1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya amani Kenya

9 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D4u7

Nairobi:

"Serikali ya Kenya na Upande wa upinzani wamekubaliana haja ya kufikiwa makubaliano ya kisiasa ili kuufumbua mzozo ulioko"-matamshi hayo yametolewa na mpatanishi wa Umoja wa Afrika,katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.Bwana Annan amesema anataraji matokeo ya maana yatapatikana hadi mapema wiki ijayo.

"Sote tumekubaliana kwamba ufumbuzi wa kisiasa unahitajika" amesema bwana Kofi Annan katika mkutano wa waandishi habari baada ya mazungumzo yaliyodumu saa moja pamoja na rais mteule Mwai Kibaki na mpinzani wake,Raila Odinga.

Wakati huo huo serikali ya Kenya imetangaza kuondowa marufuku ya mikutano ya hadhara,ikisema hali ya usalama imeanza kuimarika.Wizara ya mambo ya ndani imeshauri mikutano ya hadhara itumike hivi sasa kuhimiza amani na suluhu ya taifa.

Akizungumzia maafa yaliyotokea tangu matokeo ya uchaguzi wa rais yalipotangazwa,rais Mwai KIbaki amesema:

"Kwa muda wa mwezi mzima,tumeshuhudia matumizi ya nguvu ambayo hayajawahi kutokea,matumizi ya nguvu yaliyogharimu maisha,yaliyosababisha machungu,usumbufu,uharibifu na dhiki kwa wengi miongoni mwa wananchi ".

Watu zaidi ya elfu moja wanasemekana wameuwawa na zaidi ya laki tatu kuyapa kisogo maskani yao tangu december 27 iliyopita.