1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miito ya kutunza zaidi mazingira

19 Mei 2015

Mkutano wa kimataifa wa mazingira unafanyika mjini Berlin, kujaribu kuweka sawa masuala kadhaa yenye utata kuelekea mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi, utakaofanyika mjini Paris mwishoni mwa mwaka huu.

https://p.dw.com/p/1FRr0
Petersberger Klimadialog
Picha: picture-alliance/dpa/B. Pedersen

Mawaziri 35 kutoka duniani kote wanahudhuria mkutano huo wa siku mbili unaojadili tabianchi mjini Berlin. Ni mkutano usiyo rasmi wa maadalizi ya mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi. Akifungua mkutano huo wa 16 wa Petersberg siku ya Jumatatu, waziri wa mazingira wa Ujerumani Barbara Hendricks alisema vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni wajibu wa kimaadili wa kizazi cha sasa.

"Wajibu wa kimaadili kwa vizazi ambavyo tutavirithisha dunia yetu, na wajibu wa kimaadili kwa watu ambao tayari wameathiriwa na dhoruba, mafuriko, ukame na umaskini," alisema waziri Hendrick kutoka chama cha SPD. Kansela wa Ujeurmani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Francoise Hollande, wanazungumza katika mkutano huo na kulipa suala hilo uzito zaidi kwa kuwepo kwao.

Rais wa Ujerumani Joanchimi Gauck aliwapokea washiriki wa mkutano huo siku ya Jumatatu. "Sote tunaitambua dunia hii kuwa ndiyo nyumbani kwetu," alisema rais Gauck na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukuwa hatua za maksudi kulinda mazingira.

Mabadiliko yasiowezekana

Hii leo wanasayansi wanakubaliana juu ya ukubwa wa kitisho kinachotokana na mabadiliko ya tabianchi. Wakati hakuna moja anaweza kusema hasa mbadiliko hayo yatafananaje, waziri wa mazingira wa Ujerumani Hendricks anaamini kuwa mabadiliko hayo yatakuwa magumu sana kwa watu ikiwa joto dunia halitabakia kwenye kiwango cha nyuzi mbili za celsius. "Kanuni ya matumaini-kulingana na kaulimbiu ya "haitakuwa mbaya sana" - haiwezi kuwa mkakati. Kinyume chake: Tunapaswa kushirikiana kuongeza kasi."

Rais wa Ufaransa Francoise Hollande na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika mkutano wa mazingira wa Pertersberg mjini Berlin.
Rais wa Ufaransa Francoise Hollande na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika mkutano wa mazingira wa Pertersberg mjini Berlin.Picha: T. Schwarz/AFP/Getty Images

Lengo la mkutano wa Paris ni kupata mkataba mpana na unaozifunga nchi zote duniani na ambao utaanza kutekelezwa ifikapo mwaka 2020. Waziri wa mambo ya nje ya Ufaransa Laurent Fabius ambaye ataongoza mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris, na kwa hivyo kuwa kwake mjini Berlin kama mwenyekiti mwenza, anasisitiza kuwa "laazima tuje na matokeo." Lakini hilo ni rahisi kudai kuliko kutekelezwa. Mkataba mpya wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi unapaswa kuridhiwa na mataifa yote duniani. Hakuna hata moja kati ya wanachama 190 wa UN anaepswa kuukataa. Hii ni sheria iliyoplekea kushindwa kwa Mkutano wa Copenhagen.

Tambua mstari mwekundu

Lilikuwa janga la kisiasa lililozaa mkutano wa mazingira wa Pertersberg. Tangu mwaka 2010, mkutano huo unafanyika kila mwaka na unatumiwa kuimarisha dhana kuhusu uwezekano wa malengo ya kisiasa na kutambua misitari miekundu, ambayo mataifa hayataki kuivuka. Lakini Mkutano wa majadiliano ya tabianchi pia ni jukwaa ambako mashinikizo ya kisiasa yanafanyika. Kufikia majira ya joto, kila nchi inapaswa kuwasilisha mikakati yake ya ulinzi wa mazingira. Lakini mpaka sasa, ni mataifa 37 tu, yakiwemo ya Umoja w Ulaya, ambayo yameweka wazi mikakati yao ya utunzaji mazingira, ambayo inapaswa kujumlishwa katika mkataba ujao kimataifa wa tabianchi.

Japokuwa sehemu kubwa ya mipango ya utunzaji mazingira bado haijawasilishwa, inaonekana wazi kuwa michango ya kitaifa kwa upunguzaji wa hewa ya ukaa angani haitoshelezi kufikia shabaha ya kiwango cha joto la nyuzi mbili za celsius. Waziri Laurent Fabius tayari ameonya juu ya kushindwa kwa Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa wa tabianchi. "Hali ni ya kutisha, tunapswa kuishughulikia haraka." Kila moja anapaswa kufahamu wazi kuwa hakuna mpango mwigine.

Waziri wa Mazingira wa Ujerumani Barbara Hendricks akihutubia mkutano wa mazingira wa Petersberg.
Waziri wa Mazingira wa Ujerumani Barbara Hendricks akihutubia mkutano wa mazingira wa Petersberg.Picha: Reuters/F. Bensch

Ujerumani bado haifanyi vya kutosha

Wahifadhi wa mazingira na pia wanasiasa wa upinzani wanaitaka serikali ya Ujerumani kuonyesha dhamira zaidi na pia kutoa uongozi katika sera ya mazingira. "Kati ya hizi, mpaka sasa hakuna hatua za maana zilizochukuliwa," alisema Jürgen Trittin, mbunge wa chama cha watetezi wa mazingira cha die Grüne. "Ujerumani sasa haiko katika nafasi ya kuweza kueleza ni namna gani itafikia kiwango cha nyuzi joto mbili." Ili kutimiza malengo hayo, Ujerumani itapaswa kuhifadhi ziada ya tani milioni 70 za gesi chafu kila mwaka. Kulingana na utafiti wa shirika la mazingira la Green Peace, hilo litawezekana tu baada ya kufungwa kwa mitambo 35 ya zamani ya kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe.

Madai kama hayo hata hivyo siyo ya walio wengi na mtazamo kuelekea Paris ni wa matarajio madogo. Lakini kuna matumaini madogo kwamba mkutano wa majadiliano wa Petersberg utakuwa na nguvu fulani ya ushawishi. Suala hili linahusiana pia na fedha, na haijulikanibado iwapo mataifa yaliyoendelea kiviwanda yatatimiza ahadi yake ya kuzipatia nchi maskini kiasi cha dola bilioni 100 kuanzia mwaka 2020 kwa ajili ya utunzaji mazingira. Ahadi hizi bado hazijasainiwa.

Waziri wa mazingira wa Ujerumani alifafanua juu ya mambo yanayotangulizwa mbele ya utunzaji mazingira, yakiwemo miongoni mwa mengine, maslahi ya kiuchumi. Ili kuvuka vikwazo hivyo vyote inahitaji muda. Paris haitakuwa kituo cha mwisho, kwa maneno hayo, pengine waziri wa mazingira wa Ujerumani atazuwia kuvunjika moyo. Utunzaji mazingira una safari ndefu. "Katika mbio ndefu za nyika, ni kweli kwamba siyo wote wanaanza kwa mwendo sawa. Baadhi huongeza kasi kadiri muda unavyokwenda."

Mwandishi: Kinkartz Sabine
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman