akikilaumu chama kikuu cha upinzani nchini humo cha MDC kwamba ni kibaraka wa nchi za magharibi.